Tafuta

Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoianzisha Siku hii ili kutafakari wito, maisha na changamoto za watawa duniani! Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoianzisha Siku hii ili kutafakari wito, maisha na changamoto za watawa duniani! 

Sikukuu Ya Kutolewa Bwana Hekaluni: Miaka 25 ya Siku Ya Watawa Duniani!

Sikukuu ya kutolewa Bwana Hekaluni inaadhimishwa baada ya siku 40 tangu alipozaliwa Yesu. Kadiri ya sheria ya Musa, Yesu anatolewa Hekaluni. Hili tukio muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho kwani hapa Mwenyezi Mungu anakwenda kukutana na watoto wake, sehemu ya utimilifu wa ahadi ya ukombozi, kwa ujio wa Kristo wa Bwana. Kumbe, hii ni siku ya watu kukutana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 2 Februari 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, Sanjari na Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoanzisha Siku ya Watawa Duniani. Sikukuu ya kutolewa Bwana Hekaluni inaadhimishwa baada ya siku 40 tangu alipozaliwa Mtoto Yesu. Kadiri ya sheria ya Musa, Kristo Yesu anatolewa Hekaluni. Hili tukio muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho kwani hapa Mwenyezi Mungu anakwenda kukutana na watoto wake, sehemu ya utimilifu wa ahadi ya ukombozi, kwa ujio wa Kristo wa Bwana. Kumbe, hii ni siku ya watu kukutana. Mzee Simeoni na Ana wakiwa wameongozwa na Roho Mtakatifu wanamtambua Kristo Yesu kuwa ni Masiha wa Bwana. Mzee Simeoni akamshukuru Mwenyezi Mungu kwa utenzi wa sifa kwani amewawezesha kuuona wokovu, nuru na utukufu kwa watu wake Israeli. Huu ndio utenzi wa Mzee Simeoni maarufu kama: “Nunc dimittis servum tuum, Domine, secundum verbum tuum in pace: Quia viderunt oculi mei salutare tuum. Quod parasti ante faciem omnium populorum: Lumen ad revelationem gentium, et gloriam plebis tuae Israel.”

Yaani: “Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.” Mzee Simeoni katika ufukara wa Mtoto Yesu anauona wokovu wa watu wa Mungu. Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa. Rej. LK 2:32; Is. 49:6. Hapa Mzee Simeoni anawawakilisha binadamu wote, wanaoshuhudia utimilifu wa wokovu wa Mungu.  Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni imekuwa ikiadhimishwa na Makanisa ya Mashariki tangu Karne ya IV na ilijulikana kama Sikukuu ya watu kukutana. Kunako Karne VI Sikukuu hii ikaanza pia kuadhimishwa kwa Makanisa ya Magharibi kama siku ya toba na wongofu wa ndani. Ndiyo maana watawa wanaanza maadhimisho haya kwa kubariki mishumaa na kufanya maandamano. Siku hii inajulikana kama “Candelora”.

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Jubilei ya Miaka 25 ya Siku ya Watawa Duniani, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linakazia umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo, kama mlango wa maisha na utume wa Kanisa unaowawezesha waamini kushiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutembea katika Mwanga wa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yawe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, tayari kutembea kwa pamoja kama watoto wa Mwanga. Iwe ni nafasi ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Hii ni nafasi ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, tayari kuwashirikisha wengine chemchemi hii ya furaha inayoibuka kutoka Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Kristo Yesu awawezeshe waamini na kwa namna ya pekee watawa kufungua macho yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kuwekwa wakfu.

Hii ni fursa ya kupyaisha tena imani kwa kutambua uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19) kwa watawa wengi na hasa wazee, umekuwa ni changamoto si tu ya kijamii na kiuchumi bali imegusa na kutikisa maisha na imani ya watawa wengi. Hawa ni watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, na hasa zaidi: maskini, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji. Uwepo wao, umekuwa ni chemchemi na mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Maadhimisho haya yapyaishe tena maisha ya sadaka na majitoleo ya watawa sehemu mbalimbali za dunia! Watambue daima kwamba, wito, maisha na utume wao kama watawa ni kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Watawa 25 Yrs
02 February 2021, 17:04