Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 26 Januari 2021 amehudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Prof. Fabrizio Soccorsi aliyekuwa daktari wake binafsi kuanzia mwaka 2015-2021. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 26 Januari 2021 amehudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Prof. Fabrizio Soccorsi aliyekuwa daktari wake binafsi kuanzia mwaka 2015-2021. 

Prof. Soccorsi Daktari Binafsi wa Papa 2015-2021 Afariki Dunia!

Ilikuwa ni tarehe 8 Agosti 2015 Baba Mtakatifu Francisko alipomteua Professa Fabrizio Soccorsi kuwa daktari wake binafsi. Alikuwa ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya tumbo. Baada ya kutunukiwa shahada ya uzamivu katika magonjwa ya binadamu alitekeleza utume huu kwa uadilifu na weledi mkubwa. Alizaliwa tarehe 2 Februari 1942 Roma na kufariki dunia 9 Januari 2021.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 26 Januari 2021 ameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Familia mjini Vatican, kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Professa Fabrizio Soccorsi, daktari binafsi wa Papa Francisko, aliyefariki dunia, Jumamosi tarehe 9 Januari 2021. Professa Soccorsi ameaga dunia baada ya kushambuliwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Tangu tarehe 26 Desemba 2020 alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Saratani. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi waandamizi kutoka Vatican.

Professa Fabrizio Soccorsi, alizaliwa tarehe 2 Februari 1942 mjini Roma. Amefariki dunia wakati alipokuwa anajiandaa kuadhimisha miaka 79 tangu alipozaliwa. Ilikuwa ni tarehe 8 Agosti 2015 Baba Mtakatifu Francisko alipomteua Professa Fabrizio Soccorsi kuwa daktari wake binafsi. Alikuwa ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya tumbo. Baada ya kutunukiwa shahada ya uzamivu katika magonjwa ya binadamu alibahatika kutekeleza utume huu kwa uadilifu na weledi mkubwa, kiasi cha kuteuliwa kuwa mkuu wa kitengo cha magonjwa ya ndani, Hopitali ya San Camillo-Forlanini, iliyoko mjini Roma.

Professa Fabrizio Soccorsi, alibahatika kuwa ni jaalimu wa “kutupwa” mkoani Lazio lakini kwa namna ya pekee katika Chuo Kikuu cha “La Sapienza” kilichoko mjini Roma. Professa Soccorsi alikuwa ni mtaalam mshauri wa Wizara ya Afya nchini Italia, Kurugenzi ya Afya na Usafi mjini Vatican na pia Daktari mshauri wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Kutokana na mchango wake mkubwa kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Italia, lakini kutokana na uhusiano wa karibu aliokuwa nao kwa Baba Mtakatifu Francisko kama daktari wake binafsi, aliamua kuhudhuria Ibada ya Misa ya Mazishi ya Professa Fabrizio Soccorsi, kwa kimya na tafakari ya kina kuhusu hatima ya maisha ya mwanadamu hapa duniani.

Professa Soccorsi
28 January 2021, 13:19