Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko: Jumatano ya Majivu: Kwaresima ni safari ya maisha ya kiroho kuelekea katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko: Jumatano ya Majivu: Kwaresima ni safari ya maisha ya kiroho kuelekea katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.  (Vatican Media)

Jumatano ya Majivu: Kwaresima Ni Safari ya Kuelekea Kwa Mungu

Papa Francisko: Kwaresima ni safari inayofumbata maisha ya mtu mzima. Ni mchakato wa kutoka katika utumwa kuelekea katika uhuru wa kweli, unaomwelekeza mwamini kwa Baba yake wa mbinguni. Ni safari ya kumrudia tena Kristo Yesu ili kumshukuru kwa zawadi ya wokovu. Ni safari ya kumrudia Roho Mtakatifu, ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, ili kuonja furaha ya kupendwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, yaani Siku 40 za kufunga, kusali na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kuhakikisha kwamba, wananafsisha imani, matumaini na mapendo katika uhalisia wa maisha yao. Lakini zaidi wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambalo kwa sasa ni tishio kwa usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unaonogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu tarehe 17 Februari 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kubariki majivu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu amepakwa majivu na Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baadaye, Baba Mtakatifu amewapaka majivu Makardinali waliohudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amesema kwamba, Kwaresima ni safari inayofumbata maisha ya mtu mzima. Ni mchakato wa kutoka katika utumwa kuelekea katika uhuru wa kweli, unaomwelekeza mwamini kwa Baba yake wa mbinguni. Ni safari ya kumrudia tena Kristo Yesu ili kumshukuru kwa zawadi ya wokovu. Ni safari ya kumrudia Roho Mtakatifu, ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, ili kuonja furaha ya kupendwa! Baba Mtakatifu anasema kwamba, Nabii Yoeli ametoa dira na mwelekeo sahihi wa kufuata katika Kipindi hiki cha Kwaresima. Hii ni fursa ya kumrudia Mwenyezi Mungu kwa mioyo yao yote, kwa kufunga, kwa kulia, na kuomboleza; kwa kurarua mioyo yao na wala si mavazi, ili kumrudia Mungu. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa neema na rehema, amejaa huruma na mapendo. Rej. Yoe. 2: 12-18. Kwaresima ni safari ya kurejea kwa Mwenyezi Mungu, kwa njia ya sala na wala hakuna tena muda wa kuahilisha, kwa sababu ni Mwenyezi Mungu mwenyewe anayetoa wito wa toba na wongofu wa ndani. Kwa hakika katika maisha, hakuta kosekana vizingizio. Kwaresima ni safari inayofumbata maisha ya mtu mzima, kwa kutathmini njia, ili kupata uhakika wa kuweza kufika nyumbani kwa Baba, ili kugundua mafungamano msingi yaliyopo kati ya Mungu na waja wake, msingi wa maisha yote ya mwanadamu.

Ni fursa ya kujiondoa katika ubinafsi na uchoyo, ili kumwabudu na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Ili kuweza kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na moyo thabiti. Ni wakati wa kuondokana na unafiki, kwa kupambana vyema na maisha ya undumila kuwili. Kwaresima ni safari ya kutoka utumwani, kuelekea katika uhuru kamili. Ni kipindi cha Siku Arobaini kinachowakumbusha waamini, miaka 40 ambayo Waisraeli walitembea jangwani, wakaona wema, huruma na msamaha wa Mungu. Wakiwa jangwani waliendelea kukumbuka “mafuria ya nyama na makapu vya vitunguu swaumu”; kiasi cha kutamani kurejea tena utumwani Misri! Walikumbuka historia yao ya zamani na baadhi ya miungu waliyokuwa wanaiabudu. Si rahisi sana kutoka Misri. Hivi ndivyo inavyotokea hata kwa waamini wanapofunga safari kumrudia tena Mungu. Kikwazo kikuu ni kujishikamanisha mno na vitu; kwa kuendelea kuteleza na hatimaye kutumbukia katika mizizi na vilema vya dhambi. Mababa wa Kanisa wanavitaja vilema saba vya dhambi kuwa ni: majivuno, uroho, uzinifu, hasira, ulafi, kijicho na uzembe.

Kuna baadhi ya watu wanatabia ya kujiamini kipumbavu, kwa kujihakikishia usalama kutokana na utajiri wa fedha na mali. Kuna watu ambao litania ya malalamiko kimekuwa ni chakula chao cha kila siku. Ili kuanza safari na kutembea, mambo yote haya yanapaswa kuwekwa hadharani.Baba Mtakatifu anakaza kusema, safari ya kumrudia tena Mwenyezi Mungu inasindikizwa na Neno la Mungu. Kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, hata waamini katika hija ya maisha yao, wamesahau manukato ya nyumbani mwao, wakajikuta wakiwa na mikono tupu na moyo unaohuzunika. Ni watu ambao “wamekomba” rasilimali kwa anasa na starehe. Wamekuwa ni watu wa kuchechemea, kujikwaa na kuanguka mara kwa mara, na sasa wanahitaji msaada wa Baba ya mbinguni ili kuwashika mkono na kuwanyanyua, kwa huruma ya Mungu. Ni mwaliko kwa waamini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu yaani Sakramenti ya Upatanisho ni hatua ya kwanza kabisa kumwendea Mwenyezi Mungu. Mapadri waungamishaji, wawe ni wamisionari wa huruma na upendo wa Mungu kwa wadhambi!

Hii ni safari ya kumrudia tena Kristo Yesu, kama ilivyokuwa kwa wale wakoma kumi waliotakaswa na Kristo Yesu, lakini ni Msamaria mmoja tu alipoona kwamba, amepona alirudi huku akimtukuza na kumshukuru Mungu. Waamini wote kila mtu anayo magonjwa yake ya maisha ya kiroho anasema Baba Mtakatifu Francisko. Haya ni magonjwa yanayomhitaji “daktari bingwa” ili kuyaganga na kuyaponya. Watu wengi wanao woga unaowapiga ganzi, kiasi cha kushindwa kutembea. Waamini wanapaswa kuwa na ujasiri kama wa yule Mkoma aliyevunjilia mbali “viunzi” na kujikuta akikabiliana mubashara na Kristo Yesu, akampigia magoti, akiomba na kumwambia: ukitaka unaweza kunitakasa!  Kwa hakika waamini wanahitaji uponyaji unaotoka kwa Kristo Yesu. Lakini, kuna haja kwanza kabisa kwa waamini wenyewe kuweka mbele ya Kristo Yesu madonda na mapungufu yao ya kibinadamu, ili Kristo Yesu, aweze kuwaganga, kuwaponya na kuwaokoa. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwaponya kutoka katika undani wa nyoyo zao! Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini tena watarudi.

Kumbe, Kwaresima ni Kipindi cha kumrudia tena Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia maisha ili hatimaye, kuambata mambo yanayodumu. Ni muda wa kumrudia Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima. Ni moto unaowawezesha waamini kutoka mavumbini. Ni wakati wa kumrudia na kusali kwa ajili ya Roho Mtakatifu, ili kuwasha tena moto wa sifa unaoteketeza majivu ya “litania ya malalamiko pamoja na hali ya kujikatia tamaa ya maisha”.Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ameshuka kutoka mbinguni, ili kuja kukutana na waja wake. Akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mtakatifu Paulo, Mtume anawakumbusha waamini kwamba, wao ni vyombo na wahudumu wa Upatanisho. Huu ni wakati wa kupatanishwa na Mungu. “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye”. 2Kor. 5: 21. Kumbe, Kristo Yesu ni mwandami wa safari ya upatanisho. Kristo Yesu ameshuka kutoka mbinguni ili kuwaganga na kuwatibu waja wake. Huyu ndiye Kristo Yesu aliyechomwa mkuki ubavuni; Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuzama katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani na hivyo kuwa watu wapya zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni wakati wa kujipatanisha na Mwenyezi Mungu. Wongofu wa moyo, matendo na utekelezaji wake yanawezekana ikiwa kama mwamini atampatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha yake. Wokovu ni zawadi ya bure inayotolewa na Mwenyezi Mungu. Kumbe, waamini wawe wepesi kupokea neema na baraka ya kuweza kumrudia Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwapatia haki itakayowawezesha kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kudumu na Mwenyezi Mungu. Waamini wanapaswa kujiaminisha kwa Mungu kwa kutambua kwamba wanahitaji huruma na msaada wake wa daima. Hii ndiyo njia ya haki, njia ya unyenyekevu! Waamini wameinamisha vichwa vyao ili kupakwa majivu na baada ya Kipindi cha Kwaresima, watainama na kupiga magoti ili kuwaosha miguu jirani zao kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja takatifu; akaonesha huduma ya upendo kwa kuwaosha mitume wake miguu. Wokovu ni kielelezo cha unyenyekevu unaofumbatwa katika upendo.

Waamini wajifunze kutoka katika Mti wa Msalaba, ili waweze kujufunza ukimya wa Mungu. Iwe ni fursa ya kuangalia na kuyatafakari Madonda yake Matakatifu, ili kugundua utupu walio nao ndani mwao; dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Ni mahali pa kugundua madonda ya dhambi na matukio ambayo yamewaachia uchungu moyoni. Hata katika muktadha huu, bado Mwenyezi Mungu amefungua mikono yake ili kuwapokea wale wote wanaomwendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.” 1 Pet. 2: 24. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwasubiri waja wake ili kwa njia ya Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, aweze kuwakirimia wema, huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Kristo Yesu amewajia waja wake ili kuwainua kutoka katika udhaifu wao, ili waweze kuonja furaha ya kupendwa zaidi.

Papa Majivu

 

17 February 2021, 14:14