Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Kardinali Ladaria Ferrer Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anafafanua sababu za kitaalimungu zilizopelekea kubadili sheria namba 230§1 Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Kardinali Ladaria Ferrer Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anafafanua sababu za kitaalimungu zilizopelekea kubadili sheria namba 230§1 

Papa Francisko: Usomaji na Utumishi Wa Wanawake Altareni: Sababu za Kitaalimungu

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini ambao ni viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa wanampokea Roho Mtakatifu kadiri ya utume wao ndani ya Kanisa. Hizi ni zawadi na karama za Roho Mtakatifu zinazowawezesha kulijenga Fumbo la Mwili wa Kristo, tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake binafsi, Motu Proprio “Spiritus Domini” yaani “Roho wa Bwana”: Utume wa Waamini Walei kutoka katika Ubatizo”, amefanya mabadiliko katika kanuni namba 230 kifungu cha 1 cha Mkusanyiko wa Sheria za Kanisa na hivyo kutoa ruhusa kwa wanawake kuweza kushiriki katika huduma ya usomaji na utumishi Altareni. Itakumbukwa kwamba, daraja dogo la usomaji (Msomaji, Lector) na utumishi Altareni (Akoliti, Acolyte) tangu mwaka 1972 yamekuwa yakitolewa kwa wanaume waliokuwa wanajiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu ya Upadre, hata kama madaraja haya madogo yalikuwa yanatolewa pia kwa wanaume waliokuwa na umri na sifa zinazofaa. Akoliti huwekwa rasmi ili kuhudumia altareni na kumsaidia kuhani na shemasi. Wajibu wake wa pekee ni kutayarisha Altare na vyombo vitakatifu. Na, ikiwa ni lazima, huwagawia waamini Ekaristi Takatifu. Msomaji huwekwa kwa ajili ya kusoma masomo ya Maandiko Matakatifu, isipokuwa Injili. Msomaji huweza pia kutaja nia za maombi kwa wote, na kusoma Zaburi ya kati ya masomo, ikiwa hakuna mwimba zaburi. Katika adhimisho la Ekaristi, msomaji ana kazi yake maalum.

Kwa Barua hii binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Spiritus Domini” yaani “Roho wa Bwana”: Utume wa Waamini Walei kutoka katika Ubatizo”, kuanzia sasa wanawake wenye sifa wanaweza kupewa daraja dogo la usomaji na utumishi Altareni. Hii ina maana kwamba, wanaweza kusaidia kugawa Ekaristi Takatifu. Madaraja haya yatatolewa katika Ibada. Uamuzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Utume huu wa waamini walei unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na unatofautiana na huduma ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu Francisko ameambatanisha na Barua aliyomwandikia Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu sababu msingi za kitaalimungu zilizopelekea hadi akafikia uamuzi huu. Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu, mahusiano ya upendo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu hujenga ushirikiano na uelewano wa watu wa Mungu.

Roho Mtakatifu ni kiunganishi cha mapendo kati ya Baba na Mwana. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini ambao ni viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa wanampokea Roho Mtakatifu kadiri ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Hizi ni zawadi na karama za Roho Mtakatifu zinazowawezesha kulijenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa tayari kutoka kimasomaso ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mtakatifu Paulo, Mtume, anatofautisha kati ya karama “charismata” na huduma “diakonia”. Kumbe, ndani ya Kanisa kuna karama na huduma. Daraja Takatifu ni Sakramenti ya Huduma ambayo imegawanyika katika madaraja makuu matatu yaani: Daraja ya Ushemasi, Upadre na Uaskofu. Baadhi ya huduma zinazotolewa na Mama Kanisa zinatekelezwa na waamini walei kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa hata pengine bila ya kutambuliwa rasmi. Kuna utume unaotekelezwa na waamini walei pamoja na huduma inayofanywa na waamini waliodarajiwa!

Mashemasi, Mapadre na Maaskofu ni wahudumu wa: Neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa na Huduma ya upendo. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri na kusema kwamba Kristo Bwana ndiye Kuhani Mkuu. Kumbe, Ukuhani wa waamini wote na ukuhani wa kidaraja ingawa huhitilafiana kadiri ya kiini chake na siyo kadiri ya cheo, huelekezana kati yake kwa sababu zote mbili, na kila mmoja kwa namna yake, hushiriki ukuhani mmoja wa Kristo. Re. LG. 10. Mtakatifu Paulo VI akifanya rejea katika huduma hii kwa Kanisa Katoliki, aliyaita madaraja haya kuwa ni “Madaraja madogo” na kufafanua shughuli na malengo yake. Madaraja ya Huduma ya Neno na Utumishi Altareni. Huduma zote hizi lazima zilenge katika kujenga na kukuza umoja wa Kanisa kwa kuishi kiliturujia, huduma kwa maskini, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, waamini walei ni sehemu kubwa kabisa ya Taifa la Mungu. Wale walio wachache wahudumu wenye Daraja Takatifu ni watumishi wao. Hadhi na utume wa walei vimekuwa vikiendelea kutambuliwa zaidi katika Kanisa. Dhamana na utume wa waamini walei unapata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Waamini walei wanapaswa kufundwa zaidi ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili. Wahudumu wa Altareni kwa kutambua tofauti ya majukumu waliyo nayo, wote kwa pamoja wanapaswa kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anakuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na wote wakitembea kwa pamoja kama jumuiya ya waamini.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika tafakari yao kuhusu Kanisa katika ulimwengu mamboleo wanakazia umuhimu wa Kanisa lililopo katika ulimwengu na linaloishi na kutenda kazi pamoja na walimwengu, ndiyo maana ya Kanisa kutoka kuwaendea watu wa Mataifa! Kwa upande wao, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia walitilia mkazo pia umuhimu wa kutambua dhamana na utu wa wabatizwa wote ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Verbum Domini” alisema kwamba, Daraja dogo la Usomaji ni huduma ya waamini walei. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, pamoja na mabadiliko yote haya, lakini Mama Kanisa hana nia ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa wanawake, kama alivyowahi kutamka Mtakatifu Yohane Paulo II. Mama Kanisa anapenda kuendelea kuwa mwaminifu kwa Kristo Yesu pamoja na kuendelea kutia nia ya kuishi, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyotangazwa na Mitume pamoja na waandamizi wao, ili kweli, Kanisa liweze: kulisikiliza, kulihifadhi kitakatifu na kulitangaza kiaminifu. Mama Kanisa anataka kumtumikia Mungu na watu wake kwa uaminifu mkubwa.

Mabadiliko haya yanapania pamoja na mambo mengine, kuwahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na maamuzi muhimu katika maisha ya jamii wanamoishi. Ukuhani wa Ubatizo na Ukuhani wa Daraja ni muhimu kwa ajili ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kwa muda wa miaka mingi wanawake wamekuwa wakitoa huduma ya usomaji wa Neno la Mungu na Utumishi Altareni kwani yote haya yanapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa sasa ni jukumu la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia kutoa vigezo muhimu vitakavyotumika katika kufanya mang’amuzi na hatimaye, maandalizi ya wale wanaotaka kujisadaka katika huduma ya Neno na Utumishi wa Altare, kwa kupata kibali kutoka Vatican baada ya kuzingatia mahitaji ya uinjilishaji katika Makanisa mahalia. Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa limepewa wajibu wa kufanya marekebisho kuhusu huduma ya Usomaji na Utumishi Altareni kwenye “Pontifikale ya Kiroma” Huduma ya Akoliti na Msomaji waliowekwa rasmi.

Spiritus Domini

 

13 January 2021, 13:53