Tafuta

Tarehe 19 Februari 2021 Italia imewakumbuka na kuwaombea Madaktari, Wauguzi na Wafanyakazi katika sekta ya afya waliopoteza maisha yao wakati wakiwa kazini, kwa jili ya kuwahudumia wagonjwa! Tarehe 19 Februari 2021 Italia imewakumbuka na kuwaombea Madaktari, Wauguzi na Wafanyakazi katika sekta ya afya waliopoteza maisha yao wakati wakiwa kazini, kwa jili ya kuwahudumia wagonjwa! 

Kumbukumbu ya Madaktari na Wauguzi Waliofariki kwa KORONA

Papa Francisko anawapongeza na kuwatia shime madaktari, wauguzi pamoja na wafanyakazi wote wa sekta ya afya kwani wamekuwa ni kielelezo cha “chanjo” dhidi ya ubinafsi, uchoyo na tabia ya watu kutaka kujitafuta wenyewe. Upendo kwa Mungu na jirani iwe ni kiu inayobubujika kutoka katika nyoyo za watu wengi zaidi, ili kujisadaka zaidi kwa ari na moyo mkuu, hasa kwa maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ya watu wa Mungu nchini Italia ni kati ya watu walioguswa na kutikiswa na maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hadi kufikia Jumamosi asubuhi, tarehe 20 Februari 2021, takwimu za Serikali ya Italia zinaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni 2.78 wameambukizwa; wagonjwa milioni 2.3 wamebahatika kupona na watu zaidi ya 95, 235 wamefariki dunia kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maeneo yaliyoathirika sana ni Milano, Bergamo, Brescia, Cremona na Lodi. Kimsingi hili ni eleo la Mkoa wa Lombardia, ulioko Kaskazini mwa Italia. Katika mapambano dhidi ya Virusi vya Korona, Hospitali ya “Spallanzani” iliyoko mjini Roma, ambayo ni maarufu kwa kutibu magonjwa ya Ukanda wa Joto, imekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna madaktari 324 pamoja na wauguzi 81 waliofariki dunia kutokana na Virusi vya Korona, UVIKO-19. Itakumbukwa kwamba, kuna zaidi ya wauguzi 100, 000 ambao wameambukizwa gonjwa hili, wakiwa wanawahudumia waathirika wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 nchini Italia peke yake!

Ni katika hali na mazingira kama haya, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Jumamosi tarehe 20 Februari 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Madaktari na wauguzi waliofariki dunia wakati wanatoa huduma kwa wagonjwa na waathirika wa janga Virusi vya Korona, UVIKO-19, kielelezo cha hali ya juu cha Injili ya huduma na upendo kwa wagonjwa na hasa wale wanaohitaji msaada zaidi. Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na athari za janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, katika maadhimisho haya, amemwandikia barua Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, akimshukuru Mungu kwa moyo wa ukarimu, upendo na ushupavu mkubwa, waliouonesha madaktari wakati wa kuwahudumia wagonjwa kwa weledi, taaluma na ufanisi kadiri ya uwezo wao.

Hawa ni watu waliojisadaka bila ya kujibakiza kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao na hata wengine kukumbana na uso kwa uso na fumbo la kifo; hao ambao wanakumbukwa kwa Ibada ya Misa takatifu. Katika shida, mateso na mahangaiko ya watu, jamii inahamasishwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia upendo kwa jirani, kwa kujitaabisha kuwahudumia wengine na hasa zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anaendelea kuwapongeza na kuwatia shime madaktari, wauguzi pamoja na wafanyakazi wote wa sekta ya afya wanaotoa huduma kwamba, kweli wamekuwa ni kielelezo cha “chanjo” dhidi ya ubinafsi, uchoyo na tabia ya watu kutaka kujitafuta wenyewe. Upendo kwa Mungu na jirani iwe ni kiu inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo za watu wengi zaidi, ili kujisadaka kwa ajili ya maskini pamoja na kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu. Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala, wale wote waliokuwa wanashiriki katika tukio hili muhimu katika mapambano dhidi ya athari za janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Papa Korona
22 February 2021, 15:20