Tafuta

Papa Francisko: Anawahimiza vijana wa kizazi kipya kushiriki katika michezo kwa ajili ya kujenga urafiki na udugu wa kibinadamu! Papa Francisko: Anawahimiza vijana wa kizazi kipya kushiriki katika michezo kwa ajili ya kujenga urafiki na udugu wa kibinadamu! 

Baba Mtakatifu Francisko: Umuhimu wa Michezo Kwa Vijana!

Michezo ni nyenzo msingi katika kudumisha haki msingi za binadamu; ni mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano unaovunjilia mbali ubinafsi. Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili, Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu wa kibinadamu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja na kuwa na upendeleo kwa maskini na akina “yakhe pangu pakavu tia mchuzi”.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Januari 2021 amekutana na kuzungumza na wachezaji wa Timu ya “Spezia” waliomtembelea mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa ushindi walioupata kwa kuwatwanga wapinzani wao magoli manne kwa mawili. Mashabiki wa kabumbu wanasema, wamewanyuka kwa “4G”. Papa amewataka kusonga mbele kwa ujasiri zaidi kwa kuwakumbusha kwamba, nchini Argentina, licha la soka kutawala lakini pia watu wanapenda kujiburudisha kwa dansi na mtindo wao maarufu ni “Tango” unaochezwa na watu wa nne. Baba Mtakatifu anasema, anafurahia sana kuona jitihada za vijana katika michezo kwa sababu michezo ni furaha, inayomwezesha mchezaji kushirikisha mambo msingi yaliyomo ndani mwake na hatimaye, kumwezesha mchezaji kufikia hatua ya juu kabisa. Hizi ni jitihada zinazopaswa kudumishwa miongoni mwa vijana. Mwishoni, amewashukuru wachezaji hawa kwa ushuhuda wao katika medani ya michezo.

Papa: Michezo
20 January 2021, 14:59