Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuachana na uvivu wa maisha ya kiroho kwa kumwilisha mwanga na mang'amuzi ya Ufufuko wa Kristo katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuachana na uvivu wa maisha ya kiroho kwa kumwilisha mwanga na mang'amuzi ya Ufufuko wa Kristo katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku! 

Papa Francisko: Yesu Anageuka Sura: Acheni Uvivu wa Kiroho!

Juu ya Mlima Yesu akageuka sura yake mbele yao, mavazi yake yakimetameta, kielelezo cha utukufu wake, baada ya mateso na kifo cha Msalaba. Kristo Yesu anawakirimia Mitume wake, mwanga angavu, ili waweze kupita giza nene la mahangaiko yao na kwamba, kifo si hatima ya yote, bali ni mwanzo wa utukufu katika Fumbo la Ufufuko. Mwaliko wa kuondokana na uvivu wa kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tukio la kung’ara kwa Yesu mbele ya Mitume wake kadiri ya Mwinjili Marko linaonesha: Ukuu, utakatifu, uzuri, furaha na chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ni siri ambayo Mitume walitakiwa kuizamisha katika sakafu ya mioyo yao mpaka baada ya Fumbo la Pasaka. Hiki ndicho kielelezo cha Fumbo la Msalaba linalofafanuliwa na Yesu mbele ya wafuasi wake watatu yaani: Petro, Yakobo na Yohane katika tukio hili la kung’ara uso, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa Kanisa. Siku chache kabla ya tukio hili, Kristo Yesu aliwatangazia Mitume wake kwamba, imempasa kupata mateso, kukataliwa na hatimaye, kuuwawa juu la Msalaba! Fundisho hili lilikuwa gumu na tete sana kwa wafuasi wa Kristo waliokuwa karibu naye kiasi cha ndoto yao kutoweka kama umande wa asubuhi. Hawa ni watu waliokuwa na fikra za Masiha mwenye nguvu na mshindi. Wakaingiwa na hofu kuona kwamba, Masiha waliyemtegemea atakamatwa, atateswa na hatimaye kuuwawa kikatiliki kuliko hata “jambazi la kutupwa”.

Ni katika muktadha wa mahangaiko ya ndani, Kristo Yesu akawatwaa Petro, Yakobo na Yohane akawapeleka juu ya mlima mrefu faraghani. Mlima kadiri ya Maandiko Matakatifu ni mahali pa kukutana na Mwenyezi Mungu, mahali panapotenganisha mbingu na nchi; ni mahali ambapo Musa na Manabii waliweza kupata mang’amuzi ya ajabu kwa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu aliwashirikisha Mitume wake watatu mang’amuzi haya kutoka Agano la Kale! Hapa akageuka sura yake mbele yao, mavazi yake yakimetameta, kielelezo cha utukufu wake, baada ya mateso na kifo cha Msalaba. Kristo Yesu anawakirimia Mitume wake, mwanga angavu, ili waweze kupita giza nene la mahangaiko yao na kwamba, kifo si hatima ya maisha yake, kwani huo ni mwanzo wa utukufu katika Fumbo la Ufufuko. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 28 Februari 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mtume Petro baada ya kuonja mang’amuzi haya ya utukufu wa Kristo Yesu, Petro anashangilia na kumwambia Yesu, “Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya”. Mk. 9:5.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwanga wa Pasaka unaowapitisha waamini katika giza la Kipindi cha Kwaresima. Hata katika shida na mahangaiko ya binadamu, mwamini anapaswa kutambua kwamba Kristo Yesu, amefufuka kwa wafu na kamwe hataweza kuruhusu giza na ugumu wa mioyo uwe na neno la mwisho. Matukio kama haya ni kawaida katika maisha ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake, kiasi cha kuogopa ikiwa kama kweli wataweza kufanikiwa na hatimaye kutoka salama salimini. Watu wanatishika sana “wanapokamatwa na kupapaswa” na magonjwa, mateso ya watu wasiokuwa na hatia au Fumbo la kifo linapobisha hodi na kuingia katika maisha yao. Hata katika hija ya maisha ya kiroho na imani, kuna wakati ambapo mwamini anateleza na kuanguka kutokana na kashfa ya Fumbo la Msalaba sanjari na Masharti ya Injili, yanayowataka wafuasi wa Kristo Yesu, kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Injili ya huduma kwa jirani; kupoteza maisha kwa ajili ya upendo badala ya kuyakumbatia na kutaka kuyalinda kwa mafao binafsi.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanahitaji kuwa na mwelekeo mpya wa maisha, kupata mwanga unaoangaza undani wa Fumbo la maisha ya binadamu, ili kuwasaidia kwenda mbali zaidi na mifumo na vigezo vya ulimwengu huu. Wakristo wanaitwa kupanda juu mlimani, ili kutafakari uzuri na utakatifu wa Kristo Mfufuka, unaowasha miale ya moto ili kutoa tafsiri sahihi ya maisha, inayopata chimbuko lake kutoka katika Ushindi wa Fumbo la Pasaka! Wakristo wanapewa angalisho kuhusu maneno ya Mtakatifu Petro: “Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya”. Mk. 9:5; kwani maneno haya yanaweza kuwasukumizia kwenye uvivu wa maisha ya kiroho. Kamwe, haiwezekani watu wachache wakabaki pale juu mlimani, wakiendelea kufaidi utukufu na utakatifu wa Kristo Yesu, ambaye anawarejesha tena “bondeni kwenye machozi”, kati ya ndugu zao na katika hali ya maisha ya kila siku.

Kuna haja kwa waamini kujiangalia wao wenyewe na hivyo kuwa tayari kupambana kufa na kupona na uvivu wa maisha ya kiroho. Waamini kamwe wasiridhike na sala na liturujia zao. Wanapaswa kutambua ukweli wa maisha kwani sala kamwe haziwezi kumwondoa mtu katika mapambano ya maisha na kwamba, mwanga wa imani si kwa ajili ya kupata hisia nzuri za maisha ya kiroho! Waamini wanahamasishwa kufanya mang’amuzi mazito ya kukutana na Kristo Yesu, ili wakiwa wameangaziwa na mwanga wake, waweze kuyanafsisha mahali popote pale na hivyo kuyafanya yang’ae pia mahali popote. Huu ni mwaliko wa kuwasha miale ya moto katika nyoyo za watu; ni chagamoto ya kujivika unyenyekevu na kuwa kama taa ndogo za Injili ili kuwashirikisha wengine upendo na matumaini kwa sababu huu ndio utume wa Mkristo! Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia kuupokea mwanga wa Kristo Yesu kwa mshangao, na hatimaye kuuhifadhi pamoja na kuwashirikisha wengine!

Papa: Uvivu wa Kiroho

 

28 February 2021, 14:32