Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 17 Machi 2021 amekamilisha mzunguko wa katekesi kuhusu Fumbo la Maisha ya Saka kwa kutafakari zaidi kuhusu Roho Mtakatifu katika maisha ya sala. Papa Francisko tarehe 17 Machi 2021 amekamilisha mzunguko wa katekesi kuhusu Fumbo la Maisha ya Saka kwa kutafakari zaidi kuhusu Roho Mtakatifu katika maisha ya sala.  (Vatican Media)

Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Roho Mtakatifu

Papa ametafakari kuhusu: Sala na Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea na Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Machi 2021 kutoka kwenye Maktaba yake binafsi mjini Vatican, ametafakari kuhusu: Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia watu Yesu ni nani. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Katakesi kuhusu Fumbo la Sala na Roho Mtakatifu imeongozwa na sehemu ya Injili ya Yohane inayosema. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Yn. 14: 15-26.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi kuhusu Fumbo la Sala kama kielelezo cha mafunagamano na Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kusema, Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba wa milele, anayewafundisha na kuwakumbusha yote walioambiwa na Kristo Yesu. Roho Mtakatifu ni mwalimu wa Sala ya Kikristo na ndiye anayeiandika historia ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Roho Mtakatifu ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayewawezesha waamini kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya nyoyo zao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, huku wakivutwa na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Waamini ni mahujaji na wageni si tu hapa ulimwenguni bali hata katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ibrahimu, Baba wa Imani, kwa njia ya ukarimu kwa wapita njia, alibahatika kumkaribisha Mungu katika hema lake.

Kwa sasa waamini wanathubutu kumwita Mwenyezi Mungu “Aba” yaani “Baba” kwani ndani mwao wanaye Roho Mtakatifu anayewageuza kutoka katika undani wa maisha yao na kuwawezesha kung’amua na hatimaye, kuonja kwamba, wanapendwa sana na Mwenyezi Mungu kama watoto wake wa kweli! Katika undani wa maisha ya mwamini, Roho Mtakatifu anatenda kazi ya kuendeleza maisha yao, ili yaweze kupata utimilifu kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. “Hawezi mtu kusema: “Yesu ni Bwana,” asipoongozwa na Roho Mtakatifu.” Kila mara waamini wanapoanza kusali kwa Yesu ni Roho Mtakatifu ambaye kwa neema yake inayotangulia inawavuta waamini katika njia ya sala. Kwa kuwa anawafundisha kusali kwa kumkumbuka Kristo Yesu. Hivi inawezekanaje kutosali kwa Roho Mtakatifu mwenyewe? Ndiyo sababu Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumwomba Roho Mtakatifu kila siku, hasa mwanzo na mwisho wa kila tendo muhimu. Rej. KKK namba 2670.

Kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kuwakumbusha kuhusu Kristo Yesu na kumweka kati yao na wala si tena “Mhenga” kwani yuko kati pamoja na waja wake, vinginevyo wangelikwisha kutoweka kwenye uso wa dunia kama “Umande wa asubuhi”. Roho Mtakatifu anawategemeza na kuwaimarisha: Wakristo wa nyakati zote na ni mahali muafaka pa kuweza kukutana na Kristo Yesu kwa sababu yuko ndani ya waamini wenyewe. Roho Mtakatifu anaendelea kuwafundisha Mitume wa Kristo kwa kugeuza nyoyo zao kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro, Mtume Paul na Maria Madgalena! Kristo Yesu yupo pamoja na kati ya waja wake kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Haya ni mang’amuzi mazito ya watu wa sala waliofundwa na Roho Mtakatifu kadiri ya kigezo cha Kristo Yesu, mintarafu huruma, huduma, katika sala na katekesi makini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni neema kukutana na watu kama hao wanaoshuhudia utofauti wa maisha kiasi kwamba, wana upeo na mang’amuzi makubwa ya maisha. Huu si ushuhuda unaotolewa na Wamonaki na wakaa pweke peke yao, bali hata waamini wa kawaida tu. Hawa ni watu ambao wamejenga historia ndefu ya mafungamano ya mazungumzo ya sala na Mwenyezi Mungu; wakati mwingine, haya yamekuwa ni mapambano ya ndani, kielelezo cha imani inayotakasa. Hawa mashuhuda amini, wamejitahidi kumtafuta Mwenyezi Mungu katika Injili, kwa kupokea na kuabudu Ekaristi Takatifu; kwa kumwona Mungu katika sura ya ndugu na jirani zao waliokuwa katika shida na mahangaiko makubwa, kiasi cha kuhifadhi uwepo wa Mungu katika maisha yao kama siri ya moto wa upendo ndani mwao.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, wajibu wa kwanza wa mfuasi wa Kristo ni kuhakikisha kwamba, anaendelea kuwasha moto wa mapendo ulioletwa na kuwashwa na Kristo Yesu hapa duniani. Huu ndio upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Bila moto wa Roho Mtakatifu, unabii unakoma, huzuni “inasigina” furaha; mazoea yanachukua nafasi ya upendo; huduma inageuzwa kuwa ni utumwa. Baba Mtakatifu wakati wa ufafanuzi huu, amewakumbusha waamini kuhusu taa ya uzima inayowekwa pembeni mwa Tabernakulo, mahali ambapo Ekaristi Takatifu imehifadhiwa. Hata wakati ambapo hakuna waamini Kanisani, au Kanisa limefungwa, taa ya uzima inaendelea kuwaka. Hakuna mtu anayeiona ikiwaka, lakini daima iko mbele ya Bwana. Mababa wa Kanisa wanasema “Roho Mtakatifu ambaye mpako wake unaenea nafsi yetu yote, ni Bwana wa ndani wa sala ya Kikristo. Ndiye fundi wa Mapokeo hai ya sala. Kwa hakika, kuna vinjia vingi vya sala kama walivyo watu wanaosali, lakini ni Roho yule yule anayetenda kazi ndani ya wote pamoja na wote. Ni ndani ya ushirika wa Roho Mtakatifu ambamo sala ya Kikristo ni sala katika Kanisa.” KKK n. 2672.

Mara nyingi waamini wanajisikia kutofahamu kusali vyema, au wanakosa hamu ya kusali au wanasali vibaya kwa “kupayuka payuka maneno kama Kasuku” lakini nyoyo zao ziko mbali sana na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawashauri waamini kumkimbilia Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kusali vyema zaidi. Awashe nyoyo zao kwa upendo, awafundishe kusali vyema kwa kumwangalia Mungu Baba Muumbaji na Mungu Mwana Mkombozi. Waamini wamwite mara kwa mara Roho Mtakatifu ili awafundishe kupenda na kuwa na matumaini zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema ni Roho Mtakatifu anayeandika historia ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Waamini ni kurasa wazi ambazo ziko tayari kupokea maandishi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Katika undani wa kila mtu, Roho Mtakatifu anatenda kazi tofauti tofauti na mwingine.

Katika uwanja wa utakatifu wa maisha, Mungu mmoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ambao ni Upendo, anawezesha shuhuda mbalimbali kuchipuka miongoni mwa waja wake. Shuhuda hizi katika utu na uzuri wake ni sawa kwa sababu ni mpango wa Roho Mtakatifu kuwawezesha watu wote ambao kwa njia ya huruma ya Mungu, wote wamefanyika kuwa ni watoto wake wapendwa! Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba wa mbinguni, ni nguvu na mwanga wa maisha; na kwamba, ni Mwalimu wa sala ya Kikristo!

Fumbo la Sala
17 March 2021, 16:13

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >