Tafuta

Sakramenti ya Upatanisho ina umuhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali pa kukimbilia huruma, upendo na msamaha wa Mungu, tayari kuanza upya kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Sakramenti ya Upatanisho ina umuhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali pa kukimbilia huruma, upendo na msamaha wa Mungu, tayari kuanza upya kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. 

Sakramenti ya Upatanisho Katika Maisha na Utume wa Kanisa: Huruma

Tema zilizofundishwa ni kuhusiana na maisha na utume wa Kipadre kama Mhudumu wa Sakramenti ya Upatanisho. Waungamishaji bora ni wale wanaowasaidia waamini wao kuonja huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya. Toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha ni kati ya changamoto kubwa zinazotolewa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kwa sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sakramenti ya Upatanisho ni mahali ambapo mwamini anakimbilia kiti cha huruma ya Mungu ili kuungama, apate kugangwa na kuiponya roho yake. Ili hatimaye, aweze kupata afya bora zaidi ya maisha ya kiroho kwa kuzamishwa katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kitovu cha maungamo ni upendo wa Mungu ambao mwamini anaupokea na ambao anauhitaji daima. Ni Kristo Yesu mwenyewe ambaye anawasubiri, anayewasikiliza na kuwasamehe waamini dhambi zao. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba: Kwenye moyo wa Mungu, binadamu anatangulia kuliko makosa yake. Toba na wongofu wa ndani unafumbatwa katika: kufunga, sala na sadaka. Toba huleta msamaha na upatanisho na Kanisa. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Kristo Yesu alitaka Kanisa lake lote kabisa, katika sala, maisha na utendaji wake, liwe ni ishara na chombo cha msamaha na upatanisho ambao amewastahilisha wanadamu kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Kanisa ni mhudumu wa Upatanisho. Muundo wa Sakramenti ya Upatanisho unasimikwa katika maisha ya mwamini anayeongoka kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa: kujuta dhambi, kuziungama na kutimiza malipizi.

Tendo hili linakamilika kwa njia ya mjumbe wa Kanisa, anayetoa msamaha wa dhambi kwa jina la Kristo Yesu na kuamua aina ya malipizi yanayopaswa kutendwa. Padre muungamishi husali na kufanya toba kwa ajili ya mdhambi. Na hivyo mkosefu huponywa na kurudishwa katika ushirika na Kanisa. Rej. KKK. N. 1430-1450. Idara ya Toba ya Kitume inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama "Penitenzieria Apostolica” chini ya uongozi wa Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu pamoja na Monsinyo Krzysztof Jòzef Nykiel, Hakimu ya Idara ya Toba ya Kitume imekuwa ikiendesha kozi maalum kwa ajili ya mapadre waungamishaji pamoja na majandokasisi wanaojiandaa kuwa ni wahudumu wa mafumbo ya Kanisa. Kozi hii kuanzia tarehe 8-12 Machi 2021 imekuwa ikiendeshwa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, kwa ushiriki wa wajumbe zaidi ya 900. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaopyaisha imani kwa kuchota maji hai kutoka katika matumaini, yanayomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani, anayewawezesha wote kujisikia kuwa ni ndugu wamoja!

Hija ya Kipindi cha Kwaresima inanogeshwa na mwanga wa Ufufuko ambao huchochea mawazo, mitazamo na maamuzi ya wafuasi wa Kristo Yesu. Kufunga, kusali na matendo ya huruma ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Njia ya ufukara, kwa kufunga na upendo kwa maskini pamoja na sala ni mambo yanayowawezesha waamini kuishi kiaminifu imani yao, matumaini na upendo wa kweli. Ndiyo maana kozi hii inaendeshwa wakati wa Kipindi cha Kwaresima. Katika Sakramenti ya Upatanisho, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujizamisha kwenye upendo wa Mungu unaoganga na kuponya; kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, ili kwa njia ya upendo wake wa daima, aweze kuwaletea waja wake wongofu wa ndani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hatimaye, kunafsisha upendo huu kwa Mungu na jirani kama kielelezo cha imani tendaji. Mapadre waungamishaji watambue na kukiri kwamba, kwanza kabisa wao ni wadhambi, wameonjeshwa huruma na msamaha wa Mungu. Kumbe, wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma na msamaha wa Mungu kwa waja wake. Waamini wajenge tabia na utamaduni wa kujipatanisha na Mungu na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa kozi ya XXXI Kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, Ijumaa tarehe 12 Machi 2021.

Monsinyo Krzysztof Jòzef Nykiel, Hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume anasema kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, mwaka huu, kozi hii imefanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Tema zilizofundishwa ni kuhusiana na maisha na utume wa Kipadre kama Mhudumu wa Sakramenti ya Upatanisho. Mapadre wanakumbushwa kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, kumbe, wanapaswa kufundwa ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Waungamishaji bora ni wale wanaowasaidia waamini wao kuonja huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya. Toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha ni kati ya changamoto kubwa zinazotolewa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama zinavyobainishwa katika Nyaraka zake zilizotolewa hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha! Watakatifu walikuwa na mapungufu na dhambi zao binafsi, lakini wakathubutu kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Utakatifu ni hija ya maisha mbele ya Mwenyezi Mungu inayofumbatwa katika ujasiri, matumaini na uthubutu kwa kuamini kwamba, neema ya Mungu inaweza kuwaongoza kufikia hatima yake, yaani kuonana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujizatiti katika utakatifu wa maisha, hata wanapokuwa wagonjwa kitandani hawawezi kitu! Wanapokuwa kazini wakichakarika kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa uaminifu, uadilifu huku wakiwajibika barabara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu yameendelea kupyaisha: maana na umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha na utume wa Kanisa.

Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho na wongofu wa ndani unaodai toba na malipizi ya dhambi, ili hatimaye, kukiri sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa binadamu mdhambi. Ni kwa njia ya Sakramenti hii, mwamini hupata msamaha na amani rohoni mwake, baada ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zake. Lengo kuu la Sakramenti ya Upatanisho ni upatanisho na Mungu pamoja na Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; hapa ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.  Hii ni Sakramenti inayopania kujenga na kudumisha mahusiano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu. Hivi karibuni, Idara ya Toba ya Kitume imetoa angalisho kuhusu umuhimu wa kuzingatia “Siri ya Maungamo katika Sakramenti ya Upatanisho na katika maongozi ya maisha ya kiroho” yanayomfunga mhudumu kimaadili, kwani hata katika huduma hii, Mama Kanisa anatekeleza kwa dhati kabisa utume unaookoa. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni matukio ambayo yanamwonesha Kristo Yesu kuwa ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti.

Sakramenti ya Upatanisho
15 March 2021, 14:49