Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 4 Februari 2021 kwa mara ya kwanza inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu!

Tukio hili kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa linaadhimishwa tarehe 4 Februari 2021 kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, kuanzia saa 8:30 Mchana kwa saa za Ulaya. Tukio hili linatarajiwa kurushwa mubashara na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Lengo ni kunogesha majadiliano ya kidini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo ya Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa udugu na urafiki kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu inakazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Ujenzi wa utamaduni wa majadiliano ya kidini; umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kufahamiana, ili kushirikiana na kushikamana, kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao msingi. Udugu wa kibinadamu ni sehemu ya utu wa mwanadamu unaowasukuma kusumbukiana katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 3 Februari 2021 amerejea tena kuzungumzia umuhimu wa ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu kwa kutoa wito na mwaliko kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kuiadhimisha, ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni. Tukio hili kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa linaadhimishwa tarehe 4 Februari 2021 kwa kuwashirikisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, kuanzia majira ya saa 8:30 Mchana kwa saa za Ulaya. Tukio hili linatarajiwa kurushwa mubashara na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Washiriki wakuu ni pamoja na: Baba Mtakatifu Francisko, Dr. Ahmad Al-Tayyib, Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni mchango mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana ili kujenga na kudumisha udugu na urafiki wa kijamii.

Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini mchango wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbalimbali duniani, kama sehemu ya mchakato wa kufahamiana sanjari na kutambua tunu msingi za maisha ya kiroho wanazoweza kushirikisha kwa familia nzima ya binadamu. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini, kila kukicha! Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 21 Desemba 2020 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha Azimio Kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Lengo ni kudumisha majadililiano ya kidini na kitamaduni; umoja, mshikamano na ushirikiano wa Kimataifa, ili kujielekeza zaidi katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maridhiano, mshikamano wa kidugu na upatanisho wa Kitaifa na Kimataifa. Mambo makuu yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni: Udugu wa kibinadamu, Mshikamano na Amani. Yote haya yanapania “kufyekelea” mbali “ndago” za uchoyo na ubinafsi, ili kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Siku hii inawakumbusha watu wote wa Mungu kwamba, ni ndugu wamoja licha ya tofauti zao msingi.

Papa Udugu wa Kibinadamu
03 February 2021, 16:30