Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Waamini Jengeni Utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yenu! Papa Francisko: Waamini Jengeni Utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha yenu!  (ANSA)

Papa: Jengeni Utamaduni wa Kusoma Maandiko Matakatifu!

Waamini waendelee kujifunza “Lectio Divina, yaani “Masomo ya Kimungu”, kwa kusoma na kusali Maandiko Matakatifu, chemchemi ya nguvu, amani na utulivu katika maisha. Wahakikishe kwamba, hakuna jambo lolote linaloweza kuwa ni kizuizi cha kuendelea kukua katika ujenzi wa urafiki na Yesu tayari kutangaza na kushuhudia wema, upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Januari 2021 wakati wa Katekesi yake kutoka kwenye Maktaba binafsi ametafakari kuhusu umuhimu wa Sala kwa Kutumia Maandiko Matakatifu, yaani “Lectio Divina” yaani “Masomo ya kimungu ambayo yamegawanyika katika hatua kuu nne: Kusoma, “Lectio”, Kuwaza “Meditatio”, Kusali “Oratio” na Tafakari “Contemplatio! Kanisa linayaheshimu Maandiko Matakatifu kama linavyouheshimu Mwili wa Kristo. Haliachi kamwe kuwapa waamini mkate wa uzima, unaochukuliwa kutoka meza ya Neno la Mungu na meza ya Mwili wa Kristo. Katika Maandiko Matakatifu, Kanisa linapata siku zote chakula na nguvu yake inayobubujika kutoka katika Neno la Mungu.

Kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Mwenyezi Mungu huwashukia watoto wake ili kuingia katika majadiliano na mazungumzo nao! Rej. KKK. 103- 104. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujichotea amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu, kwa njia ya sala. Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao. Walau kila siku, wachague kifungu kimoja cha Maandiko Matakatifu, kitakachowasindikiza siku nzima ya maisha. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu itawasaidia kutambua na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Anawaombea ili Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza katika hija hii ya maisha ya kiroho.

Waamini waendelee kujifunza “Lectio Divina, yaani “Masomo ya Kimungu”, kwa kusoma na kusali Maandiko Matakatifu, chemchemi ya nguvu, amani na utulivu katika safari ya maisha ya kila siku! Waamni wahakikishe kwamba, hakuna jambo lolote linaloweza kuwa ni kizuizi cha kuishi na kuendelea kukua katika mchakato wa ujenzi wa urafiki wa dhati na Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia wema, upendo na huruma yake isiyokuwa na kifani. Baba Mtakatifu amewataka wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya kujitosa bila ya kujibakiza, kila mtu kadiri ya hali na nafasi yake kushiriki kwa ukarimu mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya kumpenda na kumhudumia Kristo Yesu kwa njia ya jirani.

Sala na Biblia

 

 

27 January 2021, 15:16