Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa matumaini watu wa Mungu nchini Venezuela ili kuonesha uwepo wake wa karibu katika mateso na mahangaiko yao kutokana na COVID-19 pamoja na umaskini. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa matumaini watu wa Mungu nchini Venezuela ili kuonesha uwepo wake wa karibu katika mateso na mahangaiko yao kutokana na COVID-19 pamoja na umaskini. 

Papa Francisko: Mshikamano wa Udugu wa Upendo na Venezuela

Wananchi wa Venezuela wanaendelea kuteseka kutokana na umaskini, gonjwa la Corona, COVID-19 pamoja na kiburi na jeuri ya viongozi, ambao wameendelea kujifungia katika ubinafsi wao. Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mwanga wa Mataifa, isaidie kuvunjilia mbali giza linaloendelea kutanda juu ya uso wa dunia. Baba Mtakatifu anamshukuru Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mèrida na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Caracas, aliyezaliwa kunako tarehe 10 Oktoba 1944 huko Caracas, nchini Venezuela, akawekwa wakfu kuwa Askofu tangu mwaka 1983 na kuteuliwa na hatimaye, kusimikwa na kuwa Kardinali mwaka 2016, amekuwa akipitia kipindi kigumu sana katika historia na maisha ya watu wa Mungu nchini Venezuela. Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mwanga wa Mataifa, hapo tarehe 6 Januari 2021, Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa kumtafuta na hatimaye kumsujudia Mwenyezi Mungu ni hija ya maisha ya kiroho, inayochukua muda mrefu hadi kufikia ukomavu wa maisha ya ndani. Hili si jambo rahisi sana, Kristo Yesu, kama Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ni Mungu kweli na mtu kweli.

Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa, katika ubinadamu wake, alipaswa pia kuabudiwa. Lakini, hapa kuna hatari kubwa ya kukosea lengo, kwani ikiwa kama mwanadamu anashindwa kumwabudu Mwenyezi Mungu ataishia kumwabudu, Shetani, Ibilisi pamoja na kuabudu miungu wengine na matokeo yake ni kutumbukia katika ibada ya kuabudu miungu wa kuchonga. Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo ujumbe wa matashi mema katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, kama kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini Venezuela ambayo imekumbwa na umaskini wa hali na kipato, hali inayogumishwa pia na madhara ya maambukizi makubwa ya ugonjwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu anamwombea heri na baraka, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aendelee kumtia nguvu, hekima na busara, ili aendelee kuwa na moyo wa kibaba katika kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu nchini Venezuela katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha yao. Wananchi wa Venezuela wanaendelea kuteseka kutokana na umaskini, gonjwa la Corona, COVID-19 pamoja na kiburi na jeuri ya viongozi, ambao wameendelea kujifungia katika ubinafsi wao. Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mwanga wa Mataifa, isaidie kuvunjilia mbali giza linaloendelea kutanda juu ya uso wa dunia. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa ushuhuda wa maisha na utume wa Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mèrida na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Caracas. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akiwa ameambatana pia na Askofu Mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, wameungana ili kuwatakia watu wa Mungu nchini Venezuela heri na baraka katika kipindi hiki cha Sherehe za Noeli na Mwaka Mpya 2021.

Papa: Venezuela

 

 

 

 

08 January 2021, 15:31