Tafuta

Vatican News
Siku ya Wagonjwa Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992. Kauli mbiu ya Maadhimisho kwa Mwaka 2021 ni "Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu" Mt. 23: 8 Siku ya Wagonjwa Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992. Kauli mbiu ya Maadhimisho kwa Mwaka 2021 ni "Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu" Mt. 23: 8  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Wagonjwa Duniani 2021

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 29 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa tareh 11 Februari 2021, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes inaongozwa na kauli mbiu “Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu”: Mt. 23:8: Mahusiano ya kuaminiana kama msingi wa mwongozo wa huduma kwa wagonjwa. Ni Siku ya Sala, Tafakari na Mshikamano wa Udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wagonjwa Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993. Hii ni siku maalum ambayo Mama Kanisa anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa wagonjwa bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Ni wakati wa kusali na kuwaombea wagonjwa na familia zao; kwa kuwaenzi wahudumu katika sekta ya afya pamoja na watu wanaojitolea usiku na mchana, kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na wazee sehemu mbali mbali za dunia. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito wa huduma, ili kuweza kuwasindikiza wagonjwa na wanaoteseka katika shida na mahangaiko yao. Ni fursa kwa Kanisa kupyaisha tena na tena huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa na wazee. Mababa wa Kanisa wanasema, kwa Mpako Mtakatifu wa wagonjwa na sala za Makuhani, Mama Kanisa huwakabidhi wagonjwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Mama Kanisa anawaalika wagonjwa na wazee kujiunga kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo Yesu, ili kutoa mchango wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Rej. KKK. 1499.

Mpako wa wagonjwa hutimiliza kufananishwa kwa waamini kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama Sakramenti ya Ubatizo inavyoanza. Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa na wazee sehemu mbalimbali za dunia! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 29 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa tarehe 11 Februari 2021, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes inaongozwa na kauli mbiu “Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu”: Mt. 23:8: Mahusiano ya kuaminiana kama msingi wa mwongozo wa huduma kwa wagonjwa. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwakumbuka na kuwaombea watu wote walioguswa na kutikiswa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Korona, UVIKO-19, hasa zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, waonje na kuguswa na uwepo wa karibu pamoja na upendo wa Kanisa kwa wagonjwa wote.

Baba Mtakatifu anasema kauli mbiu ya mwaka huu 2021 ni sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo kuhusu laana kwa Mafarisayo wanaoshindwa kunafsisha kile wanachohubiri. Imani ambayo waamini wanakiri na kuitangaza inapaswa kunafsishwa katika matendo adili, vinginevyo waamini wanaweza kutumbukia katika tabia ya kujiabudu wenyewe. Ndiyo maana Kristo Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwa kusema, “Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu”. Mt. 23:8. Kristo Yesu anakemea tabia ya unafiki inayowazuia watu kushindwa kustawi kama watoto wa Baba mmoja wanaoitwa kuishi udugu wa kibinadamu, kwa njia ya matendo kinyume kabisa cha tabia ya unafiki. Huu ni mwaliko wa kusimama na kusikiliza; kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii; kwa kuwaonea jirani huruma na mapendo, ili kutoa nafasi ya kuguswa na mahangaiko yao, ili hatimaye, kuwasaidia. Udhaifu wa kibinadamu unawasukuma kutambua kwamba kila mtu anahitaji msaada kutoka kwa jirani yake na kama viumbe, wote wanamtegemea Mwenyezi Mungu.

Katika hali na mazingira kama haya, binadamu anajiona kuwa hana nguvu kwa sababu afya yake haitegemei sana uwezo wake. Ugonjwa unaibua swali msingi la kiimani mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusu maana ya maisha! Si rahisi sana kuweza kupata majibu muafaka wa swali hili. Maandiko Matakatifu yanaweka mbele ya macho ya waamini picha ya majaribu na misiba iliyomkumba Ayubu, jinsi alivyoshutumiwa na mke pamoja na marafiki zake, kiasi cha kutamani kutokuwapo duniani. Ayubu anapuuza unafiki na kujiaminisha na kuendelea kuwa mwaminifu mbele ya Mungu na jirani zake, kiasi cha kupokea ahadi ya kufanywa upya na kwa kuona na kutubu. Moyo wa Ayubu ulijeruhiwa sana, lakini pia uliponywa, kiasi hata cha kukiri na kusema: “Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio, bali sasa jicho langu linakuona”. Ayu. 42:5. Ugonjwa una sura nyingi katika maisha ya mwanadamu. Ni sura ya wagonjwa wote, wale wanaohisi kupuuzwa, wanaotengwa pamoja na kuteseka kutokana na dhambi jamii zinazowakosesha haki zao msingi. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, umesababisha ukosefu wa usawa katika mfumo wa huduma ya afya pamoja na kuonesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kuwahudumia wagonjwa.

Wazee na maskini hawana uwezo wa kupata tiba wala kuhudumiwa katika hali ya usawa. Haya ni matokeo ya maamuzi ya kisiasa, matumizi ya rasilimali fedha pamoja na uwajibikaji wa viongozi husika. Mchakato wa uwekezaji katika sekta ya afya sanjari na huduma ya afya kwa wagonjwa inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa kwa kutambua kwamba, afya bora ni sehemu ya mafao ya wengi. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umepelekea pia wafanyakazi katika sekta ya afya kujisadaka zaidi kwa kuendelea kuonesha ukarimu. Hawa ni madaktari na wafanyakazi katika sekta, watu wa kujitolea, mapadre na watawa. Wote hawa wamekuwa mstari wa mbele: kusaidia, kutibu, kufariji pamoja na kuwahudumia wagonjwa pamoja na familia zao. Huduma hii imetolewa kwa weledi mkubwa, sadaka binafsi, uwajibikaji sanjari na upendo kwa jirani. Umati mkubwa wa watu haukuwageuzia kisogo watu waliokuwa wanateseka, bali uliamua kusimama nao katika mateso kwa kuwatambua kwamba ni jirani wema na watu wa familia moja ya binadamu.

Umoja na mafungamano haya ya kijamii ni muhimu sana kwa kutoa msaada na faraja kwa wagonjwa katika mateso yao. Hiki ni kielelezo cha alama ya upendo wa Kristo Yesu, kama Msamaria mwema. Msamaria alipomwona huyu mtu nusu mfu, tendo la kwanza: Alimwonea huruma, akashuka juu ya mnyama wake, akamkaribia, akampa huduma ya kwanza, kisha akampeleka nyumba ya kutunza wagonjwa na kulipa gharama zake huku akiahidi atalipa pia gharama zitakazoongezeka. Kkristo Yesu ni Msamaria mwema kwa watu waliojeruhiwa kwa dhambi. Waamini wakiwa wameungana na Kristo Yesu kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, wanaitwa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma, kwa kuwapenda watu waliodhaifu, wagonjwa na wote wanaoteseka. Rej. Jn. 13: 35-35. Waamini wanapata mang’amuzi ya ukaribu wa Yesu kama mtu binafsi na kama Jumuiya. Kimsingi huu ndio upendo wa udugu katika Kristo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakazia kwa namna ya pekee kabisa mshikamano wa kidugu katika huduma, kwa kuwahudumia jirani zao, familia, jamii na watu wote katika ujumla wao.

Mchakato wa huduma ya kidugu iwasaidie watu kuondokana na matamanio binafsi na uchu wa madaraka kwa kuwatazama machoni na kugusa madonda yao ili waweze kuhisi uwepo wao wa karibu na hata ikibidi kuteseka pamoja nao, kama kielelezo cha uwepo wa karibu. Huduma ya kidugu kamwe haiwezi kufumbatwa katika nadharia tu, bali huduma ni kwa ajili ya watu. Ili tiba iweze kupata ufanisi mkubwa, kuna haja ya kuwepo pia na mahusiano ya karibu na mgonjwa. Kumbe, madaktari, wahudumu wa sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uponyaji unaosimikwa katika mahusiano ya uaminifu kati yao. Mwelekeo huu anasema Baba Mtakatifu Francisko unaunda agano kati ya watu wanaohitaji huduma ya afya na wale wanaotoa huduma hii kwa jamii. Hili ni agano linalokita mizizi yake katika kuaminiana, kuheshimiana, ukweli, uwazi na uwapo! Mwelekeo huu, utasaidia kuondokana na tabia ya watu kutaka kujilinda na hivyo kukuza ari na moyo wa kuthamini utu wa mgonjwa. Huu ni wito wa kulinda taaluma ya wafanyakazi katika sekta ya afya na hivyo kukuza uhusiano na mafungamano mema na familia za wagonjwa!

Kimsingi huu ndio upendo katika Kristo Yessu ambao umeshuhudiwa na maelfu ya watakatifu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni chimbuko la upendo linalotoa maana ya kweli katika maisha ya wagonjwa na wale wanaohudumia. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Kristo Yesu anaponya kwa watu kukutana naye; kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na mtu binafsi; mambo ambayo yanapata maana ya kweli katika imani kwa wale wanaokubali. Kristo Yesu anawaponya na kuwaokoa watu kutokana na imani yao “Nenda zako imani yako imekuokoa”. Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani ijenga pia na kudumisha mahusiano na mafungamano na wagonjwa. Jamii makini inapimwa kwa njia ya udugu wa upendo kwa watu wake wanaoteseka. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanafikia lengo hili, ili kamwe asiwepo mtu anayehisi upweke hasi, kutengwa au kupuuuzwa.

Mwishoni mwa ujumbe wake unaoongozwa kwa kauli mbiu “Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu”: Mt. 23:8: Mahusiano ya kuaminiana kama msingi wa mwongozo wa huduma kwa wagonjwa”: Baba Mtakatifu Francisko, anawaaminisha wagonjwa wote, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa. Kutoka katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes na Madhabahu ya Bikira Maria yaliyo enea sehemu mbalimbali za dunia, awe ni msaada wa imani na matumaini, awasaidie watu kuhudumiana katika upendo wa kidugu. Wote hawa, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapatia baraka zake za Kitume.

Siku ya Wagonjwa Duniani 2021

 

 

10 February 2021, 16:20