Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amemtumia Dr. Bernice Albertin King salam na matashi mema wakati wa maadhimisho ya Siku ya Martin Luther King, Jr. tarehe 18 Januari 2021. Baba Mtakatifu Francisko amemtumia Dr. Bernice Albertin King salam na matashi mema wakati wa maadhimisho ya Siku ya Martin Luther King, Jr. tarehe 18 Januari 2021. 

Ujumbe wa Papa Francisko: Sikukuu ya Martin Luther King Jr.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ulimwengu mamboleo unakumbana na changamoto za ukosefu wa haki jamii, mipasuko, migawanyiko pamoja na kinzani zinazokwamisha mchakato wa mafao ya wengi, utulivu, amani na usawa kati ya watu. Haya yote ni mambo ambayo yanapaswa kupatikana kwa njia ya amani kama ambavyo Martin Luther King Jr. alitamani kuona yakitendeka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Martin Luther King Jr. alizaliwa tarehe 15 Januari 1929 huko Atlanta, Georgia, nchini Marekani. Alikuwa ni mchungaji wa Kiprotestant, mwanasiasa, mwana harakati mashuhuri na kiongozi aliyejipambanua kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wananchi wa Amerika wenye asili ya Kiafrika. Aliuwawa kikatili kunako tarehe 4 Aprili 1968 huko Mephis, Tennessee, nchini Marekani. “I Have a Dream” ni kati ya hotuba zake kali zinazokumbukwa na wapenda haki na amani duniani. Alibahatika kupata watoto wane na kati yao ni Bernice Albertine King. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa matashi mema Bernice Albertine King ambaye pia ni Rais wa Jumuiya “King Center” iliyoko huko Atlanta katika maadhimisho ya “Martin Luther King Day” yaani: Siku ya Martin Luther King Jr. ambayo imeadhimishwa hapo tarehe 18 Januari 2021.

Imekuwa ni fursa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai pamoja na mafanikio yote ambayo Martin Luther King Jr. alibahatika kuyapata. Baba Mtakatifu anasema, ulimwengu mamboleo unakumbana na changamoto za ukosefu wa haki jamii, mipasuko, migawanyiko pamoja na kinzani zinazokwamisha mchakato wa mafao ya wengi, utulivu, amani na usawa kati ya watu. Haya yote ni mambo ambayo yanapaswa kupatikana kwa njia ya amani kama ambavyo Martin Luther King Jr. alitamani kuona yakitendeka. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mwananchi anahimizwa kuwa ni chombo cha amani na chachu inayowaunganisha watu na kamwe asiwepo mtu anayepanda mbegu ya utengano kati ya watu, ili kuzima moto wa chuki na uhasama kati ya watu, ili hatimaye, kufungua njia mpya ya majadiliano katika ukweli na uwazi.

Ni katika hali na mazingira kama haya, watu wataweza kuonana na kuthaminiana kama jirani wema, kwa sababu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe ni watoto wateule wa Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kujizatiti kumwilisha dira na maono haya katika uhalisia wa maisha ya kila siku, ili hatimaye, kujenga na kudumisha jumuiya inayojikita katika haki na udugu wa upendo! Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Bernice Albertine King kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Martin Luther King Jr., kwa kuwapatia wote baraka zake za kitume, huku akiwaombea wingi wa hekima na amani kutoka mbinguni!

Papa Martin L. King

 

 

 

19 January 2021, 14:51