Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Mwaka wa Upendo Ndani ya Familia ni mwaliko wa kupyaisha tena na tena tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kuendelea kusoma alama za nyakati! Maadhimisho ya Mwaka wa Upendo Ndani ya Familia ni mwaliko wa kupyaisha tena na tena tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kuendelea kusoma alama za nyakati! 

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Umuhimu Wake!

Waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lengo kuu la Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni kama ifuatavyo: Ni kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Machi 2021 amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka nchini Poland kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Upendo Ndani ya Familia ni fursa ya kuwa na mwono mpana zaidi wa Kiinjili kuhusu Ndoa Takatifu; Kwa kuheshimu na kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021 itakuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.  

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 14 Machi 2021 alitoa mwaliko wa pekee, ili kupyaisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Ni sala ya Baba Mtakatifu kwamba, familia mbaliambali zitaweza kuonja uwepo mwanana wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ndani ya familia zao. Uwepo huu, uwe ni faraja itakayoziwezesha familia kuwa ni jumuiya za upendo wa kweli, ukarimu sanjari na kuwa ni chemchemi ya furaha licha ya majaribu na magumu wanayokumbana nayo katika maisha! Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Unatoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia.

Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia anasema Baba Mtakatifu Francisko ni muda muafaka kwa familia ya Mungu kurejea tena na kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia huu ambao unakazia: Upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawahimiza wazazi na walezi kuimarisha elimu, malezi na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao wa ndoa na familia. Tafakari hii ifanywe kwa msaada wa nyenzo mbalimbali za shughuli za kichungaji kwa kusikiliza na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na watu wa Mungu. Mkazo utolewe kwenye maandalizi ya wana ndoa watarajiwa, elimu kuhusu maana na mahusiano ya kimaumbile miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Waamini waelimishwe zaidi kuhusu: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Iwe ni nafasi ya kuadhimisha makongamano ya kitaifa na kimataifa kuhusu: upendo wa familia, wito na njia ya utakatifu ili kukabiliana na changamoto mambaoleo zinazoendelea kuibuka kila kukicha kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia sasa linaanza kutayarisha nyaraka mbalimbali zinazoweza kuwa msaada katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia”. Unaweza kupata habari zaidi kwa kupekua katika tovuti ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa anuani ifuatayo: www.amorislaetitia.va. Tovuti hii itakuwa inapyaishwa kila wakati ili kutoa habari na ushauri motomoto kama unavyopokelewa kutoka sehemu mbalimbali za dunia.  Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” liwe ni tukio shirikishi, litakalowagusa wana familia wote, kadiri ya wito na wajibu wao ndani ya familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Maadhimisho haya yakoleze ari na mwamko wa maandalizi kwa wanandoa, kwa kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao. Wazazi wapewe katekesi kuhusu dhamana na wajibu wao wa malezi: kiroho, kiutu na kitamaduni, ili waweze kutekeleza wajibu huu kwa umakini zaidi. Wazazi wafundwe na wapewe nafasi ya kushirikisha: matatizo, changamoto, uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, ili kutambua na hatimaye, kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutangaza, kushiriki na kushuhudia mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia. Wazee na wanandoa wapya waangaliwe kwa jicho la kichungaji. Tema kama vile: familia, wito wa kitawa na kipadre; useja, Injili ya uhai, utamaduni wa kifo; umuhimu na madhara ya kutumia mitandao ya kijamii; ufukara wa Kiinjili na umaskini wa hali na kipato; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maadhimisho haya yawakumbuke na kuwashirikisha watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” usaidie kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano kati ya familia na Kanisa, kwa kuwashirikisha zaidi wanandoa katika maisha na utume wa Kanisa. Malezi na katekesi ya kina, itolewe kwa mihimili yote ya Uinjilishaji, ili kukabiliana barabara na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kuibuliwa katika maisha ya ndoa na familia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, familia kama Kanisa dogo la nyumbani inaimarishwa zaidi, kwa kutambua dhamana na utume wake usiokuwa na mbadala! Ni wakati wa kukuza na kuhamasisha wito wa kimisionari ndani ya familia, kwa kuwajengea wazazi na walezi uwezo wa kufundisha na kuwarithisha watoto wao: imani na tunu msingi za Kiinjili; kwa kuwaandaa kikamilifu tangu awali kushiriki na kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia, bila kusahau wito wa Daraja Takatifu. Kumbukizi ya ndoa iwe ni fursa ya kupyaisha tena katekesi na maagano ya ndoa, ili kuweza kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Mwaka wa Upendo
17 March 2021, 15:57