Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Februari 2021 amekazia umuhimu wa sala katika liturujia na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kristo Yesu ni kiini cha Liturujia ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Februari 2021 amekazia umuhimu wa sala katika liturujia na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kristo Yesu ni kiini cha Liturujia ya Kanisa. 

Papa Francisko Umuhimu wa Sala Katika Liturujia ya Kanisa

Mababa wa Kanisa wanasema katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa, utume wa Yesu na wa Roho Mtakatifu ambao unatangaza, unatekeleza na kushirikisha fumbo la wokovu, unaendelezwa katika moyo unaosali. Sala inazamisha ndani ya Liturujia na kuitumia wakati na baada ya adhimisho lake. sala daima ni sala ya Kanisa, ni ushirika pamoja na Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia takatifu ya Kanisa kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu na watu wa milki ya Mungu. Liturujia ni chemchemi ya roho ya kweli ya kikristo kwani inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Lengo ni umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu. Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo mwenyewe. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Liturujia, Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Hili ni tendo takatifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, lengo kuu la Liturujia ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa!

Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Februari 2021 kuhusu Sala: Kusali katika Liturujia amegusia umuhimu wa Liturujia, Maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa na hatimaye, Umuhimu wa Sala Binafsi. Liturujia ya Kanisa inabeba umuhimu wa pekee katika maisha ya kiroho, kumbe, waamini wanapaswa kujifunza vyema mfumo bora zaidi wa sala unaomwilishwa katika Liturujia. Inasikitisha kuona kwamba, licha ya waamini kushiriki mara nyingi katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, lakini kwa bahati mbaya hawajaweza kufaidika zaidi kwa ushiriki wao ili kuboresha imani yao, ikilinganishwa na vyanzo vingine vya ibada. Tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika Liturujia ya Kanisa na umuhimu wake katika maisha ya waamini. Kiini cha Liturujia ya Kanisa ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Sala ya Wakristo inamwilishwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Sakramenti za Kanisa pamoja na Maadhimisho ya Liturujia mbalimbali za Kanisa. Kwa njia ya Liturujia ya Kanisa Kristo Yesu anakuwa ni njia ya wokovu, kumbe, kuna haja ya kusali kwa kutumia mwili, ili mwili huo, uweze kuwa ni sehemu ya sala! Mababa wa Kanisa wanasema katika Liturujia ya Sakramenti za Kanisa, utume wa Kristo Yesu na wa Roho Mtakatifu ambao unatangaza, unatekeleza na kushirikisha fumbo la wokovu, unaendelezwa katika moyo unaosali. Sala inazamisha ndani ya Liturujia na kuitumia wakati na baada ya adhimisho lake. Hata pale Liturujia “inapokuwa sirini” sala daima ni sala ya Kanisa, ni ushirika pamoja na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Rej.KKK 2655. Sala ni tukio linalomkutanisha mwamini na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa uelewa huu, waamini wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Ukristo bila Liturujia ni kutomfahamu Kristo Yesu. Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yanawawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu mahali walipo!

Kuna sala nyingi za Kikristo ambazo hazitokani na Liturujia ya Kanisa lakini zinapata “chapa yake” ya Kisakramenti kutoka kwa Kristo Yesu. Mama Kanisa anapoadhimisha Sakramenti mbalimbali za Kanisa, Kristo Yesu yuko kati pamoja na waja wake, ili kuwafariji wale wanaoteseka kwa Mafuta Matakatifu ya Mpako wa wagonjwa au katika Ibada ya Misa Takatifu, Kristo Yesu anapojisadaka kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu wote. Sala ya Mkristo ni kielelezo cha uwepo wa Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Ni tukio linalowawezesha waamini kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapaswa kuadhimishwa kwa ari, moyo, ibada na uchaji wa Mungu kwani inawashirikisha waamini wote waliomo kwenye ibada hii, Kristo Yesu, akiwa ni kiini cha maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Waamini katika tofauti zao msingi zinazodhihirishwa kwa: karama na utume, lakini wote wanaunganishwa na Kristo Yesu, Mhusika mkuu wa Liturujia ya Kanisa.

Wakristo wa Kanisa la Mwanzo, walianza kuadhimisha Liturujia ya Kanisa kwa kunafsisha maneno na matendo ya Kristo Yesu katika mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu na hivyo kuwakirimia kuwa ni sadaka safi ya kiroho inayotolewa kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Paulo, Mtume anapowaandikia Warumi anawasihi kwa huruma zake Mungu kuitoa miili yao iwe ni dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu ndiyo ibada yao yenye maana. Rej. Rum. 12: 1. Baba Mtakatifu amehitimisha Katekesi yake kuhusu kusali katika Liturujia kwa kutoa wito kwa Wakristo wote kuhakikisha kwamba maisha yao yanakuwa ni kielelezo cha Ibada kwa Mwenyezi Mungu, kwa kushiriki vyema katika sala. Wanaposhiriki Ibada ya Misa Takatifu, wanajumuika na waamini wenzao na hivyo wanasali pamoja na Kristo Yesu ambaye yuko kati pamoja nao!

Papa Liturujia
03 February 2021, 16:14