Tafuta

Vatican News
Tarehe 22 Februari ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja na mshikamano katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tarehe 22 Februari ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja na mshikamano katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.  (Vatican Media)

Ukulu wa Mtakatifu Petro: Umoja Katika Imani, Maadili na Utu Wema

Ukulu wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha mamlaka aliyopewa na Yesu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika kifungo cha upendo. Mtume Petro alikirimiwa neema ya pekee iliyomwezesha kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu. Waandamizi wake, walipewa dhamana ya kushuhudia: huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili na yanayojitegemea na ya jumla kwa ajili ya huduma ya roho za watu “Curam animalum”. Hivyo basi, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote na ya Kanisa zima na pia ya Makanisa mahalia, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Kwa upande mwingine na Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus Dominum, n. 2-3.

Ni katika muktadha huu, kila mwaka ifikapo tarehe 22 Februari, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, aliyemkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu mwenyewe akamthibitishia Ukulu huu kwa kumwambia “Wewe ndiwe Petro na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda”. Mt. 16:18. Ukulu wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha mamlaka aliyopewa na Kristo Yesu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika kifungo cha upendo. Mtume Petro alikirimiwa neema ya pekee iliyomwezesha kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kupewa funguo, kama Askofu wa kwanza wa Roma na baada yake wako waandamizi wake, waliopewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia: huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Maadhimisho haya ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho haya iwe ni fursa kwa ajili ya kuombea umoja na mshikamano wa Kanisa katika masuala, imani, maadili na utu wema! Tumkumbuke na kumwombea kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili daima aweze kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Ili kwamba, akisha imarika, aweze kuwaimarisha pia ndugu zake katika Kristo katika misingi ya imani, matumaini na mapendo.

Ukulu wa Mt. Petro

 

 

 

20 February 2021, 16:24