Tafuta

Vatican katika diplomasia ya Kimataifa inatekelezwa dhamana na wajibu wake kwa kushirikiana na mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Utekelezaji wa Mikataba na Itifaki za Kimataifa. Vatican katika diplomasia ya Kimataifa inatekelezwa dhamana na wajibu wake kwa kushirikiana na mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na Utekelezaji wa Mikataba na Itifaki za Kimataifa. 

Diplomasia ya Vatican: Haki, Amani, Ustawi na Mafao ya Wengi!

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2021, kuna nchi 183 zenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican. Licha ya nchi hizi, pia kuna Umoja wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Malta, Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina. Vatican pia ni mwanachama mtazamaji wa Jumuiya ya Caraibi, CARICOM. Kuna Balozi na Mashirika ya Kimataifa 88 yenye Makazi yake mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 8 Februari 2021 amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya Kimataifa yenye uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2021, kuna nchi 183 zenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican. Licha ya nchi hizi, pia kuna Umoja wa Ulaya, Shirika la Kimataifa la Malta, Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina. Hapo tarehe 4 Juni 2015 Vatican imekuwa pia ni mwanachama mtazamaji wa Jumuiya ya Caraibi, CARICOM. Balozi na Mashirika ya Kimataifa yenye makao yake mjini Roma kwa sasa ni 88 baada ya nchi za Belize, Burkina Faso, Guinea Ekwatorio pamoja na Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina kuanzisha makao yake mjini Roma. Kuna pia Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR. Tarehe 12 Oktoba 2020 Vatican na Austria zilitiliana saini Nyongeza katika Mkataba wa VII wa Makubaliano kuhusu uratibu wa mali ya Kanisa uliotiwa mkwaju na nchi hizi mbili tarehe 23 Juni 1960 huko mjini Vienna, Austria.

Vatican pia imeridhia Mkataba kati yake na DRC uliotiwa mkwaju tarehe 20 Mei 2016 pamoja na Mkataba na Burkina Faso ulioridhiwa na nchi hizi mbili tarehe 12 Julai 2019. Tarehe 5 Mei 2008 Vatican iliridhia Itifaki ya Montreal ya Mwaka 1987 “Montreal Protocol of 1987”. Huu ni Mkataba wa Kimataifa ulioridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zenye kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya ozoni angani, ambayo ni muhimu sana katika kudhibiti kiwango cha mionzi ya jua inayotua ardhini. Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mnururisho wa mionzi kama “Ultraviolet B” isifike kwenye uso wa dunia. Itifaki hii pamoja na mambo mengine inapania kuhamasisha ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kuratibu shughuli mbali mbali za binadamu zinazotishia kuharibu tabaka la hewa ya ozoni angani na hivyo kuchochea kuongezeka kwa joto duniani. Itifaki imepata mafanikio makubwa katika Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa ambayo ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kuna uhusiano wa karibu kati ya ongezeko la joto duniani na kumong’onyoka kwa tabaka la hewa ya ozoni angani. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza zaidi katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani ya binadamu. Elimu makini haina budi kutolewa kwenye vituo vya elimu na utamaduni, mahali wanapoandaliwa wanasiasa, wanasayansi na raia, ili hatimaye, waweze kuwajibika barabara katika maamuzi yao. Ustawi, mafao ya wengi sanjari na maendeleo fungamani yasaidie kuleta maboresho makubwa katika maisha ya watu. Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China, ulitiwa saini tarehe 22 Septemba 2018 kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Tarehe 22 Oktoba 2020, Mkataba huu uliongezwa kwa muda wa miaka miwili. Lengo la Vatican ni kuwapata wachungaji bora watakaotekeleza dhamana na utume wao kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiongozwa na ukarimu katika huduma kwa watu wa Mungu, katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kina ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ukaendelezwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko akashuhudia matunda ya juhudi hizi katika ukweli na uwazi.

Mkazo ni kuhusu shughuli za kichungaji na kitume, ili kuwawezesha waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato huu pamoja na mambo mengine unapania kukoleza: imani na matumaini; umoja na mshikamano wa kidugu. Uteuzi wa Maaskofu kwa ushirikiano kati ya Vatican na Serikali ya China ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini China na kwamba, huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kwa sasa na kwa siku za usoni. Serikali ya China inatambua kunathamini dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kama Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki. Huo ni mwanzo wa amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mungu nchini China. Kumbe, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China hauna uhusiano na masuala ya kisiasa bali unajikita zaidi katika maisha na utume wa Kanisa nchini China, kama kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Balozi Georgios F. Poulides kutoka Cyprus ndiye Dekano wa Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa mjini Vatican, kwa niaba ya Mabalozi wenzake, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili, hususan katika kipindi hiki cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu amejitahidi kuwa karibu na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili, kwa njia ya sala zake. Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 limedhihirisha kwamba, watu wote wanategemeana na kukamilishana, kwani wote wako katika mtumbwi mmoja! Kimsingi, wote ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake, ameendelea kujipambanua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usawa pamoja na utandawazi usiojali wa kuguswa na mahangaiko ya wengine ni mambo ambayo Baba Mtakatifu ameendelea kuyavalia njuga, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kusikia na kujibu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini”.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Msamaria mwema anawekwa mbele ya walimwengu kama ni mfano bora wa kuigwa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu inakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.  Baba Mtakatifu anagusia kuhusu siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni “familia ya Mataifa”. Balozi Georgios F. Poulides anasema kwa ufupi: hii ni dira na mwongozo wa kidiplomasia unaofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga utamaduni wa watu wa kukutana, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kung’oa vikwazo na vizingiti vinavyokwamisha maendeleo fungamani ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Noeli tarehe 25 Desemba 2020 alisema kwamba, katika kipindi hiki cha historia ya mwanadamu, kimeguswa na kutikiswa kwa namna ya pekee kabisa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 “Virusi vya Corona, COVID-19”. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa uchumi na hivyo kusababisha mwelekeo tenge katika jamii, hali inayodai ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu. Huu ni undugu unaofumbatwa katika upendo unaomwezesha mtu kukutana na jirani zake, licha ya tofauti zao msingi. Kwa njia hii, ataweza kuguswa na mateso na mahangaiko yake, tayari kumkaribia, ili kuweza kumhudumia kama alivyofanya yule Msamaria mwema. Haijalishi kama mtu huyu anatoka katika familia, kabila au dini yake, lakini ni ndugu yake. Mwelekeo huu ndio unaopaswa kuzingatiwa hata katika mahusiano na mafungamano kati ya watu na Mataifa. Haki ya huduma bora ya afya, iwe ni kipimo cha upendo unaopaswa kushuhudiwa na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Huu ni wakati wa kushirikiana na kushikamana na wala si kufanya mashindano. Ni muda wa kutafuta suluhu ya kudumu, itakayowawezesha watu wengi zaidi kupata chanjo dhidi ya Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maskini na wahitaji zaidi wapewe kipaumbele cha kwanza. Katika changamoto hii ambayo haitambui mipaka, hakuna sababu msingi ya kuweka vizuizi, kwa sababu binadamu wote wamejikuta wakiwa wamepanda “boti moja” ambayo kwa sasa imekumbwa na dhoruba ya Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021 ulionogeshwa kwa kauli “Utamaduni wa Utunzaji Kama Njia ya Amani” uligusia mambo msingi na changamoto zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa.  madhara ya Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, majanga asilia, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula, hali ngumu ya uchumi kitaifa na kimataifa, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, utaifa, chuki dhidi ya wageni, vita na kinzani mbalimbali chanzo cha maafa! Balozi Georgios F. Poulides anasema changamoto zote hizi ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kujenga umoja na udugu wa kibinadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kulinda mazingira nyumba ya wote.

Mabalozi
09 February 2021, 14:28