Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini Iraq wakati huu anapojiandaa kuanza hija yake ya kitume kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini Iraq wakati huu anapojiandaa kuanza hija yake ya kitume kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Ujumbe Kwa Wairaq

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia watu wa Mungu nchini Iraq ujumbe akisema kwamba, anakwenda nchini mwao kama hujaji wa toba, ili kumwomba Mungu msamaha na kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Anakwenda kati yao kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano. Anataka kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hii ni hija inayofumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, uhamasishaji wa ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza hija yake rasmi nchini Iraq, amewatumia watu wa Mungu nchini humo ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, akisema kwamba, anakwenda nchini mwao kama hujaji wa toba, ili kumwomba Mungu msamaha na kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Anakwenda kati yao kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Anataka kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. Kwa watu wote wa Mungu nchini Iraq, Baba Mtakatifu Francisko anawaomba waendelee kumsindikiza kwa sala na sadaka yao!

Iraq ni nchi ambayo imebahatika sana kuwa na urithi wa utamaduni wa miaka mingi. Baba Mtakatifu anasema anakwenda nchini Iraq kama hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, ili hatimaye, kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa baada ya “patashika nguo kuchanika” kutokana na vita na vitendo vya kigaidi. Anakwenda Iraq ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kuifariji nyoyo na kuponya majeraha! Ni hujaji wa amani, kwa kutambua kwamba wote ni ndugu wamoja! Hii ni changamoto ya kuhamasisha udugu wa kibinadamu, ili kwa pamoja waweze kusali na kutembea bega kwa bega kwa waamini wa dini mbalimbali kama kielelezo cha majadiliano ya kidini pamoja na kuendelea kutembea na Wakristo ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kwani: Waislam, Wayahudi na Wakristo, wote hawa ni watoto wa Ibrahimu, Baba wa Imani. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime Wakristo ambao kwa miaka ya hivi karibuni “wameguswa na kupapaswa” na majaribu magumu sana ya imani, lakini wakajizatiti na kusimama imara katika imani. Anashukuru na kulipongeza Kanisa la mashuhuda wa imani.

Mashuhuda wa imani, wanawawezesha waamini kuendelea kudumu katika nguvu na unyenyekevu wa upendo. Mbele yake anayo picha ya magofu ya nyumba zilizobomolewa kwa vita, Makanisa yaliyonajisiwa pamoja na nyoyo zilizovunjika na kupondeka kutokana na kulazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao, kwa kutafuta hifadhi na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kutoa faraja inayobubujika kutoka kwa Mama Kanisa kwa watoto wake wote walioko huko Mashariki ya Kati na kwamba, umefika wakati wa kujikita katika wema badala ya kuendekeza matendo maovu. Ni wakati wa kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo. Kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu aliyeadilika kwa imani, akatarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa Baba wa Mataifa mengi kuliko hata nyota za angani. Matumaini ya watu wa Mungu nchini Iraq yanafumbatwa katika ahadi ya Mungu.

Kwa muda mrefu anasema Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuwafikiria sana hasa kutokana na mateso makali waliyokumbana nayo katika hija ya maisha yao; wote kama ndugu wameteseka sana. Anakwenda nchini Iraq kama hujaji wa matumaini katika nchi ambayo imebarikiwa lakini ina madonda makubwa. Kama ilivyokuwa wakati wa Nabii Yona aliyetabiri toba na wongofu wa ndani, ukawa ni chemchemi ya matumaini badala ya maangamizi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata Baba Mtakatifu anapenda kuwa ni shuhuda na chombo cha matumaini mapya, matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni matumaini yanayowatia shime mchakato wa ujenzi mpya wa Iraq. Katika nyakati hizi za shida na magumu, iwe ni fursa ya kusaidiana ili kuimarisha udugu wa kibinadamu ili hatimaye, kujenga leo na kesho inayosimikwa katika msingi wa amani kwa kushirikiana na waamini wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Iraq ni mahali ambapo Ibrahimu Baba wa Imani alianzia safari ya maisha yake ya kiroho. Sasa umefika wakati kwa wao kuendeleza moyo huo kwa kutembea katika njia ya amani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuwaombea amani na baraka inayobubujika kutoka juu mbinguni, tayari kutembea katika mwanga wa matumaini. Anawaomba watu wote wa Mungu nchini Iraq kumkumbuka na kumsindikiza katika hija hii ya kitume kwa sala zao.

Papa: Ujumbe Iraq

 

 

04 March 2021, 14:47