Tafuta

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa watu wa Mungu nchini Indonesia kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi pamoja na ajali ya ndege ya abiria. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha uwepo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa watu wa Mungu nchini Indonesia kutokana na maafa ya tetemeko la ardhi pamoja na ajali ya ndege ya abiria. 

Papa Francisko: Mshikamano wa Kidugu na Wananchi wa Indonesia

Tetemeko la ardhi lililotokea katika Kisiwa cha Sulawesi, nchini Indonesia hivi karibuni limesababisha watu 78 kupoteza maisha, watu 830 kujeruhiwa vibaya na wengine 200 wanaendelea na matibabu. Nyumba 415 zimeharibika vibaya na watu zaidi 15, 000 hawana makazi ya kuishi. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 17 Januari 2021 ameonesha uwepo wake wa karibu kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa richa 6.2 lililotokea hivi karibubi huko Magharibi mwa Kisiwa cha Sulawesi, nchini Indonesia limesababisha watu 78 kupoteza maisha, watu 830 kujeruhiwa vibaya na wengine 200 wanaendelea na matibabu. Nyumba 415 zimeharibika vibaya na watu zaidi 15, 000 hawana makazi ya kuishi. Ni katika muktadha huu, licha ya Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni kutuma salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa familia ya Mungu nchini Indonesia, Baba Mtakatifu, baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Januari 2021 ameonesha tena uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini Indonesia.

Hiki kimekuwa ni kipindi kigumu sana katika historia na maisha ya wananchi wa Indonesia kwani kuna watu wengi ambao wamepoteza maisha, wamepatwa majeraha, wamepoteza makazi na kazi. Baba Mtakatifu anapenda kuwaombea wote hawa, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika shida na mahangaiko yao. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea pia abiria 62 waliofariki dunia kwa ajali ya ndege ya Shirika la Sriwijaya Air. Ndege hii aina ya SJ 182 ilikuwa na wafanyakazi 12 na abiria 50, wakiwamo na watoto 10. Ajali ilitokea muda mfupi tu tangu ndege hiyo iliporuka kutoka katika Kiwanja cha Ndege cha Jakarta nchini Indonesia. Baba Mtakatifu amewaweka wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria msaada wa Wakristo!

Papa: Indonesia

 

18 January 2021, 15:12