Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Iraq amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa, majandokasisi na makatekista na kuwataka kuwa ni vyombo vya furaha ya Injili licha ya changamoto zilizopo. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Iraq amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa, majandokasisi na makatekista na kuwataka kuwa ni vyombo vya furaha ya Injili licha ya changamoto zilizopo.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Hotuba Kwa Kanisa

Baba Mtakatifu katika hotuba yake pamoja na mambo mengine amekazia zaidi kuhusu: Changamoto za kichungaji ambazo zimeibuliwa na janga la UVIKO-19; Umuhimu wa kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mungu licha ya matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo! Amegusia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kujikita katika umoja na mshikamano wa kidugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, anafanya Hija yake ya 33 ya Kitume nchini Iraq, inayonogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija za kitume ni muhimu sana katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nyenzo ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Serikali mbalimbali duniani. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu akiwa nchini Iraq, Ijumaa tarehe 5 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi na makatekista kutoka Iraq! Baba Mtakatifu katika hotuba yake pamoja na mambo mengine amekazia zaidi kuhusu: Changamoto za kichungaji ambazo zimeibuliwa na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19; Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mungu licha ya matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo! Amegusia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kujikita katika umoja na mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu ametoa Neno kwa Maaskofu, Mapadre, Watawa na Majandokasisi kwa kuwakumbuka na kuwaombea waamini waliouwawa kikatili katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mama wa Mkombozi. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Iraq kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, licha ya matatizo na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao. Wakristo nchini Iraq wanaalikwa kupyaisha tena mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa kujitahidi kumwilisha ndani mwao ujumbe wa msamaha na upatanisho, ili tunu hizi ziweze kupyaishwa tena nchini Iraq. Kumekuwepo na changamoto nyingi za shughuli za kichungaji ambazo zimeibuliwa na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Lakini jambo la msingi ambalo kamwe halipaswi kuwekwa karantini ni ari na moyo wa shughuli za kitume walizorithishwa kutoka zamani za kale. Wasikubali kuathirika na virusi vya kukatisha tamaa. Wawe na ari na moyo wa sala na uaminifu katika maisha na huduma yao kwa watu wa Mungu.

Hii ni kinga tosha itakayowawezesha kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, ili kushirikisha furaha ya Injili kama wafuasi wamisionari wanaotangaza na kushuhudia uwepo na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha, haki na amani; mambo yanayotangazwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha furaha ya Injili inayoweza kuleta mabadiliko na mageuzi makubwa katika maisha ya watu hata katika shida na mahangaiko makubwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika miaka ya hivi karibuni, Iraq imetumbukia katika vita, nyanyaso na dhuluma. Kumekuwepo na ukosefu wa miundombinu msingi kwa ajili ya shughuli za kitume. Ukosefu wa usalama, umepelekea watu wengi kujikuta wakiwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi yao wenyewe. Analishukuru Kanisa kwa kuendelea kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika sekta ya elimu, huduma na ustawi wa jamii.

Upendo wa Kristo Yesu, unawataka kuondokana na ubinafsi na mashindano yasiyokuwa na tija wala mashiko, bali wajitahidi kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na mshikamano. Wakuze na kudumisha majadiliano ya kiekumene, ili wote kwa pamoja waweze kuwa na moyo mmoja, matumaini, mapendo na furaha ya kweli kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika ulimwengu huu uliogawanyika na kusambaratika kutokana na sababu mbalimbali. Umoja na mshikamano uwe ni kielelezo na utambulisho wa Kanisa nchini Iraq. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Iraq kushikamanishwa na kuunganishwa zaidi katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya neema, upendo, toba na msamaha wa kweli unaosimikwa katika majadiliano ya kidugu. Waamini wajifunze kuchukuliana kwa upole na kuendelea kuimarishana nyakati za majaribu na magumu ya maisha. Maaskofu wawe karibu zaidi na Mapadre wao na waamini wao. Wajitahidi kuwa ni Mababa wema wanaoangalia mahitaji yao msingi na kuwatia shime kwa moyo mweupe katika shughuli na mahangaiko yao. Wawasindikize Mapadre wao kwa sala, wawatie moyo kwa shukrani na kuwaongoza katika ukuaji wao, ili hatimaye, mwisho wa siku, wawe ni mfano bora wa Yesu Mchungaji mwema anayewafahamu na kujitoa sadaka kwa ajili ya maisha ya kondoo wake.

Baba Mtakatifu amewaambia watu wa Mungu nchini Iraq, kuitikia na kupyaisha wito wao mbele ya Mungu kwa mwanga wa Maandiko Matakatifu. Wakleri na watawa waoneshe uwepo wao wa karibu kati ya watu wanaowahudumia, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, wazee, watoto na vijana. Wafanye yote haya kwa upendo, unyenyekevu na huruma kwani kwa njia ya huduma ya upendo, Mwenyezi Mungu anawakirimia furaha ya kweli. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waamini waliouwawa kikatili ndani ya Kanisa. Hii ni changamoto ya kuondokana na chuki, uhasama, dhuluma na nyanyaso na badala yake, wawe ni vyombo na wajenzi wa amani na umoja miongoni mwa watu wa Mungu. Vijana wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya upendo, amana, utajiri na matumaini ya Iraq. Waendelee kushikamana na wazee wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Wakleri na watawa watambue kwamba, kabla ya kupewa Daraja Takatifu au kuwekwa wakfu na kuwa watawa, walibatizwa na kutumwa kwenda kuwa ni mitume wamisionari, wito ambao ni sehemu ya historia ya wokovu, changamoto na mwaliko wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.

Papa Maaskofu
05 March 2021, 17:04