Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema, Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii katika Agano Jipya na la Milele! Ni Mwana wa Mungu aliyetangaza Habari Njema na Kuwaponya wagonjwa. Baba Mtakatifu Francisko asema, Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii katika Agano Jipya na la Milele! Ni Mwana wa Mungu aliyetangaza Habari Njema na Kuwaponya wagonjwa. 

Papa Francisko: Yesu Ni Utimilifu wa Unabii: Kutangaza na Kuponya

Papa Francisko: Kwa ufupi maisha na utume wa Kristo Yesu yaligawanyika katika sehemu kuu mbili yaani: kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu sanjari na kuganga na kuwaponya wagonjwa! Sehemu hii ya Injili kadiri ya Marko inaonesha Siku ya Yesu ilivyokuwa. Lakini leo anakita mawazo yake katika Siku ya Sabato ambayo kwa Wayahudi ilikuwa ni Siku ya Mapumziko na Siku ya Sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Marko 1: 21-28 anawaalika waamini kuendelea kumjifunza Kristo Yesu kama sehemu ya safari yao ya imani, wakitambua kwamba: Yesu, ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; ni utimilifu wa ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu. Sabato ni Siku ya Mungu; ni Siku ya Kristo Yesu; Ni Siku ya Kanisa; Ni Siku ya binadamu na ni Siku ya kutafakari mambo ya nyakati kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kitume “Dies Domini” yaani “Siku ya Bwana”. Useja na usafi kamili ni zawadi kwa ajili ya ufunuo wa sura ya huruma na upendo wa Baba wa milele. Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii wa Agano Jipya na la milele kwani mafundisho yake yalikuwa yanabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake na kuwashangaza wengi. Alikazia utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Alitambua umuhimu wa Sabato kuwa ni siku ya Mungu na ni Siku ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tarehe 31 Januari 2021, kutoka katika Maktaba yake binafsi iliyoko mjini Vatican amesema, kwa ufupi maisha na utume wa Kristo Yesu yaligawanyika katika sehemu kuu mbili yaani: kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu sanjari na kuganga na kuwaponya wagonjwa! Sehemu hii ya Injili kadiri ya Marko inaonesha Siku ya Yesu ilivyokuwa. Lakini leo anakita mawazo yake katika Siku ya Sabato ambayo kwa Wayahudi ilikuwa ni Siku ya Mapumziko na Siku ya Sala. Kristo Yesu anatumia Siku hii kudhihirisha uwezo wake katika Sinagogi la Kapernaumu, humo anasoma na kutoa tafakari ya Neno la Mungu, kiasi cha kuwashangaza mno kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri na wala si kama waandishi. Kristo Yesu ni utimilifu wa unabii uliotolewa na Musa katika Agano la Kale.

Kristo Yesu anazungumza kwa Mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi Mungu, kwani Kristo Yesu ni Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Mungu Mwana anayeganga, kuponya na kuwaokoa watu wake! Kristo Yesu alijipambanua kama mtu mwenye mamlaka katika kutenda, kiasi cha kutambuliwa na mtu mwenye pepo mchafu, kuwa ni Mtakatifu wa Mungu. Lakini Kristo Yesu atamtambua yule pepo mchafu na kumkemea akimwambia “fumba kinywa na umtoke”. Kutangaza, kushuhudia, kuganga na kuwaponya watu ni mambo ambayo Mwinjili Marko anayeelezea katika sehemu hii ya Injili, lakini mkazo zaidi ni kwa ajili ya: Kuhubiri, yaani kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kazi ya kutoa pepo wachafu ilikuwa ni kielelezo cha mamlaka na nguvu ya neno lake linaloponya na kuokoa! Huu ni mwaliko kwa waamini kutembea na Biblia Takatifu, ili Neno la Mungu liendelee kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao.

Kristo Yesu alihubiri kwa mamlaka, akaonesha umahiri wake kwamba alikuwa na mafundisho yaliyokuya yanabubujika kutoka katika undani wake na wala si kama waandishi waliotegemea mapokeo na sheria walizopewa. Mafundisho ya Kristo Yesu yalikuwa yanabubujika kutoka kwa Baba yake wa milele! Kumbe, alikuwa anahubiri na kufundisha kwa mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi, kwa kuganga, kuponya na kuokoa watu. Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii, kwani anasema na kutenda kila anachosema kwani kwa hakika ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Kwa njia hii, anazungumza akiwa na mamlaka ya Kimungu! Mwinjili Marko anamwonesha Kristo Yesu akiganga, akiponya na kuwaokoa watu waliokuwa wameelemewa na magonjwa pamoja na pepo wachafu. Mahubiri ya Kristo Yesu yanalenga kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye ubaya unaomzunguka na uliomo ulimwenguni. Neno lake linapambana moja kwa moja na ufalme wa Shetani, Ibilisi, kiasi cha “kumpigisha magoti” na kumwambia “Fumba kinywa, umtoke!” Mtu yule aliyekuwa na pepo mchafu akaponywa na hivyo kugeuka na kuwa ni mtu mpya kabisa!

Mahubiri ya Kristo Yesu ni tofauti kabisa na yale ya Shetani, Ibilisi pamoja na yale yanayotolewa na walimwengu. Mahubiri ya Shetani yanaonesha jinsi ambavyo ulimwengu unavyokwenda kombo! Yule mwenye pepo mchafu alimkaribia Kristo Yesu na kupaaza sauti “Tuna nini nawe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza. Haya ni maneno yanayodhihirisha tofauti kubwa kati ya Kristo Yesu na Shetani, Ibilisi, wanaotenda kwa ngazi tofauti kabisa, wala hakuna jambo lolote linalowaunganisha, bali wanasigana sana! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushangaa kama ilivyokuwa kwa waamini katika Sinagogi la Kapernaumu, walipokuwa wanamsikiliza Kristo Yesu akitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwaondolea dhambi, kuwaganga na kuwaponya kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu!

Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa wakati ambapo Injili Takatifu inatangazwa katika liturujia ya Kanisa, ili waamini waweze kuonja ile nguvu ya neno la Kristo Yesu. Hivi ndivyo pia inavyopaswa kuwa pale mwamini binafsi, anapojisomea Injili Takatifu, huku akiwa na moyo wazi, kwani hapo mwanga na nguvu ya Kristo Yesu inapenya, inajaliwa mema, inawaangaza, inawaponya na kuwafariji. Bikira Maria alibahatika katika maisha yake, kulihifadhi Neno la Mungu na kufuatilia kwa uaminifu na uwajibikaji mkubwa kwa matendo ya Kristo Yesu. Bikira Maria awasaidie waamini kumsikiliza na kumfuata Kristo Yesu, ili kuonja katika maisha alama za wokovu wake!

Papa Dies Domini
31 January 2021, 15:47