Tafuta

Vatican News
Papa Francisko ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na machafuko yaliyoibuka huko nchini Paraguay. Ametoa wito kwa wananchi kujizatiti katika kujenga amani na utulivu. Papa Francisko ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na machafuko yaliyoibuka huko nchini Paraguay. Ametoa wito kwa wananchi kujizatiti katika kujenga amani na utulivu.  (AFP or licensors)

Machafuko ya Kisiasa Paraguay! Masikitiko ya Papa Francisko!

Baba Mtakatifu Francisko anawasihi watu wa Mungu nchini Paraguay kujizatiti katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kimsingi, watu wanatumaini kuona amani na utulivu vikitawala. Ikumbukwe kwamba, vita na vurugu ni mambo yanayosababisha majanga makubwa kwa wananchi wenyewe, kiasi cha kupoteza kila kitu! UVIKO-19 na rushwa vinachangia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 17 Machi 2021 amesikitika kusema kwamba, taarifa kutoka nchini Paraguay zinaonesha kwamba, hali ya kisiasa nchini humo inaanza kuwa tete sana kutokana na maandamano makubwa yanayoendelea kufanyika nchini humo tangu tarehe 5 Machi 2021. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaombea amani watu wa Mungu nchini Paraguay na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya maombezi ya Bikira Maria wa Miujiza wa Caacupé. Anamwomba Kristo Yesu, Mfalme wa amani, awasaidie wadau wakuu kuanza mchakato wa majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, kupata suluhu ya kweli katika mgogoro huu ambao ni hatari sana kwa ushirikiano na mafungamano ya Kitaifa.

Baba Mtakatifu anawasihi watu wa Mungu nchini Paraguay kujizatiti katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kimsingi, watu wanatumaini kuona amani na utulivu vikitawala. Ikumbukwe kwamba, vita na vurugu ni mambo yanayosababisha majanga makubwa kwa wananchi wenyewe, kiasi cha kupoteza kila kitu. Wananchi wamekuwa wakidai kwamba, Rais Mario Abdo Benitez ameshindwa kuongoza mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maambukizi yanazidi kuongezeka maradufu, baada ya Serikali ya nchi hiyo kudhibiti ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa muda wa mwaka mmoja.

Kumekuwepo na mapambano ya nguvu kati ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma; ukosefu wa dawa muhimu hospitalini pamoja na uhaba mkubwa wa dawa ya chnjo ili kudhibiti janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Jumuiya ya Kimataifa inaitaka Serikali ya Paraguay kuwahakikishia wananchi wake uhuru wa kujieleza pamoja na kuandamana kwa amani. Demokrasia na utawala wa sheria vinapaswa kutumika kikamilifu. Paraguay inapaswa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa kuzingatia ukweli, uwazi na uwajibikaji. Paraguay inapaswa kupambana na rushwa hadi kieleweke!

Paraguay

 

 

 

17 March 2021, 15:45