Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimataifa: Utu, heshima na haki msingi za wanawake zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Wanawake wa Iraq ni mashujaa wanachangia Injili ya uhai, licha ya magumu yanayowakabili. Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Kimataifa: Utu, heshima na haki msingi za wanawake zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Wanawake wa Iraq ni mashujaa wanachangia Injili ya uhai, licha ya magumu yanayowakabili. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Wanawake wa Iraq

Ni matumaini ya Papa Francisko kwamba, wanawake wataheshimiwa, watalindwa na kupewa fursa ya kujiendeleza zaidi. Anawashukuru wanawake wote kutoka katika sakafu ya moyo wake, lakini zaidi ni kwa wanawake nchini Iraq. Hawa ni wanawake wa “shoka” wanaoendelea kuchangia Injili ya uhai licha ya magumu, changamoto na madonda makubwa wanayobeba nyoyoni mwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 amehitimisha hija yake ya 33 ya kitume nchini Iraq, iliyonogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu amekuwa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Amekuwemo nchini Iraq kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Amepata nafasi ya kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. Hii ni hija ya kwanza ya kihistoria kuandikwa na Baba Mtakatifu Francisko, kama Khalifa wa kwanza wa Mtakatifu Petro kutembelea Iraq licha ya changamoto pevu zilizokuwa mbele yake.

Baba Mtakatifu mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa “Franso Hariri” huko Erbil, Jumapili tarehe 7 Machi 2021 amekutana na kusalimiana na familia ya Mzee Abdullah Kurdi kwa muda wa kutosha. Familia ya Mzee Kurdi ilimpoteza mtoto Alan Kurdi kwa kufa maji wakati wakiwa katika harakati za kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora ughaibuni. Maiti ya mtoto Alan Kurdi ikaokotwa kwenye ufuko wa bahari nchini Uturuki Mwezi Septemba 2015. Baba Mtakatifu Francisko amesikiliza kwa umakini mkubwa machungu ya familia kupoteza mtoto katika mazingira tete kama yale, katika harakati za kutafuta hifadhi, usalama na ustawi. Picha ya Mtoto Alan Kurdi ilisambaa sana kwenye vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, kuonesha utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine.

Mzee Abdullah Kurdi ametumia fursa hii, kumshukuru Baba Mtakatifu kwa kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kuwatetea na kuwalinda maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtoto Alan Kurdi ni mfano tosha kabisa wa wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji kila kukicha na kuzikwa kwenye tumbo la bahari. Wakimbizi na wahamiaji wanahitaji hifadhi, usalama na kueleweka, wanapoamua kuchukua maamuzi magumu ya kuzikimbia nchi zao.

Tarehe 8 Machi 2021, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Baba Mtakatifu anapenda kuwaaminisha watu wa Mungu nchini Iraq chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa upendo. Kwa bahati mbaya sana, taswira ya Bikira Maria nchini Iraq imekashifiwa na kunajisiwa, lakini hata hivyo, Bikira Maria anaendelea kuwaangalia kwa huruma na mapendo, kwa faraja na hatimaye, kuwatia shime kuendelea kusadaka maisha, licha ya mabaya wanayowatendea. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, wanawake wataheshimiwa, watalindwa na kupewa fursa ya kujiendeleza zaidi. Kwa namna ya pekee kabisa, anapenda kuwashukuru wanawake wote kutoka katika sakafu ya moyo wake, lakini upendeleo wa pekee, ni kwa ajili ya wanawake nchini Iraq. Hawa ni wanawake wa “shoka” wanaoendelea kuchangia Injili ya uhai licha ya magumu, changamoto na madonda makubwa wanayobeba nyoyoni mwao.

Papa Wanawake wa Iraq

 

08 March 2021, 15:34