Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amefanya hija ya kitume nchini Iraq. Mwaliko kwa waamini wa dini mbalimbali kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Francisko amefanya hija ya kitume nchini Iraq. Mwaliko kwa waamini wa dini mbalimbali kusimama kidete kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Iraq: Haki Msingi za Binadamu

Waamini wa dini zote wanahimizwa kusimama kidete: kulinda na kuheshimu: haki msingi za binadamu. Watambue na kuheshimu uraia wao, kigezo msingi cha watu kuishi kwa amani na utulivu sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Italia inamkaribisha tena Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili! Haki na Amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, Jumatatu, tarehe 8 Machi 2021 amemwambia kwamba, amerejea tena nchini Italia kutoka katika hija yake ya kitume nchini Iraq. Anasema, huko amebahatika kukutana na kuzungumza na Wakristo pamoja na wawakilishi wa dini mbalimbali, ambao wameshuhudia dhamana ya kutaka kuzama zaidi katika ule moyo wa kushirikishana; safari ya majadiliano, amani na utulivu. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka Rais Sergio Mattarella pamoja na watu wote wa Mungu nchini Italia. Mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume.

Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Italia amempongeza Baba Mtakatifu kwa kurejea salama salimini katika hija yake ya kihistoria nchini Iraq. Amekuwa ni Khalifa wa kwanza wa Mtakatifu Petro kutembelea Iraq, chemchemi ya utajiri na amana kubwa ya maisha ya kiroho. Lakini kwa bahati mbaya sana, hawa ni watu waliojaribiwa na kuteseka sana kutokana na vita, uharibifu pamoja na kupata mateso makali sana. Kwa kutambua kwamba, waamini wote hawa ni watoto wa Ibrahimu Baba wa imani, majadiliano ya kidini kwenye Uwanda wa Uru wa Wakaldayo, imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kuwapatia neno la faraja na matumaini.

Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini zote kusimama kidete: kulinda na kuheshimu: haki msingi za binadamu; kwa kuwalinda watu wanyonge na makundi ya watu wachache ndani ya jamii kwa kutambua na kuheshimu uraia wao, kigezo msingi cha watu kuishi kwa amani na utulivu sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Italia, Rais Sergio Mattarella amemkaribisha tena Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili!

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija hii ilifumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, kuhamasisha ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu.

Italia

 

09 March 2021, 15:31