Tafuta

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri Tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii watafsiriwa katika lugha ya Kirussi. Papa Francisko atuma ujumbe wa pongezi. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: "Frateri Tutti: Yaani "Wote Ni Ndugu": Kuhusu Udugu na Ufariki wa Kijamii watafsiriwa katika lugha ya Kirussi. Papa Francisko atuma ujumbe wa pongezi. 

Waraka wa Kitume Wa Papa Francisko: "Fratelli tutti: Kirussi

Kwa tafsiri hii, Waraka huu sasa unaweza kusomwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu unaotaka kujielimisha na yale yaliyoandikwa humo. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha furaha yake kubwa kwamba, tafsiri ya Waraka huu imewahusisha hata wajumbe wa Jukwaa la Wanasayansi wa Kiislam Kimataifa “Muslim International Forum”. Muhimu: Majadiliano ya Kidini na Kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” umegawanyika katika sura nane: Sura ya Kwanza: Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu: Wingu jeusi ambalo limetanda duniani. Hapa anagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Sura ya Pili ni kuhusu wageni njiani, Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Sura ya Tatu ni kuhusu mwono wa ulimwengu wazi, sehemu hii inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sura ya Nne, Moyo uliofungukia ulimwengu wote, hapa changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Sura ya Tano, ni kuhusu siasa safi zaidi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”. Sura ya Sita inajikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana.

Katika sura ya Saba, Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Sura ya Nane inakita maudhui yake katika dini na udugu; umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili. Mwishoni wa Waraka huu wa kitume, Baba Mtakatifu anagusia mambo msingi yanayofumbatwa katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Kituo cha Kitamaduni cha “Porvovskie vorota” nchini Urussi, Jumatano tarehe 3 Machi 2021 kimezundua Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliotafsiriwa kwa lugha ya Kirussi. Hili limekuwa ni tukio ambalo limezama katika mchakato wa majadilino ya kidini, kutokana uwakilishi mkubwa wa viongozi wa kidini kutoka Urussi na kwa upande wa Kanisa chini ya uongozi wa Askofu mkuu Giovanni D’Aniello, Balozi wa Vatican nchini Urussi. Ni tukio ambalo limepambwa pia na uwepo wa viongozi wa Makanisa nchini Urussi na hivyo kupata pia chapa ya majadiliano ya kiekumene. Kazi ya kutafsiri imefanywa na Kampuni ya “Medina” kwa kushirikiana na Wajumbe wa Jukwaa la Wanasayansi Waislam Kimataifa chini ya uongozi wa Shirikisho la Waislam Urussi. Waraka huu ni mfululizo wa Nyaraka maalum zinazojikita katika majadiliano ya kidini.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wa matashi mema na shukrani kwa habari za kusisimua kwamba, Waraka wake umetafsiriwa katika lugha ya Kirussi na kwamba, unazinduliwa rasmi tarehe 3 Machi 2021. Kwa tafsiri hii, Waraka huu sasa unaweza kusomwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu wanaotaka kujielimisha na yale yaliyoandikwa humo. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha furaha yake kubwa kwamba, tafsiri ya Waraka huu imewahusisha hata wajumbe wa Jukwaa la Wanasayansi wa Kiislam Kimataifa “Muslim International Forum”. Tafakari na majadiliano juu ya maudhui yaliyomo kwenye Waraka huu wa Kitume inaweza kuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene na hata kwa familia ya binadamu katika ujumla wake.

Kwa kweli, katika ulimwengu wa utandawazi, kunamwingiliano mkubwa wa watu na matukio. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi juu ya maudhui yaliyomo kwenye Waraka huu wa Kitume yanaweza kuwa ni msaada mkubwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kunogesha umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja na kuishi kweli kama ndugu wa Baba mmoja. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka wanapoendelea kuchota amana na utajiri kutoka katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”.

Fratelli Tutti
03 March 2021, 15:01