Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na viongozi wa serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa vyama vya kiraia kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Hotuba kwa Viongozi

Papa amegusia Janga la UVIKO-19, Madhara ya vita na vitendo vya kigaidi; Umuhimu wa majadiliano ya kidini. Amefafanua nia ya hija yake na kukazia mchakato wa umoja, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto zinazomwandama mwanadamu. Kimsingi, dini inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya amani na udugu wa kibinadamu. Iraq Kumenoga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, anakwenda nchini Iraq kama hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Anakwenda kati yao kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene. Anataka kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini. Hija ya kitume ya 33 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya kwanza, Ijumaa tarehe 5 Machi 2021 aliyoitoa kwa viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa asasi zisizo za Kiserikali amegusia mambo makuu yafuatayo: Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, Madhara ya vita na vitendo vya kigaidi; Umuhimu wa majadiliano ya kidini ili kukoleza umoja na udugu wa mshikamano. Baba Mtakatifu amefafanua nia ya hija yake ya Kitume nchini Iraq. Amekazia mchakato wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kimsingi, dini inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya amani na udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu nchini Iraq, maskani ya Ibrahimu Baba wa Imani na Manabii ambao wanaunda historia ya kazi ya ukombozi. Iraq ni nchi yenye amana na utajiri mkubwa wa dini ya Wayahudi, Waislam na Wakristo. Anasema, amewasili nchini Iraq kama hujaji, ili kuwatia shime katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia: imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu nchini Iraq. Ni wajibu wa waamini wa dini mbalimbali kuendelea kujichimbia katika tunu msingi za imani, maridhiano na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anafanya hija hii ya Kitume wakati ambako Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kupambana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambalo limepelekea maafa makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu. Huu ni wakati wa kushikamana, ili kuhakikisha kwamba, chanjo iliyopatikana inatolewa kwa usawa kwa ajili ya watu wote sanjari na kubadilisha mtindo wa maisha, kwa kujikita zaidi na mambo yanayowaunganisha zaidi, licha ya tofauti zao msingi, ili kudumisha amani.

Vita, vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini na kiimani imepelekea majanga makubwa, kwa vile tu watu wameshindwa kukubaliana na tofauti zao msingi. Matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumekuwepo na mauaji ya kimbari dhidi ya Wayazidi ambao wameteseka na kunyanyaswa kutokana na imani yao. Ni wakati wa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza. Lakini wote ni ndugu wamoja. Waamini wa dini mbalimbali wajitahidi kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na utu wema; ni muda wa kujenga na kudumisha ushirikiano na maisha katika jamii. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi, ili kujenga udugu wa watu wote. Huu ni mchakato mgumu na endelevu unaowataka waamini wa dini mbalimbali kuacha chuki na uhasama na kuanza kujadiliana kama watoto wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Vatican inakazia uhuru wa kidini, kwa dini zote: kutambuliwa, kulindwa, kuheshimiwa na kupewa haki zote msingi. Juhudi hizi ziendeleee kuimarishwa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu amekazia umoja, udugu na mshikamano wa kibinadamu unaotambua watu wengine kama mwandani wa safari ya maisha hapa duniani. Amewakumbuka na kuwafariji wale wote waliowapoteza wapendwa wao kutokana na vita, vitendo vya kigaidi, dhuluma na nyanyaso za kidini. Watu wasiokuwa na fursa za ajira; wakimbizi na wahamiaji, wote hawa wanapaswa kuoneshwa mshikamano na upendo wa udugu wa kibinadamu, ili baada ya majanga yote, waibuke wakiwa wamepyaishwa zaidi, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kuboresha uchumi, elimu pamoja na kupambana na umaskini. Mchakato wa udugu wa mshikamano wa kibinadamu, iwe ni fursa ya kupambana na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kuendelea kujikita katika utawala wa sheria; haki, uaminifu, ukweli na uwazi ili kuimarisha mifumo itakayosaidia kufikia lengo hili. Hii ni pamoja na kudumisha siasa safi na utawala bora. Baba Mtakatifu Francisko anasema yuko nchini Iraq kama hujaji wa amani, ili kutekeleza ile ndoto aliyokuwa nayo Mtakatifu Yohane Paulo II. Mwenyezi Mungu daima anawasikiliza waja wake, hivyo basi hata wao wanapaswa kumsikiliza, ili kuondokana na vita, kwa kujikita na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kilio cha wajenzi wa amani, cha maskini na watu wa kawaida kisikike na kujibiwa barabara, ili watu wa Mungu waweze kupata tena fursa ya kuishi, kufanya kazi na kusali kwa amani; kwa kushirikiana na kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene. Lengo kuu ni upatanisho wa kitaifa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia hii, watu wataweza kushiriki katika medani mbalimbali za maisha, kwa kuaminiana, ili kudumisha amani na utulivu. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mchakato wa umoja na ushirikiano wa Kimataifa, usaidie kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuikumba familia ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Mshikamano wa udugu usaidie kuleta usawa wa kiuchumi, amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Baba Mtakatifu anayashukuru na kuyapongeza Mashirika mbalimbali ambayo yamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma msingi kwa maskini na wahitaji zaidi, kama sehemu ya utekelezaji wa upendo, jamii na ujenzi wa amani ya kudumu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yataendelea kutoa huduma kwa watu wa Mungu nchini Iraq, kwa kushirikishana nyajibu bila kuweka masilahi binafsi kisiasa au kiitikadi.

Dini kwa asili ipo kwa ajili ya huduma ya amani na udugu wa kibinadamu. Kamwe, Mwenyezi Mungu hawezi kutumiwa ili kuhalalisha mauaji, vitendo vya kigaidi, dhuluma, nyanyaso pamoja na kuwapeleka watu uhamishoni. Mwenyezi Mungu amewaumba watu wote kwa sura na mfano wake, wakiwa na haki, utu na heshima na kwamba, wanaitwa na kuhamasishwa kutangaza na kushuhudia tunu ya upendo, utashi mwema, amani na utulivu. Kanisa Katoliki nchini Iraq linataka kujizatiti katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, huduma ya upendo na ujenzi wa amani ya kudumu, ili kweli Iraq iweze kuwa ni mahali pa salama. Ushiriki wao kama raia unafumbatwa katika haki zao msingi, uhuru na wajibu kwa kuendelea kutambua tofauti zao msingi kama amana na utajiri wa Iraq. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote ujenzi wa jamii inayosimikwa katika umoja na udugu wa kibinadamu; mshikamano, amani na maridhiano kati ya watu. Daima wajitahidi kuongozwa na hekima na busara, haki na ukweli!

Papa Hotuba Iraq

 

05 March 2021, 16:13