Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu yamenogeshwa na ujumbe kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa: Haki, Amani, Mshikamano na Mafungamano. Maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu yamenogeshwa na ujumbe kutoka kwa viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Kimataifa: Haki, Amani, Mshikamano na Mafungamano.  (Vatican Media)

Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu: Ujumbe wa Viongozi!

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 4 Februari 2021 imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Jumuiya ya Kimataifa imetoa pia tuzo kwa watu na taasisi ambazo zinaendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Katika kipindi cha Mwaka 2019 Baba Mtakatifu alifanya hija ya kitume nchini Morocco na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu ambako kuna idadi kubwa ya waaamini wa dini ya Kiislam. Lengo lilikuwa ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili waamini wa dini hizi mbili waweze kufahamiana, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Al Malik al- Kamil kunako mwaka 1219.

Ni katika muktadha wa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Jumuiya ya Kimataifa kwa mara ya kwanza hapo tarehe 4 Februari 2021 imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Jumuiya ya Kimataifa imetoa pia tuzo kwa watu na taasisi ambazo zinaendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika hotuba yake kwenye maadhimisho haya, amezishukuru nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kuridhia kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Hizi ni juhudi zilizofanikishwa zaidi na Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Misri. Lengo ni kudumisha amani na maridhiano miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Haya ni matunda ya ushirikiano na majadiliano ya kidini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Azimio hili linapata chimbuko lake kutoka katika misingi ya imani inayonafsishwa katika mshikamano wa kibinadamu.

Umoja wa Mataifa unawapongeza viongozi hawa wa dini kwa kunogesha majadiliano ya kidini, ili kudumisha heshima na maridhiano. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya maisha ya mwanadamu, udugu wa kibinadamu unahitajika zaidi. Hii inatokana na kukithiri kwa mifumo mbali mbali ya ubaguzi, vitendo vya kihalifu, chuki, uhasama na misimamo mikali ya kidini. Katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu, iwe ni fursa ya kunogesha majadiliano ya kidini na kitamaduni; kwa kukzaia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maadhimisho haya yamefanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii na kurushwa mubashara na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan: “The Zayed Award for Human Fraternity’s (ZAHF) imetolewa kwa mara ya kwanza kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Mama Latifa Ibn Ziaten, Mwanaharakati kutoka Ufaransa.

Tuzo hii inatambua mchango wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2017, ameendelea kujielekeza zaidi katika ujenzi wa misingi ya; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili kudumisha usalama na mshikamano wa Kimataifa. Ameendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19), kwa kujikita katika amani, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kujielekeza zaidi katika mapambano dhidi ya UVIKO-19. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, amepokea tuzo hii kwa heshima kubwa, ili kuendelea kujikita zaidi katika mchakato wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tuzo hii inaelekezwa zaidi kwenye huduma zinazotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji. Mama Latifa Ibn Ziaten ni “Mwanamke wa shoka” ambaye amejipambanua kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini dhidi ya misimamo mikali ya kidini na kiimani, baada ya kumpoteza mtoto wake wa pekee kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika kunako mwaka 2012. Ni mwanaharakati anayeendelea kusimama kidete kutangaza na kushuhudia: amani, majadiliano ya kidini pamoja na kuheshimiana.

Kwa upande wake, Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, amesema, ni heshima kubwa kushirikiana na kushikamana na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu sehemu mbalimbali za dunia, ili kuimarisha: udugu wa kibinadamu, amani ya kudumu, ushirikiano wa kimataifa pamoja na kuondokana na dhana ya vita. Ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, upatanisho na amani ya kweli dhidi ya chuki, uhasama na uchu wa mali na madaraka. Tangu sasa kila mwaka ifikapo tarehe 4 Februari, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa watakuwa wanakumbushwa umuhimu wa kuendelea kuimarisha misingi ya udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja na wanayo haki ya kuishi katika mazingira ya amani.

Viongozi wengine walioshiriki katika mkutano huu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii ni pamoja na: Jaji Abdel Salam, Catherine Samba Panza, aliyewahi kuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, CAR, Muhammad Jusf Kalla, aliyewahi kuwa Rais wa Indonesia. Kwa upande wake, Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani ambaye amegusia umuhimu wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu, kama kikolezo cha mshikamano, umoja na udugu wa kibinadamu. Viongozi wengine wamekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini, maridhiano, heshima, utu, na haki msingi za binadamu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuanzisha Siku hii inayoonesha umuhimu wa umoja, mshikamano na mafungamano ya familia ya binadamu katika ujumla wake, licha ya tofauti zao msingi. Hapa kuna haja ya kukazia zaidi tunu msingi za maisha ya kiutu, kijamii na kiroho; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video katika maadhimisho haya anakazia udugu wa kibinadamu. Kwa namna ya pekee, anamshukuru na kumpongeza Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, ambaye amekuwa kwa hakika mwandani wa changamoto na hatari katika mapambano ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Anamshukuru kwa mchango wake mkubwa katika kuhariri Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju hapo tarehe 4 Februari 2019 huko mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Uwepo wa Dr. Ahmad Al-Tayyib, umekuwa msaada mkubwa na ushuhuda wa ujasiri kwa Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Hii ilikuwa ni dhamana nyeti, lakini Dr. Ahmad Al-Tayyib ameitekeleza na hivyo kwa pamoja kuweza kusaidiana. Mchakato huu umeendelea kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anamshukuru pia Sheikh Mohammed Bin Zayed kwa jitihada zake zote ili kufanikisha safari hii ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Aliamini na kuwaamini wadau katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Katika shukrani hizi, Baba Mtakatifu anampongeza pia Jaji Abdel Salam, mchapakazi hodari na kiongozi mwenye mawazo mapana, aliyewatia shime kusonga mbele pasi na mawaa, kiasi kwamba, leo hii, udugu wa kibinadamu ni mpaka mpya wa ubinadamu. Hapa hakuna cha uchaguzi, au ni kushikamana na kuwa wamoja kama ndugu, au wote kuangamizana na kupotea kama “ndoto ya mchana”. Hakuna tena muda wa kuangaliana kwa “jicho la kengeza”, wala kunawa mikono kwamba, hakuna anayehusika au kujiweka pembeni! Wote ni ndugu wamoja, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika ulimwengu mamboleo. Udugu wa kibinadamu maana yake ni kushikamana, kusaidiana, kuthaminiana na kuheshimiana hata katika tofauti msingi. Majadiliano ni muhimu katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwani wote ni watoto wa Baba mmoja, Mungu Mwenyezi. Ni watu wenye tamaduni tofauti, lakini wote ni ndugu wamoja. Kwa kuheshimu tamaduni, mapokeo na mahali anapotoka mtu, mambo yote haya yasaidie mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kusikilizana kwa makini na kukaribishana katika ukweli na uwazi. Huu ni mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii, vinginevyo, watu watageuka na kuwa maadui. Hakuna sababu ya kuwa na vita, ili kujenga uadui, inatosha tu kutomjali wala kumthamini jirani yako na huo ukawa ni mwanzo wa uadui.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza Dr. Ahmad Al-Tayyib, kwa msaada na ushuhuda wake wenye mvuto na mashiko, lakini zaidi kwa kutembea kwa pamoja kama ndugu wamoja. Tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza tuzo la Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulioanzishwa tarehe 2 Desemba 1971 imetolewa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri. Viongozi hawa ndio waasisi pia wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu. Tuzo hii pamoja na mambo mengine, inataka kunogesha jitihada za watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali zinazojipambanua katika kutafuta, kujenga na kukuza mahusiano na mafungamano ya kibinadamu; madaraja ya majadiliano ya kidini sehemu mbalimbali za dunia; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa. Kimsingi Tuzo hii ni alama ya ushirikiano na mshikamano kati ya waamini wa dini mbalimbali wanaojipambanua kwa huduma kwa ajili ya binadamu wote!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru pia Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia tuzo pamoja na jitihada zake mbali mbali zinazopania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; mambo yanayoweza kupatikana ikiwa kama watu wanao ule moyo wa udugu. Ni kiongozi ambaye amejipambanua kwa kusadaka maisha yake, ili watu wote waweze kujisikia kuwa ni ndugu wamoja. Huu ni wakati wa kupandikiza maneno ya mbegu ya amani ili kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu. Hizi ni juhudi zilizotekelezwa kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu inayoundwa na wajumbe wafuatao: Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Aliyekuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu.

Wakati huo huo, Tuzo ya Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan, Muasisi wa Umoja wa Falme za Kiarabu inaundwa na wajumbe wafuatao: Jaji Mohamed Abdelsalam, Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya HCHF. Bwana Adama Dieng, Mshauri mstaafu wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kuzuia mauaji ya kimbari. Bwana Michaelle Jean, Gavana na Amiri Jeshi mkuu wa Canada. Mheshimiwa Muhammad Jusuf Kalla, Rais mstaafu wa Indonesia. Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama Kuu ya Kanisa: “The Supreme Tribunal of the Apostolic Signatura” pamoja na Mama Catherine Samba-Panza, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, CAR.

Viongozi wa Kimataifa

 

06 February 2021, 08:23