Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Yesu alimhurumia mgonjwa wa Ukoma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumtakasa. Changamoto ya kuwa na ujasiri wa kumwendea Kristo Yesu, kwa imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu Francisko: Yesu alimhurumia mgonjwa wa Ukoma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumtakasa. Changamoto ya kuwa na ujasiri wa kumwendea Kristo Yesu, kwa imani, matumaini na mapendo. 

Papa Francisko: Yesu Alimhurumia Mkoma, Akamgusa na Kumtakasa!

Kristo Yesu, alimwachia nafasi yule mgonjwa wa Ukoma kumkaribia. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumtakasa. Huu ni utimilifu wa Habari Njema ya Wokovu inayosema, Mwenyezi Mungu ameamua kuwa jirani mwema katika maisha ya waja wake, ana huruma kwa madonda ya binadamu, amekuja ili kuvunjilia mbali vizingiti vya utengano kati yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwatia shime wamisionari, wafanyakazi katika sekta ya afya na watu wa kujitolea, kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa umakini zaidi. Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki ya afya bora, hasa miongoni mwa maskini na dhaifu ndani ya jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa wataunganisha nguvu zao, ili kufutilia mbali ugonjwa wa Ukoma na hivyo kuwawezesha waathirika kurejea na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii zao. Ikumbukwe kwamba, ugonjwa wa Ukoma unatibika, unganisha nguvu ili kupambana na unyanyapaa; unga mkono juhudi za kuragibisha afya ya akili kwa watu waliokwisha kuathirika kwa ugonjwa wa Ukoma pamoja na magonjwa mengine ya Ukanda wa Joto! Ugonjwa wa Ukoma bado upo na watu wanaendelea kupimwa na kugundulika kwamba wanasumbuliwa na ugonjwa wa Ukoma. Inaonekana kana kwamba, ugonjwa huu pamoja na wagonjwa wenyewe wamesahaulika, jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 68 ya Ukoma Duniani kwa Mwaka 2021 ambayo ilinogeshwa kwa kauli mbiu: “Pambana na ukoma, Ondoa unyanyapaa, Ragibisha afya ya akili”

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mwinjili Marko anamwonesha Kristo Yesu aliyekutana na Mkoma, akamtakasa. Wagonjwa wa Ukoma walihesabiwa kuwa najisi na hivyo kadiri ya sheria walipaswa kutengwa na kukaa nje kabisa ya makazi ya watu. Walitengwa na hawakupaswa kuwa na mahusiano ya kiutu, kijamii na kidini. Kristo Yesu, alimwachia nafasi yule mgonjwa wa Ukoma kumkaribia. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumtakasa. Huu ni utimilifu wa Habari Njema ya Wokovu inayosema, Mwenyezi Mungu ameamua kuwa jirani mwema katika maisha ya waja wake, ana huruma kwa madonda ya binadamu na kwamba, amekuja ili kuvunjilia mbali vizingiti vinavyokwamisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na waamini kutoka katika undani wao! Ukaribu, Wema na Huruma ni mambo yanayopaswa kupewa uzito wa pekee kabisa!

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili 14 Februari 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, katika tukio hili, Mwinjili Marko anaweka mbele ya macho ya waamini “wavunja sheria wawili” wanaokutana yaani: Mgonjwa wa Ukoma anayemwendea Kristo Yesu kinyume cha sheria na Kristo Yesu ambaye alishikwa na huruma na upendo, akamgusa na kumtakasa. Licha ya sheria kali iliyokuwepo dhidi ya wagonjwa wa Ukoma, lakini, Mkoma anayezungumziwa kwenye Injili ya Marko, aliweza kuvuka viunzi na vikwazo vyote, hata akafanikiwa kukutana na Kristo Yesu mubashara. Ukoma ulihesabiwa kuwa ni adhabu ya dhambi zilizotendwa na mgonjwa mwenyewe. Lakini, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ndiye anayewagusa, kuwataka na kuwaponya na Ukoma wao, kwani hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na huruma ya Mungu.

Ni huruma na upendo unaoweza kumwokoa mwanadamu kutoka katika hali ya kutengwa, kwani katika Kristo Yesu, mgonjwa anapata mwandani wa maisha, anayeshirikiana naye katika mateso na mahangaiko yake. Mgonjwa huyu wa Ukoma alivutwa sana na ushuhuda wa Kristo Yesu, kiasi cha kupiga moyo konde kwa kutoka katika undani wake na kumwendea Kristo Yesu, ili kumwaminisha historia ya mateso na mahangaiko yake. Baba Mtakatifu anasema, “Mtuhumiwa wa pili” ni Kristo Yesu ambaye alifahamu fika kwamba, ilikuwa ni marufuku kumgusa mgonjwa wa Ukoma, lakini Yeye: akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumtakasa. Kristo Yesu alifanya “kweli” si tu kwa maneno, bali kwa kumgusa na kumtakasa kwa huruma na upendo mkuu uliojenga uhusiano na mafungamano ya dhati yanayokita mizizi yake katika maisha, kiasi hata cha kuweza kushirikishana hata madonda ya maisha! Hapa Kristo Yesu anatangaza na kushuhudia kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kumgeuzia mtu kisogo ili kutekeleza sheria ya usalama kwa kuwa mbali na mgonjwa wa Ukoma. Anavunja sheria hii, kwa huruma na upendo kiasi cha kugusa maisha ya mgonjwa wa Ukoma na kumtakasa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata leo hii, bado kuwa maelfu ya watu wanaoteseka na ugonjwa wa Ukoma na magonjwa mengine ambayo kimsingi yanahusianishwa na maamuzi mbele ya kijamii. Katika baadhi ya magonjwa kuna hata ubaguzi kwa misingi ya kidini. Inawezekana kwamba, kila mtu katika safari ya maisha yake, akawa amepata madonda, akateleza na kuanguka; akateseka kutokana na ubinafsi unaowafanya kuwabagua wengi na Mungu pamoja na jirani zao. Pamoja na “patashika zote hizi nguo kuchanika” leo Kristo Yesu anatangaza na kushuhudia kwamba, “Mwenyezi Mungu si wazo la kufikirika au mafundisho ya ajabu” bali kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ameamua “kujichanganya na binadamu” ili kugusa, kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu, bila woga wala makunyanzi. Baba Mtakatifu amewapongeza wakleri wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa maisha na utume wao, ili kuwaonjesha watu wa Mungu: Ukaribu, wema na huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao. Hawa ndio wamisionari wa huruma ya Mungu wanaoendelea kuungamisha sehemu mbalimbali za dunia katika hali ya ukimya na unyenyekevu mkuu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kwa kuheshimu na kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na heshima, watu wanathubutu kunyamazisha mateso na mahangaiko ya watu. Wanavaa vinyago usoni ili wasionekane, wala kuhusishwa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wamwombe Mwenyezi Mungu ili awakirimie neema na baraka za kuishi kama hawa watu wawili waliovunja sheria kama anavyosimulia Mwinjili Marko. Mgonjwa wa Ukoma awe ni mfano bora kwa waamini kutoka katika undani na ubinafsi wao, unaowafunga na kuwafanya kila siku kulalama tu kutokana na kushindwa katika maisha. Mwanamke mdhambi aliyemwendea Kristo Yesu na kumpaka mafuta safi ni mfano bora wa kuigwa, kwani alipata nafasi ya kukutana mubashara na huruma na upendo wa Mungu, kiasi cha kusamehewa dhambi zake

Waamini wawe na ujasiri wa “kupiga moyo konde” na kumwendea Kristo Yesu kwa imani na ujasiri mkuu, ukweli na uwazi na jinsi walivyo! Waamini wajitahidi kumuiga Kristo Yesu aliyevunja sheria, kwa kumwonea huruma, akamwendea Mkoma, akamgusa na kumtakasa. Kwa kufanya hivi, Kristo Yesu, anavunjilia mbali vizingiti vya maamuzi mbele, woga na wasi wasi tayari “kujichanganya katika maisha ya watu wengine”. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awasindikize katika hija hii ya toba na wongofu wa ndani!

Papa: Ukoma

 

 

 

14 February 2021, 15:32