Tafuta

Vatican News
Jumatano ya Majivu: Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima. Hiki ni kipindi cha kupanda kwenda Mlimani Kalvari pamoja na Kristo Yesu ili kupyaisha: imani, matumaini na mapendo Jumatano ya Majivu: Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima. Hiki ni kipindi cha kupanda kwenda Mlimani Kalvari pamoja na Kristo Yesu ili kupyaisha: imani, matumaini na mapendo 

Jumatano ya Majivu: Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima: Fadhila!

Jumatano ya Majivu, mwanzo wa Siku 40 za kufunga, kusali na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kuhakikisha kwamba, wananafsisha imani, matumaini na mapendo katika maisha yao. Lakini zaidi wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, hatari kwa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 14 Februari 2021 amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 17 Februari 2021 ni Jumatano ya Majivu, mwanzo wa Siku 40 za kufunga, kusali na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kuhakikisha kwamba, wananafsisha imani, matumaini na mapendo katika uhalisia wa maisha yao. Lakini zaidi wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kupambana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambalo kwa sasa ni tishio kwa usalama, ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Jumatano ya Majivu, kuanzia Saa 3:30 asubuhi kwa saa za Ulaya, anatarajia kuongoza Ibada ya Misa Takatifu ambapo atabariki majivu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii itahudhuriwa na watu wachache kama sehemu ya utekelezaji wa Protokali ya kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kutokana na uwepo wa Ibada hii ya Misa Takatifu, hakutakuwepo na Katekesi inayotolewa kila Jumatano na Baba Mtakatifu. Katika Kipindi cha Kwaresima, kila Ijumaa, kutakuwepo na Tafakari za Kipindi cha Kwaresima. Kauli mbiu inayoongoza tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2021 zinazotolewa kwa Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Roma” pamoja na wafanyakazi wa Jimbo kuu la Roma ni “Akawaambia, “Nanyi mwaninena kuwa mimi kuwa ni nani? Tafakari hizi zitatolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa.

Jumatano ya Majivu

 

15 February 2021, 16:04