Tafuta

Tarehe 25 Machi ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Hii pia ni Siku ya Injili ya Uhai na Utakatifu wa maisha. Tarehe 25 Machi ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Hii pia ni Siku ya Injili ya Uhai na Utakatifu wa maisha. 

Siku ya Injili ya Uhai na Utakatifu wa Maisha: Fumbo la Umwilisho

Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Mungu, ili kupyaisha tena mang’amuzi na utambuzi katika dhamiri za watu, familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake, tunu msingi ya maisha ya binadamu katika hatua zake zote, tangu pale anapotungwa mimba na katika hali mbalimbali za maisha yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 25 Machi ya kila mwaka anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, mwanzo wa Fumbo la Umwilisho. Hii ni siku ya Injili ya Uhai na Utakatifu wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Kuna uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Umwilisho na utume wa familia. Kadiri ya mpango wa Mungu, Yesu Kristo alizaliwa na kukulia katika familia ya binadamu iliyoundwa na Yosefu pamoja na Bikira Maria. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Machi 2021 amewakumbusha watu wa Mungu nchini Poland kwamba, Bunge la Poland kunako mwaka 2004 lilipitisha sheria ya Maadhimisho ya Siku ya Utakatifu wa Maisha.  Kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Mungu, ili kupyaisha tena mang’amuzi na utambuzi katika dhamiri za watu, familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake, tunu msingi ya maisha ya binadamu katika hatua zake zote, tangu pale anapotungwa mimba na katika hali mbalimbali za maisha yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, waamini wanahimizwa kuonja uwepo wa daima wa Bikira Maria katika maisha yao, na kwamba, kamwe hawezi kuwatelekeza, bali atawafariji na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Kanisa linapoadhimisha Siku ya Uhai, linapenda kukazia umuhimu wa: maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu alipenda kuibariki familia na kuipatia dhamana ya kuendeleza kazi ya uumbaji; ili kweli iweze kuwa ni Jumuiya ya maisha na upendo katika moyo wa jamii. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inajenga na kudumisha utamaduni wa uhai kwani huu ni urithi wa binadamu wote. Ni mwaliko wa kusoma na kutafakari kwa mara nyingine tena, amana, utajiri na urithi mkubwa ulioachwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Injili ya Uhai, “Evangelium vitae” iliyochapishwa tarehe 25 Machi 1995. Huu ni ujumbe endelevu kwani Mama Kanisa anatambua na kuthamini haki, utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, yaani tarehe 25 Machi, Kanisa sehemu mbali mbali za dunia linatafakari kuhusu Injili ya Uhai kwa sala na shuhuda mbali mbali.

Huu ni mwendelezo wa mafundisho ya kina kuhusu Injili ya uhai yaani: Maisha ya mwanadamu yaliyotolewa na Mtakatifu Paulo VI, “Humanae vitae” pamoja na Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu: Wajibu wa Familia za Kikristo katika Ulimwengu mamboleo: “Familiaris consortio”. Waamini wanahamasishwa kusimama kidete kutangaza Injili ya Uhai, Injili ya Familia na kukataa katu katu kumezwa na utamaduni wa kifo. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa kukumbatia kweli za Kiinjili na Kanuni maadili kama zilivyobainishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II: “Mng’ao wa ukweli” Veritatis splendor”. Nyaraka zote hizi za Mama Kanisa zinalenga kutetea na kuendeleza Injili ya Uhai kwa kuheshimu na kuthamini uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Mama Kanisa amezindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Lengo kuu la Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni kujitahidi kumwilisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka ili kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani. Familia ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu.

Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha.

Siku ya Maisha
24 March 2021, 15:42