Tafuta

Vatican News
Miaka 10 ya Madhara ya Vita nchini Siria: Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Mario Zenari wamezungumzia kuhusu vita hii na umuhimu wa kuonesha mshikamano wa Kimataifa katika ujenzi wa Siria mpya! Miaka 10 ya Madhara ya Vita nchini Siria: Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Mario Zenari wamezungumzia kuhusu vita hii na umuhimu wa kuonesha mshikamano wa Kimataifa katika ujenzi wa Siria mpya!  (AFP or licensors)

Miaka 10 ya Vita Nchini Siria: Maafa Makubwa Kwa Watu wa Mungu!

Vita nchini Siria ilifumuka rasmi tarehe 15 Machi 2011 na tangu wakati huo, watu milioni 1.5 wamefariki dunia. Na zaidi ya wananchi milioni 12 hawana makazi ya kudumu; wengi wao wamelazimika kuikimbia nchi yao kutokana na kuandamwa na njaa, umaskini na magonjwa. Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria ni shuhuda wa majanga yanayoendea kuwatesa watu wa Siria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Miaka 10 imegota tangu Siria ilipoingia vitani na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wananchi wa Siria wanaendelea kupoteza maisha kutokana na aina mbalimbali za silaha: Kuna mabomu ya kurushwa na yale yanayotegwa ardhini, bila kusahau silaha za kinyuklia. Hakuna jambo linalosikitisha kuona kwamba, mtu anapoteza maisha na wala hakuna anayesikitika wala kujali. Makali ya vita yanaendelea kupungua, lakini watu wa Mungu wanakabiliana na umaskini mkubwa wa hali na kipato. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 80 % ya wananchi wote wa Siria ni maskini na haki zao msingi zinaendelea kusiginwa kutokana na baa la njaa, utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto wa Siria pamoja na magonjwa mengine. Kuna baadhi ya makampuni ya kigeni na kimataifa yanayoendelea kujichotea mafuta ghafi kwa kiwango cha kutisha sana. Watu wanaotafuta mbao, wamekuwa wakikata miti ovyo kana kwamba “hiki ni kichwa cha mwendawazimu”. Kana kwamba, mambo yote haya hayatoshi, kuna baadhi ya makapuni makubwa makubwa ya kigeni yamekwapua maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya mafao binafsi. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainishwa kwamba, kuna zaidi ya watu 10, 000 wamepotea katika mazingira ya kutatanisha na hawajulikani mahali walipo! Kati yao kuna Maaskofu wawili wa Aleppo pamoja na Mapadre watatu ambao kati yao yumo Padre Paolo Dall’Oglio, SJ., ambaye kwa muda wa miaka saba, hajulikani mahali alipo.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 14 Machi 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesikitika kusema kwamba, vita hii imesababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Kuna idadi kubwa sana ya watu ambao wamepoteza maisha na wengine kupata majeraha na vilema vya kudumu. Kuna mamilioni ya watu ambao wamejikuta wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji; watu wasiokuwa na makazi maalum. Vita imesababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu, mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Siria. Lakini, waathirika wakubwa ni wanawake, watoto na wazee. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu ametoa wito kwa wadau wote wanaohusika katika mgogoro huu, kuonesha mapenzi mema, kwa kuwasha moto wa matumaini kwa watu wa Mungu nchini Siria. Anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kufanya maamuzi pamoja na dhamana ya kuijenga Siria upya, kama kielelezo cha mshikamano wa kidugu na Jumuiya ya Kimataifa.

Ni wakati wa kusitisha vita, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii, tayari kunogesha mchakato wa ujenzi wa Siria mpya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuiombea Siria, ili kamwe mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini humo yasije yakasahaulika. Mshikamano wa kidugu usaidie kupyaisha matumaini! Itakumbukwa kamba, vita nchini Siria ilifumuka rasmi tarehe 15 Machi 2011 na tangu wakati huo, watu milioni 1.5 wamefariki dunia. Na zaidi ya wananchi milioni 12 hawana makazi ya kudumu; wengi wao wamelazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, kutokana na kuandamwa na baa la njaa, umaskini na magonjwa. Hivi ndivyo anavyobainisha Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria ambaye amekuwemo nchini Siria kwa kipindi hiki chote cha vita na mauaji ya kimbari, katika mahojiano na Vatican News anabainisha kwamba, miaka 10 ya vita nchini Siria imepelekea kuporomoka kwa masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, kiasi kwamba, hata leo hii watu wengi, wameanza kupoteza matumaini kwa Siria iliyo bora zaidi kwa leo na kwa kesho.

Siria ni kati ya nchi ambazo mahangaiko ya watu wa Mungu yameacha chapa ya kudumu katika akili na sakafu ya moyo wa Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni wakati wa kuonesha mshikamano wa Kimataifa, kwa kusitisha vita na kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Ni wakati wa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa Siria mpya katika medani mbalimbali za maisha, ili kupambana na ujinga, maradhi na umaskini wa hali na kipato! Aslimia 90% ya wananchi wote wa Siria wanakabiliwa na umaskini. Hii ni vita ya kiuchumi na madhara yake ni ukosefu wa fursa za ajira na kwamba, viwanda vingi vimebomolewa. Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea kupekenya maisha ya watu wa Mungu nchini Siria. Amana na utajiri wa maliasili umekuwa ni chanzo cha vita na maafa ya wananchi wa Siria. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, kiasi cha kukatisha tamaa ya maisha. Hakuna utashi wa kisiasa kwa Jumuiya ya Kimataifa kupata suluhu ya amani ya kudumu nchini Siria. Waathirika wakuu ni wanawake, watoto na wazee. Zaidi ya watoto milioni mbili kutoka Siria hawana fursa ya kwenda shule. Watoto wa kike wamekuwa wakitumbukizwa kwenye ndoa za shuruti. Lakini, ikumbukwe kwamba, vijana ni tumaini la watu wa Mungu nchini Siria. Changamoto kubwa kwa wakati ni uhakika wa usalama wa chakula pamoja na huduma bora za afya.

Kuna kiwango kikubwa cha rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma. Ikumbukwe kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo ya binadamu kama anavyosema Mtakatifu Paulo wa VI akakazia Mtakatifu Yohane Paulo II na sasa Baba Mtakatifu Francisko anahimiza udugu wa kibinadamu. Kuna haja ya kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa upatanaisho, haki na amani nchini Siria. Kanisa limeendelea kujipambanua kuwa kama “Msamaria mwema” katika huduma za kiroho na kimwili. Miaka 10 ya Vita Nchini Siria ni wakati wa kuamka na kutenda kwa ari na nguvu mpya, ili amani ya kweli iweze kutawala akili na nyoyo za watu. Mchakato wa kufufua uchumi hauna budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria anawashukuru wale wote ambao wameendelea kujisadaka kama “Wasamaria wema” kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Siria.

Miaka 10 ya Vita Siria

 

16 March 2021, 14:58