Tafuta

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya safari zake za kitume iliyo sheheni changamoto nyingi, lakini kwa kujiaminisha mbele ya Mungu na kwa maombezi ya Bikira Maria, akapiga moyo konde na kwenda huko Iran. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya safari zake za kitume iliyo sheheni changamoto nyingi, lakini kwa kujiaminisha mbele ya Mungu na kwa maombezi ya Bikira Maria, akapiga moyo konde na kwenda huko Iran. 

Papa Francisko: Vipaumbele vya Maisha na Utume Ndani ya Kanisa

Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, tarehe 19 Machi 2013, Papa Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mt. Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo: Maskini, Amani, Mazingira na sasa Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 19 Machi 2021 anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki, Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu, aliyezaliwa kwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yosefu akamwita jina lake Yesu, maana Yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao na kutambuliwa kisheria kuwa ni Mwana wa Ukoo wa Daudi, Mwana wa Ibrahimu, Baba wa imani. Mtakatifu Yosefu aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi mwaminifu wa Nyumba ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu sanjari na kukubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake, kama alivyoambiwa na Malaika wakati akiwa usingizini. Akamchukua Bikira Maria kama mchumba wake. Katika hali ya hatari, alimchukua Mtoto na Mama yake Bikira Maria, wakakimbilia Misri na kukaa huko hata alipofariki Herode, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema, “Kutoka Misri nalimwita mwanangu”. Rej. Mt 1: 1-25; 2: 1-23.

Amani na utulivu viliporejea tena, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ikarejea tena Nazareti. Baada ya tafakari ya kina, Papa Pio IX kunako mwaka 1870 akamtangaza Mtakatifu Yosefu kuwa ni Mlinzi wa Kanisa la Kiulimwengu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko akatangaza Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu. Papa Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 akazindua maadhimisho haya yanayotarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika katika ndoto!

Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hawa pia ni wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa adhimu kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa; tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa. Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa maisha ya kiroho na kimwili, dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayotenga, nyanyasa na kuwabagua maskini. Kwa sasa tofauti msingi kati ya watu, kimekuwa ni chanzo cha kinzani, migogoro na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kwa kuthamini, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma kama ulivyofunuliwa na Kristo Yesu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawe ni wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema, wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa: unyenyekevu, ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, umoja na mshikamano wa binadamu.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, na kwa mara ya kwanza imeadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbu kumbu endelevu ya huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika ujumla wao. Siku hii ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini. 

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, anazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ekolojia vinavyohusiana na watu; Ekolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ekolojia na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote anakazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, amekazia kuhusu umuhimu wa diplomasia ya Vatican kufumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anapembua utamaduni wa udugu wa kibinadamu kama chombo cha ujenzi wa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kubainisha njia itakayotumika na malengo yake katika uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ujenzi wa ushirikiano na mafungamano yanayokita mizizi yake katika maendeleo na ushirikiano katika masuala ya kiuchumi kwa kuzingatia majadiliano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa yaani amani. Kwa sababu vita inasababisha maafa kwa watu na mali zao; vita ina sababisha vifo, inaharibu mazingira pamoja na kufisha matumaini ya watu. Majadiliano katika ukweli na uwazi yanavunjilia mbali kuta za utengano: kiroho na kiakili; yanafungua nafasi ya msamaha na kukoleza upatanisho. Majadiliano ni chombo cha haki kinachochochea na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kukazia amani. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yanapaswa kufumbata uvumilivu, yanajielekeza katika mchakato wa ushuhuda kama chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, upendo na mafao ya wengi. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anakazia utawala bora kama sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Utawala bora unaozingatia: sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa na wengi. Hapa, dhana ya “Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ni mfano bora wa kuigwa! Kumbe, utawala bora unapaswa kuakisi matakwa ya jamii na wala si hisia za mtu binafsi. Pamoja na vipaumbele hivi vyote, Injili ya uhai na maisha ya ndoa na familia zinapewa uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo!

Papa Francisko 8YRS
20 March 2021, 09:54