Tafuta

Vatican News
Papa Francisko katika ujumbe wake kwa wajumbe wa mkutano wa V wa Kimataifa wa Watu Asilia anakazia umuhimu wa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kukabiliana na baa la njaa duniani. Papa Francisko katika ujumbe wake kwa wajumbe wa mkutano wa V wa Kimataifa wa Watu Asilia anakazia umuhimu wa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kukabiliana na baa la njaa duniani.  (ANSA)

Papa: IFAD: Mapambano ya Baa la Njaa Duniani, UVIKO-19: Umoja!

Utandawazi hauna budi kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujikuta ikiteleza na kutumbukia katika mifumo mipya ya ukoloni. Tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu ni amana na utajiri mkubwa unaopaswa kutumiwa ili kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kimataifa ili kupambana na changamoto mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD, kuanzia tarehe 1Februari hadi tarehe 15 Februari 2021 unaendesha mkutano wa V wa Kimataifa wa Watu Asilia kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Thamani ya mfumo wa chakula cha watu mahalia: Ustahimivu katika Muktadha wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19). Washiriki wa mkutano huu wamekuwa wakichambua mada mbalimbali kuhusu: Mwenendo na maendeleo ya wadau wa IFAD kwa watu mahalia; mchakato wa uwezeshaji wa watu mahalia katika ngazi mbalimbali. Wajumbe pia wamejadili na kupembua thamani ya mfumo wa chakula cha watu mahalia: ustahimivu katika muktadha wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mwishoni mwa mkutano huu, wajumbe watatakiwa kupitisha maazimio na hatimaye, kutoa tuzo kwa washindi wa Tuzo ya IFAD kwa Mwaka 2021. Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa IFAD pamoja na wawakilishi, watahitimisha tukio hili kwa kukutana katika mkutano wao wa faragha hapo tarehe 15 Februari 2021.

Monsinyo Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye: Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD, pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP., amesoma ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano huu unaowajumuisha viongozi 154 kutoka katika nchi 57. Ni mkutano unaofanyika kwa kutumia vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.   Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu anakazia kuhusu dhamana na mchango wa Kanisa katika kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kimataifa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kuikumba Jumuiya ya Kimataifa. Utandawazi hauna budi kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kujikuta ikiteleza na kutumbukia katika mifumo mipya ya ukoloni.

Changamoto katika ulimwengu mamboleo zinaweza kushughulikiwa kikamilifu kwa kujikita katika mchakato wa umoja na mshikamano wa Kimataifa. Tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu ni amana na utajiri mkubwa unaopaswa kutumiwa ili kujenga umoja na mshikamano wa Kimataifa. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajielekeza zaidi katika maendeleo fungamani ya binadamu yanayofumbata kimsingi utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; utamaduni wa kusikilizana, kujifunza na kuheshimiana. Hiki ni kiini cha ekolojia fungamani inayotoa uwezo kwa haki jamii kuwa ni nguzo na mlinzi wa sayari dunia. Ni katika muktadha huu wa hali ya unyenyekevu, ndipo Jumuiya ya Kimataifa inaweza kushinda baa la njaa duniani, kwa kujikita katika tunu dumifu zinazofumbatwa katika haki na wema na wala si katika masuala ya mpito!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano huu, utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani upendo ambao watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia wanataka kuujenga na kuudumisha kwa pamoja. Hii ni changamoto inayowataka kusimama kidete ili kulinda na hatimaye, kukirithisha kizazi kijacho ulimwengu ulio bora zaidi na amana na wala si shimo la takataka. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mchakato utakaowawezesha watu wa Mungu kurithisha upendo na ukarimu kwa jirani, badala ya ukame wa maisha ya kiroho, kwa kujitafuta wenyewe au kwa kuelemewa na uchoyo pamoja na ubinafsi! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano wa V wa Kimataifa wa Watu Asilia ambao unanogeshwa na kauli mbiu “Thamani ya mfumo wa chakula cha watu mahalia: Ustahimivu katika Muktadha wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19) kwa kuwapatia baraka zake za kitume, ili Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD uendelee kutekeleza dhamana yake kwa kuwasaidia watu wanaopekenywa zaidi na umaskini pamoja na baa la njaa duniani, ili hata wao waweze kufurahia na hatimaye, kushiriki wema na uzuri unaomiminwa kutoka katika mazingira bora na mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Papa Ifad
06 February 2021, 07:50