Tafuta

Vatican News
Kilele cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq ni tarehe 6 Machi 2021 katika mkutano wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano wa kidugu, amani na upendo. Kilele cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq ni tarehe 6 Machi 2021 katika mkutano wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano wa kidugu, amani na upendo.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Majadiliano ya Kidini

Masomo kutoka katika Koran Tukufu na Biblia Takatifu yamesomwa na shuhuda za imani zikatolewa. Waamini wa dini mbalimbali wakasali kwa heshima ya Ibrahimu Baba wa imani. Papa Francisko akatoa hotuba. Hii ni safari inayowawezesha kutazama juu angani, huku wakiwa wanasafiri hapa duniani. Ni safari inayojikita katika njia ya ujenzi wa amani na baraka ya amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hii ni hija inayofumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, uhamasishaji wa ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu yuko nchini Iraq kama hujaji wa toba, ili kumwomba Mungu msamaha na kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Yuko kati pamoja nao kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Anapenda kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. 

Kilele cha hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu ni Jumamosi tarehe 6 Machi 2021 kwa kukutana na viongozi wa dini mbalimbali kwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo eneo maarufu ambalo Mwenyezi Mungu alikutana na kufanya ahadi na Ibrahimu, Baba wa imani. Baba Mtakatifu na ujumbe wake, wamesafiri kutoka Baghdad hadi mjini Najaf. Huu ni kati ya miji mitakatifu inayoheshimiwa sana na waamini wa dini ya Kiislam. Akiwa mjini hapo amekutana na kuzungumza na Ayatollah Ali Sistani, kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq kwa faragha. Wachunguzi wa mambo wanasema hii ni fursa ya kumwilisha kwa vitendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Baadaye Baba Mtakatifu ameendelea na safari yake hadi mjini Nassiriya kwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo. “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”. Mwa. 12:1-3.

Hapa kumekuwepo na Masomo kutoka katika Koran Tukufu na Biblia Takatifu. Baadhi ya waamini wametoa shuhuda za imani yao. Watoto wa Ibrahimu pamoja na waamini wa dini mbalimbali wakasali kwa heshima ya Ibrahimu Baba wa imani. Baba Mtakatifu Francisko akatoa hotuba na baadaye. Hii ni safari inayowawezesha kutazama juu angani, huku wakiwa wanasafiri hapa duniani. Ni safari inayojikita katika njia ya ujenzi wa amani na baraka ya amani. Baba Mtakatifu amewataka watoto wa Ibrahimu Baba wa Imani kushikamana katika sala, kwa kutambua kwamba, peke yao, “hawawezi kufua dafu”, kwani wanahitaji neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wakiwa wameungana katika fadhila ya upendo, waweze kufika mbinguni. Wajitahidi kuwa watumishi wema wa Mungu ili aweze kuwakomboa kutoka katika ubinafsi na hali ya kutaka kumezwa na malimwengu, ili hatimaye, waweze kupenda, kama kielelezo makini cha uchaji wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya kiroho.

Dini ya kweli ni kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumpenda jirani; hivyo kuendelea kumtolea ushuhuda wa wema na ukarimu wake wa kibaba unaojionesha kwa njia ya udugu wa kibinadamu. Uwanda wa Uru wa Wakaldayo ni chemchemi ya imani, mahali ambapo Mwenyezi Mungu amejifunua kuwa ni Mungu mwenye huruma. Kashfa kubwa dhidi ya Mwenyezi Mungu ni vita, chuki na uhasama vinavyotekelezwa kwa jina la Mungu. Misimamo mikali ya kidini na kiimani, vita, ghasia, pamoja na vitendo vya kigaidi ni dalili za kutoelewa maana ya dini na matokeo yake ni usaliti na hatimaye, kuzama katika mawingu ya chuki na uhasama. Kwa hakika watu wa Mungu nchini Iraq wameteseka sana kutokana na misimamo mikali na chuki za kidini. Jumuiya ya Wayazidi imeomboleza kutokana na vifo vya ndugu zao. Imeshuhudia watoto wao wakitekwa nyara na kuuzwa kama watumwa. Wakateswa, wakanyanyaswa na hatimaye kufanyiwa wongofu wa shuruti. Kuna baadhi yao, wameweza kuhimili mateso na nyanyaso zote hizi, wote hawa wamekumbukwa na kuombewa, ili waweze kuwa na ujasiri na hatimaye kurejea tena nchini mwao. Hii imekuwa ni fursa ya kusali kwa ajili ya kuombea uhuru wa kidhamiri na uhuru wa kidini, ili uweze kuheshimiwa na kuthaminiwa mahali popote pale duniani kwa sababu mambo haya ni sehemu ya haki msingi za binadamu.

Vitendo vya kigaidi nchini Iraq vimepelekea uharibifu mkubwa wa amana, utajiri na urithi wa nchi hii. Hata katika hali tete namna hii, bado kuna vijana wa Kiislam kutoka Mosul walijisadaka kukarabati Makanisa yaliyokuwa yamebomolewa kama kielelezo cha urafiki wa udugu wa kibinadamu. Leo hii, Waislam na Wakristo wanaendelea kushikamana ili kukarabati Misikiti na Makanisa yaliyobomolewa na kwamba, mahujaji wameanza kurejea tena katika maeneo haya yenye utajiri wa maisha ya kiroho. Kupenda na kulinda maeneo matakatifu ni muhimu sana kama sehemu ya kumbukumbu endelevu kwa Ibrahimu Baba wa imani. Maeneo Matakatifu yawe ni chemchemi ya amani na mahali ambapo watoto wote wa Mungu wanaweza kukutanika. Uwepo wa waamini wa dini mbalimbali kwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo iwe ni fursa ya neema na baraka kwa Iraq, Mashariki ya Kati na Ulimwengu katika ujumla wake! Baba Mtakatifu anasema, safari ya Ibrahimu Baba wa Imani ilianzia kwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo, ikiwa na changamoto kedekede pamoja na sadaka zake, ili kumpenda Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake, kwa sababu wanategemeana na kukamilishana katika hija ya maisha ya hapa duniani. Falsafa ya mtu kutaka kujiokoa peke peke ni hatari sana.

Huu ni mwanzo wa ujenzi wa kuta za utengano na mashindano ya utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha. Lakini silaha za mahangamizi hazitaweza kumkomboa mwanadamu, bali zitaendelea kukuza mpasuko na kinzani. Uchu wa mali na madaraka utawatumbukiza watu katika mchakato wa ulaji wa kupindukia, ukosefu wa usawa, mwanzo wa kudumaa kwa mawazo na hatimaye kifo cha moyo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni safari inayokita mizizi yake katika njia ya amani. Inasikitisha sana kuona watu wengi wakiwa wamejizatiti katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, lakini kuna baadhi ya watu wakiwa wamezama kwenye ubinafsi, wanatafuta masilahi yao. Hakuna amani ya kweli, bila ya watu kupokeana, kushirikiana na kushikama. Hakuna haki ikiwa kama usawa, ustawi na maendeleo ya wengi hayapo. Hakuna amani ya kweli ikiwa kama hakuna ukarimu wa kidugu na matokeo yake ni watu kuanza kukinzana. Amani ya kweli inajengwa juu ya udugu wa kibinadamu ili kwa pamoja waweze kusafiri kutoka katika kinzani na kuanza mchakato wa ujenzi wa umoja wa kidugu. Mkutano huu, imekuwa ni fursa pia kwa ajili ya kuiombea Siria.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ibrahimu Baba wa imani amewaunganisha na kuwazamisha kwenye mchakato wa ujenzi wa amani, unaosimikwa katika urafiki wa kijamii na hivyo kufutilia mbali dhana ya chuki, uhasama na maadui. Ni wakati wa kufua panga ili ziwe majembe, na mikuki iwe miundu, tayari kusimama kidete kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umefika wakati wa kuondokana na uchu wa mali na madaraka, nyanyaso na ukatili. Ni muda wa kuzama katika Injili ya matumaini, kwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani na wakarimu kwa watu wenye njaa. Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na baa la njaa, magonjwa, ujinga na pamoja na kupokwa utu wao. Huu ni muda wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, safari ya Ibrahimu Baba wa imani ilikuwa ni baraka ya amani na ilisheheni shida pamoja na changamoto nyingi.

Mashuhuda wameonesha kwamba, inawezekana kabisa kwa vijana wa Kiislam na Kikristo kusoma na hatimaye, kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu wamoja. Vijana wa kizazi kipya wafundwe ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chanjo dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, tayari kujikita katika amani kwa sababu vijana ni matumaini ya leo na kesho! Hawa ndio jeuri ya Nchi wanaoweza kusaidia mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya miaka ya nyuma. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapongeza wale wote ambao wameendelea kujisadaka na kujitosa katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Watu ambao wamekuwa ni msaada mkubwa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi ya kudumu. Amewapongeza vijana ambao ameamua kwa dhati kabisa kubaki nchini Iraq licha ya matatizo, changamoto na hata kishawishi cha kutaka kuikimbia nchi yao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wale wote waliolazimika kuikimbia nchi yao, waonje ukarimu wanaporejea tena nchini mwao. Ukarimu unavuta baraka kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu Baba wa imani. Familia ya binadamu inapaswa kujenga fadhila ya ukarimu kwa watoto wake wote, ili kwa pamoja waweze kusafiri katika njia ya amani.

Majadiliano ya Kidini
06 March 2021, 14:59