Tafuta

Vatican News
Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene Inanogeshwa na kauli mbiu: Udugu na Majadiliano: Dhamana ya Upendo. Kristo Ndiye amani Yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja. Rej. Efe. 2:14. Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene Inanogeshwa na kauli mbiu: Udugu na Majadiliano: Dhamana ya Upendo. Kristo Ndiye amani Yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja. Rej. Efe. 2:14.  (AFP or licensors)

Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene Nchini Brazil 2021!

Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene, 2021 inanogeshwa na kauli mbiu: Udugu na Majadiliano: Dhamana ya upendo. Kristo ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja” Rej. Efe: 2:14. Lengo la maadhimisho haya ni ushuhuda wa kiekumene yaani umoja katika tofauti, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, Siku 40 za toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika: sala, kufunga na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko kwa ufupi kabisa anasema kwamba, Kwaresima ni safari inayofumbata maisha ya mtu mzima kiroho na kimwili. Ni mchakato wa kutoka katika utumwa kuelekea katika uhuru wa kweli, unaomwelekeza mwamini kwa Baba yake wa mbinguni asili ya huruma na chemchemi ya mapendo. Ni safari ya kumrudia tena Kristo Yesu ili kumshukuru kwa zawadi ya wokovu. Hii pia ni safari ya kumrudia Roho Mtakatifu, ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, tayari kuonja ile furaha ya kupendwa! Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB kwa kushirikiana kwa dhati kabisa na Baraza la Makanisa Nchini Brazil, CONIC, Jumatano ya Majivu, tarehe 17 Februari 2021 wamezindua Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene Katika Kipindi cha Kwaresima 2021, CFE. Hii ni Kampeni ambayo huadhimishwa kiekumene kila baada ya miaka mitano, kwa kutambua amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Makanisa ya Kikristo nchini Brazil. Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene, 2021 inanogeshwa na kauli mbiu: Udugu na Majadiliano: Dhamana ya upendo. Kristo ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja” Rej. Efe: 2:14.

Lengo la maadhimisho haya ni ushuhuda wa kiekumene yaani umoja katika tofauti, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Uzinduzi wa maadhimisho haya umefanyika kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, kwa kuonesha pia umuhimu wa Makanisa katika mchakato wa mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watu wa Mungu nchini Brazil, kila mwaka wakati wa Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, sadaka yote inayokusanywa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 230 ya mshikamano miongoni mwa watu wa Mungu nchini Brazil. Kutokana na janga laVirusi vya Korona, UVIKO-19, mwaka 2020, Kampeni hii haikufanyika. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene Katika Kipindi cha Kwaresima 2021, anagusia umuhimu wa mshikamano wa upendo ili kupambana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Matendo ya huruma: kiroho na kimwili yawe ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayomwilishwa katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanafanya tafakari ya kina kuhusu maisha yao, tayari kutembea na Kristo Yesu jangwani, ili hatimaye, kushuhudia ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kristo Yesu anaendelea kufanya hija na waja wake hata katika kipindi hiki cha janga laVirusi vya Korona, UVIKO-19. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni muda muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa ajili ya madaktari na wafanyakazi wote katika sekta ya afya, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kama alivyofanya yule Msamaria mwema alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai! Rej. Lk. 10:25-37.

Huu ni mwaliko wa kushinda janga hili kwa njia ya mshikamano upendo, kwa kusimama kidete kulinda na kutangaza Injili ya uhai dhidi ya Utamaduni wa kifo. Ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi na uchoyo uliokithiri bila kusahau ulaji wa kupindukia pamoja na kujihami kusikokuwa na mvuto wala mashiko. Ili kuepukana na hayo yote yasitendeke katika maisha yao, kipindi cha Kwaresima ni msaada mkubwa unaowapatia changamoto ya kumwilisha toba, wongofu wa ndani, sala na matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha yao. Baba Mtakatifu anawapongeza watu wa Mungu nchini Brazil kwa kuendesha Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene, 2021 inayonogeshwa na kauli mbiu: Udugu na Majadiliano: Dhamana ya upendo. Kristo ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja” Rej. Efe: 2:14. Huu ni wakati wa kukaa pamoja, kujadiliana na kusikilizana ili kuvuka kikwazo cha unafsia, kwa kumkubali na kumpokea mwingine kama jirani mwema. Huu ndio mchakato wa utamaduni wa majadiliano kama anavyohimiza Kristo Yesu kwani Kristo ndiye amani yao, aliyewafanya wote kuwa wamoja. Rej. Efe: 2:14.

Majadiliano ya kiekumene hayana budi kuchukuliwa kama dhamana ya upendo na Wakristo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Watambue kwamba, hapa duniani wao wote ni mahujaji na hivyo wanapaswa kuaminiana kwa kuondoa tabia ya kutiliana shaka au kutokuaminiana na hivyo kujielekeza zaidi katika kile ambacho Wakristo wote wanakitafuta yaani: amani na mng’ao wa ufunuo wa Uso wa Mungu. Rej. EG, n. 244. Kumbe hiki ni kiini cha matumaini katika Kampeni hii ya Kiekumene inayolishirikisha Baraza la Makanisa Nchini Brazil, CONIC. Na katika muktadha huu, wanatekeleza kwa vitendo Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mchakato wa kutambua na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mchango muhimu sana katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na ulinzi wa haki jamii. Ufanisi wa ushuhuda wa kiekumene utategemea uwezo wao katika majadiliano ya kiekumene, kwa kutafuta mambo msingi yanayowaunganisha na hatimaye kuyamwilisha katika matendo na hasa zaidi kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anawatakia wote mafanikio mema katika Kampeni ya Tano ya Udugu wa Kiekumene Katika Kipindi cha Kwaresima 2021, CFE.

Papa Brazil
18 February 2021, 15:16