Tafuta

Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Februari 2021: Kwa ajili ya wanawake wanaodhulumiwa na kunyanyaswa kijinsia! Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio chao kwa kujenga jamii inayosimikwa katika haki. Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Februari 2021: Kwa ajili ya wanawake wanaodhulumiwa na kunyanyaswa kijinsia! Ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio chao kwa kujenga jamii inayosimikwa katika haki. 

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Februari 2021: Nyanyaso!

Inasikitisha sana kuona wanawake na wasichana wakitendewa unyama na ukatili kama huu. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Februari 2021 kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anakita ujumbe wake dhidi ya ukatili wanaofanyiwa wanawake. Huu ni unyanyasaji wa binadamu katika ujumla wake! Usitishwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican. 

Kumekuwepo na vitendo vya: Kinyama, ukatili, vipigo, ubakaji, matusi na kunyimwa fursa za kiuchumi mambo ambayo yamewaathiri sana wanawake wengi duniani: kiuchumi, kiafya, kisaikolojia na kijamii. Inasikitisha sana kuona wanawake na wasichana wakitendewa unyama na ukatili kama huu. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Februari 2021 kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anapenda kukita ujumbe wake dhidi ya ukatili wanaofanyiwa wanawake. Kutokana na woga hali na kutojiamini, wanawake wengi wamekujikuta wakinyanyasika na kudhulumiwa, huku utu, heshima na haki zao msingi zikiendelea kusiginwa. Huu ni unyanyasaji wa binadamu katika ujumla wao. Katika hali na mazingira kama haya, kuna wanawake mashuhuda ambao kwa ujasiri mkubwa wameamua kuvunjilia mbali ukimya huu na kuanza kupaaza kilio cha sauti zao ili waweze kusikilizwa na hatimaye, hatua muhimu kuweza kuchukuliwa. Umefika wakati wa kushughulikia kilio cha wanawake dhidi ya nyanyaso za kijinsia na kamwe wasipewe kisogo anasema Baba Mtakatifu.

Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea wanawake ambao wameathirika kutoka na nyanyaso na ukatili wa kijinsia, ili sasa, jamii iweze kuamka na kujizatiti zaidi katika kusikiliza na kujibu kilio cha nyanyaso na ukatili wa kijinsia, ili hatimaye, kuweza kuwaokoa na kuwalinda! Wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya nyanyaso na ukatili wa kijinsia, kwani waswahili wanasema, “mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe! Takwimu zinaonesha kwamba, duniani kote ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ikiwemo ubakaji unaongezeka maradufu na wengine wanathubutu kusema kwamba haya ni matokeo pia ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Takwimu za Kitengo cha Wanawake cha Umoja wa Mataifa kwa Mwezi Novemba 2020 zinaonesha kwamba, takribani wanawake 137 wanauwawa kikatili kila sika na watu kutoka ndani ya familia zao.

Kumekuwepo na wimbi kubwa la biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na nyanyaso za kingono. Kwa sehemu kubwa, mambo yote haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na itifaki ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa kuwataka watu kukaa karantini, kutotembea ovyo pamoja na madhara ya kuporomoka kwa uchumi, ulinzi na usalama. Kuna Mkataba wa Kimataifa wa kupinga aina yoyote ya Ubaguzi dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979: (Convention on the Elimination of all Forms of Discrimination against Women of 1979). Pili kuna Mkataba wa Nyongeza wa Afrika wa Haki za Wanawake wa Mwaka 1981 (Option Protocol to the African Charter on the Rights of Women in Africa or Maputo Protocol of 1981). Mikataba yote miwili inaelezea umuhimu wa kulinda haki za wanawake na pia kusimamia mchakato wa kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana! Nchi 155 zimeridhia Mkataba wa Kimataifa wa kupinga aina yoyote ya Ubaguzi dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979.

Licha ya sheria na itifaki zote hizi, lakini bado kuna nyanyaso na ukatili wa kijinsia sehemu mbali mbali za dunia unaendelea kushika kasi ya ajabu. Kutokuwepo kwa sheria zinazoainisha ukatili kwa wanawake majumbani ni kikwazo katika kupambana na unyanyasaji na ukatili kwa wanawake. Kuna Nchi 125 pekee ulimwenguni ambazo sheria zake zinaweka bayana kwamba, ukatili wa majumbani ni kosa la jinai huku nchi nyingine nyingi sheria zake haziainishi ukatili wa majumbani kama kosa la jinai jambo linalochangia ukatili huo kwa wanawake kuendelea kuwaathiri wanawake na wasichana. Ukatili huu unadumaza familia na ni kikwazo cha maendeleo fungamani ya binadamu.

Kwa upande wake, Padre Frédéric Fornos S.J., Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakaza kusema, umefika wakati wa kuivalia njuga changamoto hii bila kupepesapepesa macho dhidi ya nyanyaso na ukatili wa kijinsia. Haya ni mambo ambayo yameota mizizi yake katika tamaduni na jamii za watu wengi duniani. Katika Injili ya Yohane 8: 2-11 Waandishi na Mafarisayo walimhukumu adhabu ya kifo yule mwanamke aliyekamatwa “mubashara” akizini. Wakataka kibali kutoka kwa Kristo Yesu, lakini hakumhukumu, akamsamehe dhambi zake na kumpatia tena nafasi ya kuandika ukurasa mpya wa matumaini katika maisha yake. Aina na mifumo yote ya nyanyaso na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana haikubaliki hata kidogo na kwamba, kilio cha wanawake kinafika hadi mbinguni! Ukatili huu ni kashfa dhidi ya Kristo Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria Maria. Mwanadamu amepata wokovu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Huu ni wakati kwa waamini wote kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wanawake na wasichana wote ambao ni wahanga wa nyanyaso na ukatili wa kijinsia, ili wote kwa pamoja waweze kusimama kidete katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, ili iweze kuwalinda, kuwasikiliza na kuwaokoa kutoka katika shida na mahangaiko yao!

Unyanyasaji wa kijinsia ni aina ya ukatili unaochukiza sana, na unajumlisha kubaka na aina yoyote ya mashambulizi yanayohusu ngono ambayo hufanywa dhidi ya wanawake, wasichana, wanaume na wavulana. Matokeo yake yanaweza kuwa ya kikatili na huweza kuwa na madhara ya kimwili na kisaikolojia kwa walionusurika na mashuhuhuda pia huyumbisha mno jumuiya na raia kwa ujumla. Ni muhimu kutambua kwamba wanawake, wanaume, wasichana na wavulana wote wanaweza kuwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia. Hata hivyo, kihistoria na kimuundo, kutokuwepo kwa usawa kati ya wanaume na wanawake na mifumo mbalimbali ya ubaguzi wa jinsia, ambapo wanawake dunia nzima wamekuwa wakionewa, kumechangia kufanya wanawake na wasichana kuathirika zaidi na unyanyasaji wa kijinsia katika mazingira yenye mfarakano. Kumbe, kuna haja ya kuimarisha vyombo vya haki ili kuweza kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake! Pengine umefika wakati wa kuwa na sheria maalumu kuhusu ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani. Wanawake wanapaswa kuacha tabia ya kuvumilia ukatili wanaofanyiwa na wenza wao. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema, kuna wanaume pia wanaofanyiwa ukatili wa majumbani, lakini wameamua kunyamaza na “kufa na tai shingoni” kwani ni fedheha sana kusimulia kipigo kutoka kwa mwanamke.

Papa: Nia Februari 2021
24 February 2021, 14:59