Tafuta

Papa Francisko: Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa unaopokelewa kwa imani, kutangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kiini cha Injili ya Kristo Yesu. Papa Francisko: Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa unaopokelewa kwa imani, kutangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kiini cha Injili ya Kristo Yesu. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Yesu Ni Mwanga Na Wokovu wa Mataifa

Baba Mtakatifu Francisko asema: Sherehe ya Tokeo la Bwana ni mwendelezo wa maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, ambalo ni mwanga unaowangazia watu wote. Huu ni mwanga angavu unaopokelewa kwa njia ya imani, ili kuwapelekea wengine kwa njia ya upendo unaotangazwa na kushuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kiini cha Injili ya Kristo! Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania kama inavyojulikana kwa lugha ya Kigiriki ἐπιφάνεια, epifaneia, ni Sherehe ya ufunuo wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa anayejifunua kwa watu wote bila ubaguzi kwa kutambua kwamba, wokovu ulioletwa kwa njia ya Kristo Yesu hauna mipaka. Sherehe ya Tokeo la Bwana ni mwendelezo wa maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, ambalo ni mwanga unaowangazia watu wote. Huu ni mwanga angavu unaopokelewa kwa njia ya imani, ili kuwapelekea wengine kwa njia ya upendo unaotangazwa na kushuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kiini cha Injili ya Kristo! Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Tokeo la Bwana, inawaletea waamini mwangwi wa maneno ya Nabii Isaya kuhusu Nuru ya Mungu inayoangaza ulimwenguni hususan katika kipindi hiki ambacho Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia maafa makubwa kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Nabii Isaya anasema, “Maana, tazama, giza litaifunika dunia, na giza kuu litazifunika kabila za watu; bali Bwana atakuzukia wewe, na utukufu wake utaonekana juu yako”. (Isa. 60: 2). Nabii Isaya anatangaza na kushuhudia Nuru ya Mungu itakayoangaza mji wa Yerusalemu ni Nuru ambayo pia itawaangazia watu wote.

Ni Nuru yenye nguvu na mvuto kwa watu walio karibu na hata kwa wale wanaoishi mbali; kwani wote kwa pamoja wanaweza kufunga safari ili kuiendea Nuru hii. Mwono wa Nabii Isaya inafungua nyoyo za waamini, unawapatia watu fursa ya kuweza kupumua kwa nguvu kwani huu ni wito wa matumaini. Kwa hakika giza bado ni tishio kubwa katika maisha ya kila mwamini na hata katika historia ya maisha ya mwanadamu. Lakini, ikumbukwe kwamba, Nuru ya Mungu ina nguvu sana, wito mahususi ni kuipokea Nuru hii angavu na kuisambaza kwa wengine, kwa sababu ni chemchemi ya furaha kubwa kwa mji wa Yerusalemu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, Jumatano tarehe 6 Januari 2021 kutoka katika Maktaba ya Kitume iliyoko mjini Vatican. Hii pia ni Sikukuu ya Utoto Mtakatifu, ambayo kwa mwaka 2021 inaongozwa na kauli mbiu “Tunogeshe udugu wa kibinadamu”. Mwinjili Mathayo kwa upande wake anajielekeza kufafanua tukio la Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliofunga safari kwenda kumtafuta Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa mjini Bethlehemu walipomwona Mtoto Yesu, Maria na Yosefu wakaanguka na kumsujudia.

“Nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu: dhahabu na uvumba na manemane.” Mt. 2: 11-12. Zawadi hizi zinafumbata maana na utume wa Kristo Yesu hapa duniani. Dhahabu ni kielelezo cha heshima ya hali ya juu kwa Kristo Yesu kama Mfalme. Huu ni ufalme wa kweli na uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Uvumba unadokeza Umungu wa Kristo Yesu. Hii ni alama ya upendo na sadaka itakayofikia kilele chake Mlimani Kalvari. Manemane inaashiria ubinadamu wake ambao umefunuliwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Mwinjili Mathayo inasema kwamba Nuru hii angavu ni Mtoto Yesu, ambaye Ufalme wake, haukukubaliwa na wengi. Ni nyota angavu, Masiha aliyekuwa akisubiriwa na wengi, ili kwa njia yake Mwenyezi Mungu aweze kutekeleza Ufalme wake hapa duniani unaosimikwa katika upendo, haki na amani. Mtoto Yesu amezaliwa si tu kwa wateule wachache, bali ni kwa ajili ya walimwengu wote.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Nuru angavu ya Mtoto Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu inazidi kung’ara si kwa njia ya watawala na watu wenye nguvu katika ulimwengu mamboleo, ambao daima wamekuwa wakitaka kuififisha Nuru hii. Nuru ya Kristo Yesu, inang’aa kwa kwa njia ya Injili inayotangazwa na kushuhudiwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na imani tendaji. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ameamua kuja na kukaa kati pamoja na waja wake. Kwa njia hii, amekuwa ni jirani mwema na daraja ya kuwakutanisha watu katika uhalisia wa maisha yao. Kristo Yesu ni Nuru ya Mungu ambaye ni Upendo wenye mvuto na mashiko, unaowavuta na kuwaambata wote. Kimsingi, Kristo Yesu ndiye ile Nyota angavu, lakini, kila mwamini anapaswa kuwa ni nyota angavu kwa ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wale wote anaokutana nao katika safari ya maisha yake.

Waamini wawe ni Nyota ya amana na utajiri wa wema, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani; upendo ambao Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu anawapatia watu wote bure kabisa. Changamoto na mwaliko ni kwa kila mwamini kuupokea Mwanga huu angavu, tayari kuwashirikisha wengine miale yake. Ole wao, wanaotaka kuukumbatia na kuumiliki kama mtu binafsi. Kama ilivyokuwa kwa Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali, wataalam wa nyota, waamini pia wanaitwa na kuchangamotishwa na Mama Kanisa ili kweli waweze kujiachia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwashangaza kwa Nyota angavu, wavutwe, waongozwe na kuangaziwa na Nyota hii, ili hatimaye, waweze kutubu na kumwongokea Kristo Yesu. Hii ni hija safari ya maisha ya kiroho inayofumbatwa katika sala na tafakari ya matendo makuu ya Mungu yanayoendelea kuwajaza waja wake furaha na mshangao wa maisha. Nuru ya Kristo haiwezi kuenezwa kwa wongofu wa shuruti, bali kwa njia ya kutangaza na kushuhudia kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji, hata ikiwezekana kumwaga damu kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Mwishoni mwa tafakari yake kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu, amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa ajili ya Kanisa zima, ili hatimaye, Habari Njema ya Kristo Yesu Mwanga wa Mataifa, “Lumen gentium”, iweze kuwafikia na kuwaambata watu wote duniani!

Papa: Angelus Epifania

 

06 January 2021, 15:50