Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa na ajali iliyotokea mjini Madrid, Hispania na kusababisha watu 4 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 11 kupata majeraha makubwa. Baba Mtakatifu Francisko asikitishwa na ajali iliyotokea mjini Madrid, Hispania na kusababisha watu 4 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 11 kupata majeraha makubwa.  (AFP or licensors)

Papa Francisko Asikitishwa na Ajali Iliyotokea Mjini Madrid, Hispania

Papa Francisko asikitishwa na janga la moto lililotokea tarehe 20 Januari 2021 huko Madrid na kusababisha watu 4 kupoteza maisha na wengine 11 kupata majeraha makubwa. Kati ya waliofariki dunia ni Padre Rubén Pérez Ayala, mwenye umri wa miaka 36 kutoka Jimbo kuu la Madrid aliyekuwa ameangukiwa na kifusi cha nyumba ya ghorofa tatu iliyoungua na hatimaye, kuporomoka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na taarifa za janga la moto lililotokea tarehe 20 Januari 2021 huko Madrid, Hispania na kusababisha watu 4 kupoteza maisha na wengine 11 kupata majeraha makubwa. Kati ya waliofariki dunia ni Padre Rubén Pérez Ayala, mwenye umri wa miaka 36 kutoka Jimbo kuu la Madrid aliyekuwa ameangukiwa na kifusi cha nyumba ya ghorofa tatu iliyoungua na hatimaye, kuporomoka. Baba Mtakatifu katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kutumwa kwenda kwa Kardinali Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania, anasema, anawaombea wote waliopoteza maisha yao na anawaombea majeruhi ili waweze kupona haraka na kurejea tena katika shughuli za ujenzi wa nchi yao.

Wote hawa, Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa “Almudena”. Akiwa na matumaini ya Kikristo katika ufufuko, uzima na maisha ya milele, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za Kitume kwa wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Wakati huo huo, Kardinali Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid amempongeza Marehemu Padre Rubén Pérez Ayala, kwa maisha na majitoleo yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni Padre kijana sana, ambaye amefariki dunia, takribani miezi saba tu, tangu alipowekwa wakfu kuwa Padre. Katika Ibada ya Misa ya Shukrani, alikua amewaalika waamini kujiaminisha na kumwangalia Kristo Yesu ambaye ni chemchemi ya furaha ya kweli na amani kwa ajili ya watu wake.

Maafa Madrid
21 January 2021, 15:11