Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Watakatifu Angela Merici na Mtakatifu Thoma wa Akwino ni mifano bora ya kuigwa katika kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha! Papa Francisko: Watakatifu Angela Merici na Mtakatifu Thoma wa Akwino ni mifano bora ya kuigwa katika kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha!  (ANSA)

Watakatifu Thoma wa Akwino na Angela Merici: Mashuhuda wa Neno!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Angela Merici ni mfano bora wa kuigwa katika kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha. Mtakatifu Thoma wa Akwino, Msimamizi wa Shule Katoliki Duniani ni mfano bora na mwaliko kwa wanafunzi kumwangalia Kristo Yesu kuwa ndiye Mwalimu na Mlezi wao mkuu katika maisha ya kila siku! Hekima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Angela Merici, Bikira alizaliwa tarehe 21 Machi 1474 March 21, Lombardia, Kaskazini mwa Italia. Akiwa na umri wa miaka 10, wazazi wake walifariki dunia na akabaki na dada yake tu. Na baada ya muda mfupi, dada yake nae akafariki dunia. Mtakatifu Angela Merici alijiunga na Utawa wa tatu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, ambako aliweka nadhiri ya ubikira. Akiwa na miaka 20, mjomba wake, ambaye ndiye aliyekuwa mlezi wake, alikufa. Mtakatifu Angela aliamua kurudi kijijini kwao ambako aliona wasichana wengi wakiishi maisha yasiyo mpendeza Mungu. Hawakuwa na elimu wala matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Na wazazi wao hawakujali. Mtakatifu Angela Merici aliamua kufungua kituo nyumbani kwao, akiwafundisha wasichana hao kuhusu: Katekesi, na Sala hususan juu ya imani ya Kanisa Katoliki. Mwaka 1524 alifanya hija katika Nchi Takatifu, lakini alipata maradhi ya upofu katika kisiwa cha Crete. Aliendelea na hija hiyo akiwa kipofu akipita sehemu zote. Akiwa njiani kurudi nyumbani, aliweza tena kuona. Kunako Mwaka 1525 alienda mjini Roma ili kuhiji na Papa alisikia habari zake na alimfurahia mno.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 25 Novemba 1535, Mtakatifu Angela akiwa na mabikira 12, walianzisha rasmi Shirika la Watawa wa Ursoline. Shirika lilikuwa na kupanuka kiasi hata cha kuweza kufungua vituo vya kulelea watoto yatima na shule. Mwaka 1537 Mtakatifu Angela alichaguliwa kuwa mkuu wa Shirika. Sheria, Kanuni na Taratibu za shirika zilipitishwa mwaka 1544 na Papa Paulo III. Mtakatifu Angela Merici aliitupa mkono dunia hapo, tarehe 27 Januari 1540 akazikwa katika Kanisa la Mtakatifu Afra Brescia. Alitangazwa kuwa Mwenyeheri mwaka tarehe 30 Aprili. 1768 na Papa Clement XIII. Akatangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 24 Mei,1807 na Papa Pius VII. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Januari 2021 amesema kwamba, Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Angela Merici, Muasisi wa Shirika la Kitawa la Ursoline.

Kutokana na tasaufi yake, kuna mashirika mengi ya Waorsoline yameibuka na kuenea sehemu mbalimbali dunia hata kufanikiwa kufika nchini Poland. Mtakatifu Angela Merici akiwa anaongozwa na Neno la Mungu katika maisha na utume wake, aliwahimiza watawa wake, kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani zao. Aliwataka kujizatiti kwa ujasiri katika sekta ya elimu kwa ajili ya watoto na vijana wa kizazi kipya, huku akiwataka kuendelea kuhifadhi mila na desturi njema, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa maisha mapya. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Angela Merici ni mfano bora wa kuigwa katika kusoma, kulitafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika maisha, ili kulitangaza na kulishuhudia kwa furaha kama kielelezo cha imani tendaji!

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 28 Januari 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, Msimamizi wa Shule Katoliki. Kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2020, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Angelicum, kilichoko mjini Roma, kilizindua rasmi Taasisi ya Utamaduni, ambayo iko chini ya Kitivo cha Falsafa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko alimwandikia ujumbe, Padre Michal Paluch, O.P., Gambera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum, akimpongeza kwa hatua hii muhimu. Baba Mtakatifu aliwapongeza wajumbe wa Mfuko wa “Futura Iuventa” na wa “Saint Nicholas” inayofadhili Taasisi ya Utamaduni, Chuo Kikuu cha Angelicum. Baba Mtakatifu alisema, lengo la Taasisi hii ni kufanya upembuzi yakinifu kuhusu tamaduni mamboleo, kwa kushirikiana na wanafalsafa, wanataalimungu pamoja na wanawake waliobobea katika medani hii. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni muasisi na lengo kuu la Mradi huo. Ni kiongozi wa Kanisa anayestahili kupewa shukrani kutokana na amana na utajiri mkubwa ambao ameliachia Kanisa; lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa uwazi wa mawazo yake, tafakari ya kina sanjari na upendo wake kwa Mwenyezi Mungu na binadamu; kwa kazi ya uumbaji, historia na sanaa!

Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko ametoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, lakini zaidi wanafunzi, kuiga mfano wa Mtakatifu Thoma wa Akwino, ili kumwangalia Kristo Yesu kuwa ndiye mwalimu pekee wa maisha! Mafundisho ya Mtakatifu Thoma wa Akwino yawatie shime watu wa Mungu kujiaminisha katika hekima na busara ya kiroho, ili kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao.

Watakatifu
27 January 2021, 14:54