Tafuta

Tarehe 27 Januari, Jumuiya ya Kimataifa Inaadhimisha Kumbukumbu ya Mauaji ya Shoah yaliyotokea kati ya Mwaka 1940 -1945. Wayahudi kati ya milioni 5-6 waliuwawa kikatili. Tarehe 27 Januari, Jumuiya ya Kimataifa Inaadhimisha Kumbukumbu ya Mauaji ya Shoah yaliyotokea kati ya Mwaka 1940 -1945. Wayahudi kati ya milioni 5-6 waliuwawa kikatili. 

Papa: Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Shoah, 27 Januari 1945

Kumbukumbu ya watu walioteswa na hatimaye kuuwawa kikatili wakati wa utawala wa Kinazi, iguse utu wa binadamu. Kumbukumbu ni alama ya ustaarabu, ili kujizatiti kwa ajili ya siku za usoni ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajibidiisha katika mchakato wa ujenzi wa amani na udugu wa kibinadamu. Ni angalisho ili mauaji ya kimbari yasijirudie tena kwa kudhibiti sera potofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maangamizi makubwa dhidi ya Wayahudi wa Ulaya: Holocaust, kwa lugha ya Kiebrania Shoah השואה) yalikuwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi milioni 5-6 kutoka Barani Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya miaka 1940 na 1945. Mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na serikali ya Ujerumani chini ya Adolf Hitler kwa msaada wa serikali za nchi zilizofungamana na Ujerumani au zilizokuwa chini ya jeshi la Ujerumani. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika historia ya mwanadamu, Wayahudi wamekumbana na nyanyaso pamoja na dhuluma, kiasi hata cha kukabiliana uso kwa uso na mauaji ya kimbari wakati wa Shoah.

Waamini wa dini ya Kiyahudi kati ya milioni tano hadi sita, walipoteza maisha yao kwa vile tu walikuwa ni Wayahudi. Haya ni matokeo ya sera zilizojimwambafai na mwanadamu kutaka kuchukua nafasi ya Mwenyezi Mungu. Historia iliyopita isaidie kuboresha hali ya siku za mbeleni; tayari kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na amani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 27 Januari 2021 amesema kwamba, tarehe 27 Januari ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Shoah yaliyotokea kwenye kambi ya mateso na mauaji ya kimbari ya Auschwitz Birkenau.

Hii ni siku ambayo kambi hiyo ambayo imeacha kurasa chungu katika maisha na nyoyo za watu, ilipokombolewa rasmi na watu waliokuwemo humo kuachiwa huru! Kumbukumbu ya watu walioteswa na hatimaye kuuwawa kikatili wakati wa utawala wa Kinazi, iguse utu wa binadamu. Kumbukumbu ni alama ya ustaarabu, ili kujizatiti kwa ajili ya siku za usoni ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajibidiisha katika mchakato wa ujenzi wa amani na udugu wa kibinadamu. Ni angalisho la kuendelea kuwa makini ili mauaji ya kimbari kama haya yasijirudie tena, kwa kudhibiti sera “zinazojidai” kutaka kuokoa baadhi ya watu, lakini mwishoni, wanaishia kwa mauaji ya kimbari. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kutoa angalisho jinsi ambavyo sera za mauaji ya kimbari huko Auschwitz Birkenau yalivyoanza kwa kuwatumbukiza watu katika mateso, kifo na hatimaye mauaji ya kimbari!

Kumbukumbu ya Shoah
27 January 2021, 15:33