Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 8 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya KImataifa mjini Vatican. Amefafanua kuhusu Diplomasia ya Vatican kwenye Jumuiya ya Kimataifa Papa Francisko tarehe 8 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya KImataifa mjini Vatican. Amefafanua kuhusu Diplomasia ya Vatican kwenye Jumuiya ya Kimataifa  (ANSA)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Wanadiplomasia wa Vatican 2021!

Hija za kitume ni muhimu katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, mikataba na itifaki za kimataifa ni nyenzo muhimu katika kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na mgogoro wa kiafya, uharibifu wa mazingira, myumbo wa uchumi na kijamii: kitaifa na Kimataifa. Mwaka 2020 utakumbukwa na wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni dhamana na wajibu wa mtu binafsi, jamii na taifa katika ujumla wake. Hija za kitume ni muhimu katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, mikataba na itifaki za kimataifa ni nyenzo muhimu katika kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwaka 2020 utakumbukwa na wengi kutokana na madhara yake katika historia ya maisha ya mwanadamu. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na mgogoro wa kiafya, uharibifu wa mazingira, myumbo wa uchumi na kijamii: kitaifa na Kimataifa. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa IOM mwaka 2021 linaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Kuna mgogoro mkubwa wa kisiasa kitaifa na Kimataifa kutokana na baadhi ya wanasiasa kusigina demokrasia na tunu msingi za maisha ya kisiasa! Inasikitisha kuona kwamba, biashara haramu ya silaha duniani inaendelea kushamiri kila kukicha, kiasi cha kutishia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, vitendo vya kigaidi vimeongezeka maradufu duniani! Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 limetibua mahusiano na mafungamano ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha na maafa yake yanaonekana katika kusigina: uhuru wa kuabudu na haki ya elimu kwa watoto na vijana wengi.

Kwa muhtasari haya ndiyo mawazo mazito yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 8 Februari 2021, alipokutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa. Anasema, mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni dhamana na wajibu wa mtu binafsi, jamii na taifa katika ujumla wake. Kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija ya kitume nchini Iraq, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hija za kitume ni muhimu sana katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni nyenzo ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi na Serikali mbalimbali duniani. Ni fursa ya kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inapenda kuheshimu Mikataba na Itifaki mbalimbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Mwaka 2020 utakumbukwa na wengi, kutokana na madhara yake katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 limechangia kiasi kikubwa athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula duniani; athari za uchumi pamoja na ongezeko kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Mgogoro wa kiafya, umeanika wazi maisha ya mwanadamu; magonjwa na kifo. Hii ni changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kujizatiti, ili kuwahudumia maskini, kwa heshima, huku utu na haki zao msingi zikiheshimiwa. Hawa ni watu wanaopaswa kupewa huduma bora za afya pamoja na matunzo. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, yameiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuweza kupata chanjo ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 kwa haraka zaidi.

Chanjo itolewe kwa haki na usawa kwa watu wote bila kuangalia sana uwepo wao wa kiuchumi, kipaumbele cha kwanza, wakiwa ni maskini na wazee. Lakini wananchi wanapaswa kuzingatia ushauri unaotolewa na madaktari pamoja na wafanyakazi katika sekta ya afya dhidi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watu wasiweke matumaini yao yote kwenye chanjo na kusahau kutekeleza dhamana na wajibu wao msingi wa kujilinda na kuwalinda wengine dhidi Virusi vya Korona, UVIKO-19. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Mkutano wa 26 wa kimataifa wa mbadiliko ya tabianchi, COP26 utafanyika kuanzia tarehe 1-12 Novemba 2021 huko mjini Glasgow nchini Scotland. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna maafa na majanga makubwa yanayotokana na ukame wa kutisha, mafuriko pamoja na majanga ya moto sehemu mbalimbali za duniani. Matokeo yake ni watu wengi kuanza kunyemelewa na baa la njaa na utapiamlo.

Kuna myumbo wa uchumi na kijamii: kitaifa na Kimataifa hali ambayo imegumishwa kutokana na Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna watu wamekosa fursa za ajira na viwanda vingi kufungwa. Hali hii imepelekea kuibuka kwa kasi kubwa nyanyaso za kijinsia na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa uchumi fungamani unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu, utu, heshima na haki zake. Fursa za ajira; uhakika na usalama wa huduma za afya ni muhimu sana kwa sasa na kwa siku za usoni, vinginevyo watu wengi watatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Michezo ya kamari na upatu ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Mchezo wa kamari na upatu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti katika ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amegusia pia uhalifu wa kimitandao, biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.

Mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka ulioshuhudia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa IOM mwaka 2021 linaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Vatican ambayo pia ni wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR., itaendelea kuwa aminifu kwa Mkataba wa Geneva wa Mwaka 1951 na Protokali ya mwaka 1967 inayotoa maana ya mkimbizi, haki zake msingi na wajibu wa nchi zinazotoa hifadhi. Baba Mtakatifu inasikitishwa sana na wimbi kubwa la wakimbizi pamoja na kiwango kikubwa cha watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbalimbali za dunia, lakini zaidi katika Ukanda wa Sahel.

Kuna mgogoro mkubwa wa kisiasa kitaifa na Kimataifa kutokana na baadhi ya wanasiasa kusigina demokrasia na tunu msingi za maisha ya kisiasa! Machafuko ya kisiasa, kusiginwa kwa demokrasia, uhuru wa kujieleza na hatimaye, mapambano ya silaha ni kati ya mambo yanayoendelea kujitokeza sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika mchakato wa majadiliano shirikishi katika ukweli na uwazi ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Haki na wajibu ni chanda na pete! Amani haina budi kutawala katika akili na nyoyo za watu wa Mungu. Tarehe 22 Januari 2021, Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Matumizi ya Silaha za Nyuklia, TPNW, ambao umeridhiwa na Mataifa zaidi 50 umeanza kutumika rasmi. Huu ni Mkataba wa Kimataifa unaopiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za nyuklia. Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha hizi hayana macho wala pazia, na hayawezi kuchagua wala kubagua! Katika kipindi kifupi tu, matumizi ya silaha hizi yanaweza kusababisha maafa makubwa na yatakayodumu kwa muda mrefu kwa binadamu na mazingira yake. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna silaha nyingi duniani zinazotishia amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Vitendo vya kigaidi vimeendelea kuongezeka zaidi katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amesema kuna mgogoro mkubwa wa mahusiano na mafungamano ya kibinadamu yanayokita mizizi yake katika dhamiri, utu, heshima na haki zake msingi. Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha madhara makubwa katika sekta ya elimu. Kuna baadhi ya wanafunzi wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na UVIKO-19 sanjari na kukosa uwezo na teknolojia ya kuweza kufuatilia masomo wakiwa majumbani mwao. Uhalifu wa kimitandao umeongezeka maradufu kiasi cha kuhatarisha maisha ya wanafunzi wengi. Kumbe, kuna haja ya kupyaisha mfumo wa elimu inayotolewa; kwa kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; uhuru, ukweli, haki na upendo wa dhati. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la nyanyaso na vipigo majumbani kutokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini umesiginwa sana katika kipindi cha Mwaka 2020. Utunzaji bora wa mwili hauna budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa maisha ya kiroho, ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Papa: Mabalozi

 

09 February 2021, 15:02