Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza viongozi wa Kanisa nchini Perù kwa kuanzisha kampeni ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuchangia ununuzi wa vifaa tiba kwa wajili ya wagonjwa na waathirika wa UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza viongozi wa Kanisa nchini Perù kwa kuanzisha kampeni ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuchangia ununuzi wa vifaa tiba kwa wajili ya wagonjwa na waathirika wa UVIKO-19.  (AFP or licensors)

Kampeni ya Mshikamano wa Ununuzi wa Vifaa Tiba Nchini Perù!

Papa anawaomba viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu katika mahangaiko yao wanaonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa ni kifani. Mshikamano wa huruma na mapendo, usaidie kujenga na kudumisha: upendo na udugu wa kibinadamu. Katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korana, UVIKO-19 asiwepo hata mtu mmoja anayebakizwa nyuma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Mama Kanisa anawahamasisha waamini kutumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali, kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu anayewatakasa na kuwafariji waja wake. Tafakari ya Neno la Mungu, inalenga kuendelea kusoma alama za nyakati kwa mwanga wa Injili ya imani na matumaini. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo cha Injili ya huruma na upendo kwa Mungu. Ibada ya Rozari Takatifu, inapania kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja kwa Mwenyezi Mungu anayeokoa kwa kutambua kwamba, sala ni chemchemi ya matumaini.

Katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, watu wa Mungu wanapaswa kuendelea kufuata ushauri wa wataalam wa afya pamoja na kutekeleza itifaki dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili mafanikio yaliyokwisha kupatikana yaweze kuendelezwa zaidi badala ya kutumbukia tena kwenye taharuki na hofu ya maambukizi mapya ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kimsingi vita dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni tete sana. Kumbe, silaha za kisayansi, maisha ya kiroho, kijamii na kiuchumi hazina budi kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amefurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Jimbo kuu la Trujillo, nchini Perù la kampeni ya kuchanga fedha kwa ajili ya kununulia vifaa tiba kwa ajili ya wagonjwa pamoja na familia zao, wanaoshambuliwa na Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kutumwa kwenda kwa Askofu mkuu Miguel Cabrejos, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Perù. Kampeni hii inanogeshwa na kauli mbiu “Perù Pumua”. Baba Mtakatifu anawaomba viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao wanaonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa ni kifani. Mshikamano wa huruma na mapendo, usaidie kujenga na kudumisha: umoja, upendo na udugu wa kibinadamu. Katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korana, UVIKO-19 asiwepo hata mtu mmoja anayebakizwa nyuma au kutelekezwa!

Papa: Uviko 19

 

 

 

 

 

 

19 February 2021, 14:36