Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 19 Machi 2021 amefanya kumbukizi la miaka 8 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Salam na Pongezi kutoka kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia Papa Francisko tarehe 19 Machi 2021 amefanya kumbukizi la miaka 8 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Salam na Pongezi kutoka kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia  (ANSA)

Kumbukizi la Miaka 8 ya Papa Francisko: Khalifa wa Mt. Petro

Ni katika muktadha wa kumbukizi la Miaka nane, tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki, Rais Sergio Mattarella, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, tarehe 19 Machi 2021 amemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa heri, baraka na matashi mema katika maisha na utume wake, hasa katika ulimwengu mamboleo wenye changamoto kibao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2013 alianza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, sanjari na Maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko pia ni Askofu wa Jimbo la Roma, Kanisa ambalo ni kielelezo cha upendo na mshikamano na Makanisa mengine yote yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya na utamadunisho unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ameendelea kuhimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Anapenda kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa.

Ni katika muktadha wa kumbukizi la Miaka nane, tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki, Rais Sergio Mattarella, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, tarehe 19 Machi 2021 amemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa heri, baraka na matashi mema katika maisha na utume wake, hasa katika ulimwengu mamboleo wenye changamoto kibao! Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 limeendelea kusababisha maafa makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu. Changamoto hii inapaswa kushughulikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuzingatia haki na ufanisi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amekuwa ni shuhuda, msaada na faraja kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Rais Sergio Mattarella anakaza kusema, kufanya kazi kwa ari na moyo wa udugu wa kibinadamu ni nyenzo msingi katika kuvuka matatizo na changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa.

Kila wananchi anapaswa kuwajibika vyema kadiri ya uwezo na nafasi yake katika jamii. Ni mwaliko wa kufuata na kutekeleza kwa dhati itifaki za mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Jumuiya ya Kimataifa ishikamane kwa dhati katika kuboresha sekta ya afya na ustawi wa jamii katika ujumla wake. Hii ni changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko aliitoa wakati wa hija yake ya Kitume nchini Iraq hivi karibuni. Rais Sergio Mattarella anamshukuru Baba Mtakatifu kwa upendeleo wa pekee anaouonesha kwa familia ya Mungu nchini Italia. Kwa mara nyingine tena anapenda kuchukua fursa hii, kumtakia heri, baraka na mafanikio mema, Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro sanjari na Sherehe za Pasaka ya Bwana, zinazokaribia!

Rais Sergio
20 March 2021, 09:42