Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Kuhusu Wito: Wito wa kwanza: Maisha, Imani na Ndoa, Upadre au Maisha ya Kuwekwa Wakfu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko Kuhusu Wito: Wito wa kwanza: Maisha, Imani na Ndoa, Upadre au Maisha ya Kuwekwa Wakfu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. 

Papa Kuhusu Wito: Maisha! Imani: Ndoa, Daraja Takatifu Au Wakfu

Wito wa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni wito wa maisha unaomuunda mtu kama binadamu. Wito wa pili kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni Imani inayomfanya mwamini kuwa ni sehemu ya watoto wa familia ya Mungu. Mwenyezi anamwita mwamini katika wito maalum, ili aweze kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia; au katika wito wa upadre au maisha ya kuwekwa wakfu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Yohane Mbatizaji katika maisha na utume wake, alitangaza na kushuhudia Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi. Akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya, kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana.

Kristo Yesu alijionesha kama Mwanakondoo wa Mungu anayeichukua na kuiondoa dhambi ya ulimwengu. Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha Kristo Yesu kuwa ndiye Mwanakondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu! Hawa ndio akina Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu mwenyewe! Mitume wa kwanza wa Yesu waliyaamini maneno na utambulisho uliotolewa na Yohane Mbatizaji, wakaamua kumfuata naye Kristo Yesu akawauliza “Mnatafuta nini?” Nao wakamwambia, Rabi, maana yake, Mwalimu, unakaa wapi? Kristo Yesu hakutoa jibu la mkato kwamba anaishi maeneo gani, bali aliwapatia mwaliko kwa kusema, “Njoni, nanyi mtaona”.

Huu ni mwaliko wa kukutana na Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao, wakaamua kumfuata na kushinda kwake hadi saa kumi. Ulikuwa ni muda wa kumsaili, lakini zaidi muda wa kumsikiliza Kristo Yesu, kiasi cha kuwasha nyoyo zao kwa moto wa upendo. Ilikuwa imekwishagota jioni, lakini ndani mwao, kukachomoza mwanga ambao ni zawadi ya Mungu katika maisha yao, kiasi cha kuambizana, “tumemwona Masiha, maana yake Kristo! Hivi ndivyo Andrea alivyomwambia ndugu yake Simoni, ambaye baadaye alipewa jina la Kefa, tafsiri yake Petro, au Jiwe! Ni tukio ambalo liliacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo zao, kiasi hata cha kukumbukwa ile saa baada ya miaka sabini kupita. Mchakato wa kukutana na Kristo Yesu ni tukio linaloacha kumbukumbu hai na chemchemi ya furaha ambayo ilileta mabadiliko makubwa katika maisha yao.

Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyoichambua Injili ya Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kawaida cha Mwaka B wa Kanisa, Jumapili tarehe 17 Januari 2021 kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kukaa kidogo na kulitafakari tukio hili, ambalo Kristo Yesu, anawaalika Mitume wake wa kwanza, kukaa pamoja naye, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake. Mwenyezi Mungu anapenda kutoa mwaliko kwa ajili ya maisha, imani na wakati mwingine, huwaalika watu kwa ajili ya miito maalum katika maisha na utume wa Kanisa. Wito wa kwanza kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni wito wa maisha unaomuunda mtu kama binadamu, huu ni wito binafsi kwa sababu Mwenyezi Mungu hafanyi matoleo ya watu. Wito wa pili kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni Imani inayomfanya mwamini kuwa ni sehemu ya watoto wa familia ya Mungu.

Mwishoni, Mwenyezi Mungu anamwita mwamini katika wito maalum, ili aweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha ya ndoa na familia; au katika wito wa upadre au maisha ya kuwekwa wakfu. Hii yote ni miito na mitindo mbalimbali ya maisha inayopania kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya kila mwanadamu na kwamba, kimsingi huu ni mpango wa upendo. Furaha kubwa kwa kila mwamini ni kuhakikisha kwamba, anajibu wito huu na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na kwa jirani zake. Mwenyezi Mungu anatumia njia mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, wito wake unamfikia mlengwa. Mwenyezi Mungu anaweza kutumia watu, matukio yenye furaha au majonzi. Wakati mwingine, anasema Baba Mtakatifu Francisko mwamini anaweza kuukataa wito wa Mungu katika maisha yake, pale ambapo mwamini anadhani kwamba, wito huu unakwenda kinyume na matamanio binafsi; au wakati mwingine ni woga usiokuwa na mvuto wala mashiko, kwa kudhani kwamba, wito huo ni dhamana kubwa na pengine hauna “mashiko”.

Ikumbukwe kwamba, wito wa Mungu ni chemchemi ya upendo unaojibiwa kwa upendo. Mwanzoni kabisa kuna watu kukutana na Kristo Yesu anayesimulia kuhusu Baba yake wa mbinguni na hivyo kuwasaidia kufahamu na hatimaye, kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anasema, ile shauku ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa jirani inaibuka mara moja, kwa sababu mwamini amekutana na upendo na maana ya maisha. Kwa maneno machache kabisa ni kwamba, katika mchakato huu, mwamini amekutana na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuyageuza maisha yao, ili yaweze kuwa ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu mintarafu jibu la wito wa kutekeleza kwa dhati kabisa, kwa furaha na unyenyekevu wa moyo, mapenzi ya Mungu katika maisha! Kwa hakika kila mtu katika hija ya maisha yake, amekutana na Mwenyezi Mungu, akamwita kwa wito maalum. Hii ni fursa ya kuweza kufanya kumbukumbu ya tukio hilo, ili kuendelea kupyaisha mchakato wa kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya hapa duniani!

Papa: Wito

 

 

17 January 2021, 15:13