Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, Jumatatu tarehe 01 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa "Catholic News Serivice" Idara ya Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Jubilei ya Miaka 10o ya uwepo wake. Papa Francisko, Jumatatu tarehe 01 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa "Catholic News Serivice" Idara ya Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Jubilei ya Miaka 10o ya uwepo wake.  (ANSA)

Jubilei ya Miaka 100 ya "Catholic News Service" Nchini Marekani

Papa Francisko: Kanisa linahitaji vyombo vya mawasiliano vitakavyowasaidia watu na hasa vijana wa kizazi kipya kutambua mema na mabaya, kwa kukuza na kukomaza maamuzi makini yanayokita mizizi yake katika ukweli sanjari na kutambua umuhimu wa kuendelea kufanya kazi ili kudumisha haki, maridhiano ya kijamii, kwa kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni unanogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone” Yn. 1:46. Sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane. Haya ni maneno ya Kristo Yesu alipokutana kwa mara ya kwanza na Mitume wake, kielelezo makini cha mawasiliano ya kibinadamu. Ili kutangaza na kushuhudia ukweli wa maisha unaounda historia kuna haja ya kujitosa kimasomaso na kwenda kutazama, kukaa pamoja na wadau mbalimbali, kuwasikiliza, kupokea maoni yao na hatimaye kufungua macho ili kujionea hali halisi. Mawasiliano hayana budi kuwa wazi na ya kweli katika kurasa za magazeti, kwenye mitandao ya kijamii, wakati wa mahubiri na hata katika mawasiliano katika mambo ya kisiasa na kijamii. Njoo uone ni mchakato ambao imani ya Kikristo imeweza kutangazwa na kushuhudiwa!

Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa waandishi wa habari “kuchakarika usiku na mchana ili kutafuta habari”, tukio lile na kwenda na kuona limekua ni mwanzo na chemchemi ya imani, changamoto na mwaliko kwa waandishi wa habari kuwa na ujasiri. Baba Mtakatifu anagusia fursa na mitego iliyoko kwenye tovuti. Hakuna kitu mbadala cha kuona kama mwanadamu. Ni katika muktadha huu wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, Idara ya Habari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, “The Catholic News Service” inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Hii imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Idara ya Habari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Jumatatu tarehe 1 Februari 2021 kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu ameipongeza Idara hii kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa lugha ya Kiingereza. Imekuwa mstari wa mbele kupasha habari kuhusu maisha na utume wa Kanisa; Mamlaka ya Kanisa katika kutangaza Injili sanjari na kushuhudia upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kuna uwezekano mkubwa wa kukumbana na habari za kughushi na kupotosha. Lakini, kwa wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa, wanapaswa kujizatiti kutafuta ukweli na kuufanya ufahamike, huku ukinogeshwa zaidi na kauli mbiu: haki, uaminifu na habari. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza kwa kazi kubwa waliyokwisha kuitenda na anapenda kuwatia shime, ili waendeleze mchakato wa majadiliano kati ya watu na jumuiya. Kanisa linahitaji vyombo vya mawasiliano vitakavyowasaidia watu na hasa vijana wa kizazi kipya kutambua mema na mabaya, kwa kukuza na kukomaza maamuzi makini yanayokita mizizi yake katika ukweli sanjari na kutambua umuhimu wa kuendelea kufanya kazi ili kudumisha haki, maridhiano ya kijamii, kwa kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika umoja na mshikamano na Idara ya Catholic News Service, wataendelea kutekeleza huduma yao katika ukweli, unyenyekevu na uwajibikaji mkubwa. Mwishoni, amewahakikishia sala zake, wanapotekeleza utume huu nyeti katika maisha na utume wa Kanisa nchini Marekani.

Mawasiliano USA
01 February 2021, 15:31