Tafuta

Papa Francisko asema, "Neno Alifanyika Mwili" ni kiini cha Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane! Habari Njema ya Wokovu. Papa Francisko asema, "Neno Alifanyika Mwili" ni kiini cha Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane! Habari Njema ya Wokovu. 

Papa Francisko: Neno Alifanyika Mwili: Kiini Cha Injili ya Yohane

Kitabu cha Mwanzo kinasimulia pia kuhusu kazi ya uumbaji kwa kusema: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” Mwa. 1:1. Mwinjili Yohane anasimulia kwamba, yule ambaye waamini wamemtafakari wakati wa Sherehe ya Noeli, Neno wa Mungu, Kristo Yesu alikuwepo hata kabla ya nyakati. “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu”.Yn. 1:4.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili, baada ya Sherehe ya Noeli inafanya rejea si katika maisha ya Kristo Yesu, bali katika historia ya uwepo wake, kabla ya Fumbo la Umwilisho. Huyu ndiye Neno aliyekuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huu ni muhtasari wa Injili kama ilivyoandikwa na Yohane katika dibaji ya Injili yake. Hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu inayowaambata na kuwakumbatia watu wa nyakati zote. Ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Huyu ndiye Nuru halisi inayomtia nuru kila mtu na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuikwepa nuru hii. Ndiye Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Hii ni tafakari inayowarejesha waamini mwanzoni kabisa mwa kazi ya uumbaji Mwinjili Yohane anaposema: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno” Yn. 1:1. Kitabu cha Mwanzo kinasimulia pia kuhusu kazi ya uumbaji kwa kusema: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” Mwa. 1:1. Mwinjili Yohane anasimulia kwamba, yule ambaye waamini wamemtafakari wakati wa Sherehe ya Noeli, Neno wa Mungu, Kristo Yesu alikuwepo hata kabla ya nyakati. “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu”.Yn. 1:4. Kristo Yesu alikuwepo kabla ya kitu kingine chochote.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 3 Januari 2021 kutoka kwenye Maktaba ya Kitume mjini Vatican. Hapa Neno la Mungu linaonesha kwa namna ya pekee, ile nguvu ya mawasiliano inayofumbatwa katika jina la Yesu, Neno wa Mungu tangu milele yote. Hizi ni jitihada za makusudi kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu za kutaka kuwasiliana na waja wake, pamoja na kuzungumza nao. Kristo Yesu, Mwana pekee atokaye kwa Baba anataka kuwashirikisha watu wa Mungu ule uzuri wa kuwa waana wapendwa wa Mungu, Yeye ni “Nuru halisi” inayotambua maisha ya waja wake na kwamba Mwenyezi anawapenda watu wake upeo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ujumbe wa leo ni kwamba Yesu ni Neno wa Baba wa milele, anayewafikiria watoto wake na anayo nia ya kuwasiliana nao! Ili kuweza kutekeleza azma hii, Kristo Yesu ametenda kwa ujasiri na unyenyekevu mkuu “Naye Neno alifanya mwili, akakaa kwetu” Yn. 1:14.

Hiki ndicho kiini cha Injili ya Yohane. Mwinjili Yohane anatumia Neno “Mwili” kuonesha mwili wa binadamu, mapungufu pamoja na udhaifu wake; mahali ambapo kimsingi, mwanadamu anapaonea aibu sana. Neno wa Mungu akafanyika Mwili na kusonga mbele. Akauchukua udhaifu wa binadamu katika Fumbo la Umwilisho tangu wakati huo na kwa daima na hata kudiriki kukaa kati ya waja wake na kutembea nao katika hija ya maisha yao ya kila siku. Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho anasema Baba Mtakatifu Francisko anapenda kujenga na kudumisha mahusiano ya dhati kabisa, ili kuweza kushirikiana na Kristo Yesu nyakati za furaha, machungu, shauku, woga na wasi wasi. Kristo Yesu anataka kushirikiana na waja wake: matumaini, majonzi; kwa hakika anataka kushirikiana na watu pamoja na mazingira yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao, ili waweze kumkaribisha na kumpokea. Kristo Yesu anapowaombea mbele ya Mwenyezi Mungu, anamwonesha pia Madonda yake Matakatifu, kwani aliteseka, akafa na kufufuka ili kuwaokomboa kutoka katika dhambi na mauti.

Ni wakati wa kukaa kimya kwa kitambo kidogo mbele ya Pango la Mtoto Yesu, ili kuonja wema na huruma ya Mungu aliyeamua kuwa jirani, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Bila wasi wasi, woga wala makunyanzi, waamini wawe na imani na ujasiri wa kumkaribisha Kristo Yesu katika nyumba zao, ndani ya familia lakini zaidi katika udhaifu wa maisha ya kibinadamu. Kila mtu anafahamu fika udhaifu wake wa kibinadamu. Kristo Yesu atakuja na kwa hakika maisha yatabadilika. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria Mama wa Mungu, ambaye Neno wa Mungu alitungwa mimba ndani mwake, awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumkaribisha na kumpokea Kristo Yesu anayebisha hodi katika malango ya nyoyo zao, ili aweze kuishi pamoja nao.

Papa Neno wa Mungu
03 January 2021, 15:09