Tafuta

Maadhimisho ya Siku ta 65 ya Kongamano la Elimu ya Dini Shuleni kwa mwaka 2021 yamenogeshwa na kauli mbiu ""Tangaza Ahadi", Jubilei ya Miaka 50 ya Siku ya Vijana Kitaifa. Kuna Ujumbe wa Papa Francisko. Maadhimisho ya Siku ta 65 ya Kongamano la Elimu ya Dini Shuleni kwa mwaka 2021 yamenogeshwa na kauli mbiu ""Tangaza Ahadi", Jubilei ya Miaka 50 ya Siku ya Vijana Kitaifa. Kuna Ujumbe wa Papa Francisko. 

Papa Francisko: Umuhimu wa Somo la Dini kwa Waamini

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa Kongamano la Elimu ya Dini Jimbo Kuu la Los Angeles nchini Marekani amekazia zaidi juu ya uaminifu wa Mungu katika kutekeleza ahadi zake; ushuhuda wa upendo unaofumbatwa katika: ujirani mwema, huduma na sadaka katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, vijana ni chemchemi ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Elimu ya dini shuleni ni muhimu sana katika mchakato wa kusaidia kuwalea na kuwafunda watoto tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema dhidi ya mmomong’onyoko wa kimaadili unaoendelea kuikumba jamii kwa kasi ya ajabu hasa kutokana na athari kubwa za utandawazi, ukanimungu na unafsia. Kuna haja ya kukazia, kanuni maadili, utu, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, mambo ambayo kwa sasa yanalega lega kutokana na watu wengi kujikita katika uhuru usiokuwa na mipaka. Kanisa kwa upande wake, halina budi kuendelea kuwekeza katika utume wa maisha ya ndoa na familia, ili kuimarisha tunu msingi za ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Kanisa dogo la nyumbani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko Juu ya Elimu ya Kikristo wanasema, kati ya vyombo vyote vya kukuza elimu shule inao umuhimu wa pekee. Kutokana na lengo na wajibu wake, pamoja na kupevusha kwa bidii nyingi wepesi wa akili, inakuza pia uwezo wa kubainisha mambo. Inashirikisha urithi wa utamaduni wa vizazi vilivyotangulia; inasisitiza umuhimu wa tunu mbalimbali; inaandaa kwa maisha ya kikazi. Pamoja na hayo hustawisha uhusiano wa kirafiki kati ya wanafunzi wenye tabia na hali zinazotofautiana, na hivyo inakuza uelewano kati yao.

Aidha, shule yenyewe inakuwa kituo ambapo kazi na ustawi wake lazima visimamiwe kwa ushirikiano wa wazazi, walimu, vyama vya aina mbalimbali vyenye malengo ya kiutamaduni, kisiasa ama kidini, serikali na jamii yote kwa jumla. Ule wito wa wale wote ambao, kwa kushirikiana na wazazi katika wajibu wao na kwa kufanya kazi kwa niaba ya jumuiya nzima, wanajipatia wajibu wa kufundisha shuleni, kweli ni wito bora na wenye maana kubwa. Wito wa namna hiyo unahitaji vipaji vya pekee vya akili na vya moyo, maandalizi ya makini sana, uwezo mwepesi na wa kudumu wa kujipyaisha na kujirekebisha. Rej. G E, 19. Kongamano la Elimu ya Dini Jimbo Kuu la Los Angeles nchini Marekani “The Los Angeles Religious Education Congress (REC)” ni tukio lililoanzishwa kunako mwaka 1956 na limekuwa likihudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Los Angeles nchini Marekani. Kumbe, kwa mwaka 2021 maadhimisho haya ni 65. Maadhimisho haya yamezinduliwa rasmi tarehe 19 na kilele chake ni tarehe 21 Februari 2021, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Proclaim the Promise” yaani “Tangaza Ahadi”. Tarehe 18 Februari 2021 watu wa Mungu nchini Marekani wameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Siku ya Vijana Kitaifa.

Kutokana na kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 maadhimisho yote haya yanafanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitando ya kijamii na hivyo kuwafikia watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa Kongamano la Elimu ya Dini Jimbo Kuu la Los Angeles nchini Marekani amekazia zaidi juu ya uaminifu wa Mungu katika kutekeleza ahadi zake; ushuhuda wa upendo unaofumbatwa katika: ujirani mwema, huduma na sadaka katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, vijana ni chemchemi ya matumaini. Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe wa Kongamano la Elimu ya Dini Jimbo Kuu la Los Angeles nchini Marekani kwa kufanya kumbukizi la miaka 65 tangu kuasisiwa kwake na Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Vijana Kitaifa. Hiki ni kipindi kigumu sana katika maisha ya watu wangi kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Lakini, jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kutangaza na kushuhudia uaminifu wa Mungu ambao umefunuliwa kwa namna ya pekee na Kristo Yesu, chimbuko la kilele cha umoja, nia na shauri moja. Rej. 1 Kor. 1: 9-11.

Waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, kila mtu katika nafsi yake, anabeba ndani mwake ahadi ya Mungu inayoweza kusaidia mchakato wa mahusiano mapya; kiakili, kitamaduni na kiroho. Janga la Virusi vya Korana, UVIKO-19 limesababisha madhara makubwa katika maisha na historia ya watu na jamii katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja ya kukaza uso na kuangalia ya mbeleni kwa matumaini zaidi, hali inayohitaji nguvu na majitoleo ya watu wote, mintarafu upendo na mshikamano kama ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Msamaria mwema. Umoja na mafungamano haya ya kijamii ni muhimu sana ili kutoa msaada na faraja kwa watu walioathirika na na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hiki ni kielelezo cha alama ya upendo wa Kristo Yesu, kama Msamaria mwema. Msamaria alipomwona huyu mtu nusu mfu, tendo la kwanza: Alimwonea huruma, akashuka juu ya mnyama wake, akamkaribia, akampa huduma ya kwanza, kisha akampeleka nyumba ya kutunza wagonjwa na kulipa gharama zake huku akiahidi atalipa pia gharama zitakazoongezeka. Kuna na mashuhuda wa Injili ya imani, matumaini na mapendo ambao wameacha alama ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wakati wote huu wa mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushuhuda wa upendo unakita mizizi yake katika: ujirani mwema, huduma na sadaka katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama njia muafaka ya utekelezaji wa ahadi ya Mungu. Kanuni msingi inayoongoza mapambano haya ni kwamba, kamwe watu hawataweza kutoka kwenye janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 wakiwa jinsi walivyo. Au wanaweza kuwa ni watu wema zaidi au wakawa wamekengeuka na kutopea katika ubinafsi. Katika janga hili, watu wa Mungu wanapaswa kujifunza kuona jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anajifunua kwa waja wake. Huyu ni Mungu mkuu ambaye hatikisiki hata kidogo, ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha anajionesha katika ukuu, lakini pia anamwinamia binadamu katika udogo na udhaifu wake wa kibinadamu. Hii ni changamoto ya kuchagua na kuambata safari ambayo mwanadamu anataka kuikamilisha.

Ni muda muafaka wa kutambua na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu, nguzo msingi ya udugu wa kibinadamu. Kuna haja ya kuwa na jumuiya inayowaunga watu mkono na kwa njia hii, wanaweza kusaidiana na kusumbukiana katika kukabiliana na changamoto za maisha, tayari kukaza shingo ili kusonga mbele. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza vijana wa kizazi kipya wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Vijana Kitaifa. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini inayosimikwa katika utu wa binadamu, tofauti kabisa na mazingira, historia na hali yake ya maisha. Ni vyema ikiwa kama vijana wanaota ndota na ndoto hii inamwilishwa kati yao. Tofauti zao msingi ziwawezeshe kujisikia kwamba, wote ni ndugu wamoja. Haya ndiyo matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana wanaohudhuria Kongamano la Elimu ya Dini Jimbo Kuu la Los Angeles nchini Marekani.

Kwa upande wake, Askofu mkuu José H. Gomez wa Jimbo kuu la Los Angeles anasema, janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha athari kubwa sana katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Lakini ni jambo muhimu sana, kwa waamini kujielekeza na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake. Bado waamini wanapaswa kutangaza na kushuhudia ahadi za Mungu kati ya watu wa Mataifa hata katika nyakati hizi za maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hii inatokana na ukweli kwamba, mchakato wa Uinjilishaji mpya unafumbatwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na ushuhuda wa utakatifu wa maisha kwa kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani.

Kongamano Elimu

 

22 February 2021, 14:33