Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwakwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo ameshiriki katika sala ya watoto wa Ibrahimu Baba wa Imani, siku ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Ibrahimu, Baba wa Imani. Baba Mtakatifu Francisko akiwakwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo ameshiriki katika sala ya watoto wa Ibrahimu Baba wa Imani, siku ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Ibrahimu, Baba wa Imani. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Watoto wa Ibrahimu

Maadhimisho ya Siku ya Sala ya Watoto wa Ibrahimu, kumekuwepo na Masomo kutoka katika Koran Tukufu na Biblia Takatifu pamoja na shuhuda za waamin. Hii ni safari inayowawezesha watoto wa Ibrahimu Baba wa imani kutazama juu angani, huku wakiwa wanasafiri hapa duniani. Ni safari inayojikita katika njia ya ujenzi wa amani na baraka ya amani! Sala chemchemi ya amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Sala ni chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba”. Rum. 8:14. Katika maadhimisho ya Siku ya Sala ya Watoto wa Ibrahimu,  kumekuwepo na Masomo yaliyoimbwa kutoka katika Koran Tukufu na Biblia Takatifu. Baadhi ya waamini wametoa ushuhuda wa imani yao. Watoto wa Ibrahimu pamoja na waamini wa dini mbalimbali wakasali kwa heshima ya Ibrahimu Baba wa imani. Hii ni safari inayowawezesha kutazama juu angani, huku wakiwa wanasafiri hapa duniani. Ni safari inayojikita katika njia ya ujenzi wa amani na baraka ya amani.

Itakumbukwa kwamba, Wayahudi, Waislam na Wakristo wote hawa ni watoto wa Ibrahimu Baba wa imani. Baba Mtakatifu Francisko katika sala yake, Jumamosi tarehe 6 Machi 2021, amemshukuru Mwenyezi Mungu aliyemweka Ibrahimu Baba wa imani kuwa ni mfano bora wa kuigwa kutokana na utii wake, uliomwezesha kuacha yote na kutumainia ahadi ya Mungu. Akaonesha ujasiri, uthabiti, nguvu ya roho na ukarimu uliotengwa na Ibrahimu kwa ajili ya watoto wake wote katika imani. Ibrahimu Baba wa imani ni shujaa wa imani kwa kuwa tayari hata kumtoa sadaka Mwanaye mpendwa kama kielelezo cha utii wa Amri ya Mungu. Haya yalikuwa ni majaribu makubwa sana, lakini Ibrahimu Baba wa imani, akaibuka kidedea, kwa sababu alimwamini Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma ambaye yuko tayari kumkirimia mja wake fursa ya kuanza tena upya.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumfanya Ibrahimu Baba wa Imani kuwa ni chemchemi ya baraka kwa watu wote. Amekuwa ni mfano bora katika imani inayowafungamanisha katika matendo mema; imani inayofungua nyoyo kwa Mungu na jirani. Ni kielelezo makini cha matumaini yasiyokuwa na mipaka, kwa kuendelea kubaki katika uaminifu kwa ahadi za Mungu. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia watoto wa Ibrahimu Baba wa imani ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, wajane, yatima pamoja na wagonjwa.

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwafungulia nyoyo zao ili waweze kutoa na kupokea msamaha na hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, wajenzi wa upendo, haki na jamii inayosimikwa katika udugu. Awakaribishe katika makao yake ya mwanga na amani wale wote waliofariki dunia, lakini zaidi wahanga wa machafuko na vita. Mwenyezi Mungu apende kuwawezesha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa katika juhudi zao za kuwasaka na kuwatia mbaroni wateka nyara; viongozi wawe mstari wa mbele kuwalinda wanawake na watoto. Watoto wa Ibrahimu wawezeshwe kuwa watunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ambayo Mwenyezi Mungu kutokana na wema na ukarimu wake, amewapatia ili wayatumie. Mwishoni, Baba Mtakatifu amemwomba Mwenyezi Mungu apende kuiongoza mikono ya watu wake katika mchakato wa ujenzi mpya wa Iraq, awatie nguvu wanazohitaji ili kuwasaidia wale ambao wamelazimika kuikimbia nchi yao, ili waweze kurejea tena, kwa amani na utulivu, huku wakihakikishiwa usalama, utu na heshima yao.

Sala Watoto wa Ibrahimu
06 March 2021, 14:37