Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kulaani Mapinduzi ya Kijeshi yaliyofanyika nchini Myanmar. Baba Mtakatifu anatoa wito kwa viongozi wanaohusika kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kulaani Mapinduzi ya Kijeshi yaliyofanyika nchini Myanmar. Baba Mtakatifu anatoa wito kwa viongozi wanaohusika kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. 

Mapinduzi ya Kijeshi Myanmar: Papa: Majadiliano Katika Ukweli

Papa anapenda kutoa wito kwa viongozi wanaohusika, kuanza mchakato wa majadiliano ili kuondokana na matumizi makubwa ya mtutu wa bunduki, hali inayoendelea kusababisha uvunjifu wa amani na ukosefu ulinzi na usalama. Papa anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati na kuiokoa Myanmar inayoanza kuzama katika machafuko na maafa makubwa kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kulaani na kushutumu mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar yaliyotokea hivi karibuni na kutoa wito wa kurejeshwa tena utawala wa kidemokrasia sanjari na kuachiliwa huru Aung San Suu Kyi na wanasiasa wenzake. Jeshi la Myanmar limewaonya waandamanaji wanaopinga mapinduzi kote nchini humo kwamba, huenda wakakabiliwa kifungo cha hadi miaka 20 jela wakizuia vikosi vya jeshi kutekeleza kwa ufanisi shughuli zao. Adhabu ya muda mrefu na faini pia vitatolewa kwa wale wote watakaopatikana na hatia ya kuchochea "chuki na dharau" dhidi ya viongozi wa mapinduzi ya kijeshi. Hatua hiyo ya kisheria imetangazwa huku magari ya kivita yakionekana barabarani katika miji tofauti nchini humo, ili kuwajengea wananchi hofu ya “kipigo cha mbwa koko” ikiwa kama wataendelea kukaidi amri halali za viongozi wa mapinduzi ya kijeshi. Maelfu ya watu wamekuwa wakishiriki maandamano katika siku za hivi karibuni.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Machi 2021 ameyaelekeza mawazo yake nchini Myanmar ambako watu wengi wasiokuwa na hatia, wanaendelea kumwaga damu na kupoteza maisha. Baba Mtakatifu anapenda kutoa wito kwa viongozi wanaohusika, kuanza kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na matumizi makubwa ya mtutu wa bunduki, hali inayoendelea kusababisha uvunjifu wa amani na ukosefu ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kuingilia kati na kuiokoa Myanmar inayoanza kuzama katika machafuko na maafa makubwa. Vijana nchini Myanmar wapewe tena nafasi ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, mahali ambapo chuki na uhasama havina nafasi tena na badala yake, watu wajikite katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa na msamaha wa kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa demokrasia ulioanza kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni nchini Myanmar, utapyaishwa tena kwa kuwaachia huru wanasiasa waliofungwa gerezani au kuwekwa kizuizini.

Myanmar

 

03 March 2021, 15:24